Mrisho na mpira wake baada ya
kufunga mabao matano

Na  Mahmoud Zubeiry, Kampala
TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars imefuzu kuingia Robo Fainali ya michuano ya CECAFA Challenge, baada ya kuilaza Somalia mabao 7-0 katika mchezo uliofanyikakwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa.
Matokeo hayo yanaifanya Bara itimize pointi sita baada ya kucheza mechi tatu, wakishinda mbili na kufungwa moja.
Stars ilionyesha kandanda safi na kusisimua mashabiki wa Tanzania waliokuja kuoiunga mkono hapa, akiwemo Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Alhaj Juma Nkamia.
Iliwachukua sekunde 48 tu Stars kupata bao la kwanza, kupitia kwa mshambuliaji wa Simba SC, Mrisho Khalfan Ngassa aliyewazidi ujanja mabeki wa Somalia.
Kabla hawajakaa vizuri, Somalia walipachikwa bao la pili, dakika ya 23 lililofungwa na Ngassa tena, aliyeunganisha kona nzuri ya Issa na Rashid.
John Bocco ‘Adebayor’ alifunga bao la tatu katika mchezo wa leo na la tatu kwake katika mashindano haya dakika ya 26 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Issa Rashid kutoka wingi ya kushoto.
Bocco tena aliwainua vitini mashabiki wa Tanzania kwa kufunga bao la nne kwa kichwa, akiunganisha krosi ya Ngassa dakika ya 41.
Ngassa alifunga bao la tatu katika mchezo wa leo dakika ya 44 na la tano kwa Stars baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Hussein Abdallah kufuatia shuti kali la Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’
Somalia ilipata pigo dakika ya 30, baada ya kipa wake namba moja, Mohamed Abdullah kuumia baada ya kugongana na Bocco na kutoka, nafasi yake ikichukuliwa na Hussein Abdallah. 
Kipindi cha pili Stars walirejea na moto wao na tena na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi yaliyotiwa kimiani na Ngassa yote dakika za 73 pasi ya Erasto Nyoni na 74 pasi ya Ramadhani Sinago ‘Messi’.
Kwa kufunga mabao matano, Ngassa sasa ameingia kwenye mbio za kaiti cha dhahabu akikwa anaongoza, akifuatiwa na Bocco ambaye ana manne hivi sasa.
Kocha wa Stars, Mdenmark Kim Pouslen baada ya mchezo huo, alisema aliwapongeza vijana wake kwamba wamejitahidi kucheza vizuri na akasifu pia hali nzuri ya Uwanja wa Lugogo kuwa ilichangia ushindi huo.
Mbunge Nkamia alisema kwamba amevutiwa na soka ya vijana leo na anaamini wana uwezo wa kurejea na Kombe nyumbani. Nkamia aliwapongeza wadhamini wa Stars kwa kuchangia mafanikio ya timu hiyo tangu waanze kuidhamini na akaomba Watanzania zaidi wajitokeze mjini hapa kuisapiti timu hiyo.
Waandishi wa Habari waliopo mjini hapa pia wamevutiwa mno na kiwango cha timu hiyo na kusema wana wana imani itafika mbali.
Wallace Karia, Mjume wa Kamati ya Utendaji ya TFF aliye hapa Uganda amesema amefurahishwa na kiwango cha timu na anaamini itafika mbali.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa Kilimanjaro Stars, George Kavishe ametuma salamu za pongezi kwa ushindi wa leo na mafanikio ya kutinga Robo Fainali na kusema anatakia mafanikio zaidi timu hiyo.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Kevin Yondan/Ramadhani Singano, Shaaban Nditi, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco/Christopher Edrwad, Frank Domayo/Athumani Iddi na Amri Kiemba.
Somalia; Mohalim Abdullahi/Hussein Abdallah dk30, Ali Mohamed, Said Mahamud, Ali Dadir, Sadaq Abdikadir, Mohamed Salah, Abdikarim Abubakar, Abdallah Mohamed/Hamza Mukhtar, Ahmed Abdikadir Dahir/Muhad Hajji na Ali Ahmed Ali.  
Katika mchezo mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa Nankurunkuru, Burundi ilishinda 1-0 bao hivyo kuongoza Kundi B baada ya kufikisha pointi tisa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hayo ndiyo mambo tunayotaka kusikia,kutoa dozi za ukweli.Rwanda nao wapewe dozi yao.Naomba fainali tukutane na MALAWI!Hongera sana vijana.

    David V

    ReplyDelete
  2. hahahahaha eti majisifu yote haya kumbe mmewafunga somalia hahaaha

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...