Na Mwandishi Wetu

Familia ya mdogo wake Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  Marehemu Joseph Nyerere, imejitokeza na kusema haimtambui mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, anayejitambulisha kwa jina la Makongoro Joseph Nyerere.

Taarifa iliyotolewa na Nuru Nyerere-Inyangete, kwa niaba ya familia hiyo jana, ilisema hadi kifo cha baba yao, Joseph Kizurira Nyerere, mwaka 1994 haina taarifa zozote za kuwa na ndugu yao anayeitwa Makongoro Joseph Nyerere.

“Hadi baba anafariki dunia hatukuambiwa tuna ndugu anayeitwa Makongoro Joseph Kizurira Nyerere …watoto wote wa Mzee Joseph tunafahamiana, lakini kwa huyu ndiyo kwanza tunaambiwa kuwa ni ndugu yetu. Tunauhakikishia umma kwamba hadi kifo cha baba yetu hatukuambiwa juu ya kuwapo kwa ndugu mwenye jina hilo; hii ina maana kwamba hatumtambui,” alisema Nuru.

Naye mtoto mwingine wa Joseph, Matare, alisema, “Tangu kutangazwa kwa habari hizi tunapata simu nyingi za pole. Tunashangaa kwa sababu huyu mtu hatukuwahi kuambiwa kuwa ni ndugu yetu, na wala yeye mwenyewe hakuwahi kuja kwetu kujitambulisha kama ni mmoja wa watoto wa Mzee Joseph.”

Matare aliongeza, “Tumesoma kwa mshituko kwenye magazeti ya Februari 14, 2013 na katika mitandao ya kijamii, kuwa kuna mtu anayejiita Makongoro Joseph Nyerere. Huyu huyu hatumtambui kwa uhusiano, taarifa wala sura. Watoto wote wa marehemu Joseph Nyerere wanafahamika, hakuna mtoto wa marehemu mwenye jina hilo.”
Juzi, Makongoro ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo akikabiliwa na mashitaka ya mauaji ya mfanyabiashara mwenzake, Onesphory Kitoli. Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kuunganishwa katika kesi hiyo na mtuhumiwa mwingine mfanyabiashara maarufu, Marijani Abubakari marufu kama Papaa Msofe (50). Kesi hiyo itatajwa Februari 20, mwaka huu.

Wakili wa Serikali, Charles Anindo, alimsomea Makongoro mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome, na kudai kuwa Novemba 6, 2011 huko Magomeni Mapipa, Makongoro alimuua kwa makusudi Kitoli kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Anindo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Februari 20, mwaka huu, ambako Makongoro ataunganishwa na Papaa Msofe kwenye mashitaka hayo.

Mtuhumkiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. pimeni DNA. ka kweli karibu.

    lakini m sikane tu kwa kuwa ana kesi.

    ReplyDelete
  2. Tafadhali fanya marekebisho kwenye mwaka aliofariki baba wa Taifa. Hakufariki 1994 bali ni 1999.

    ReplyDelete
  3. Siyo lazima muambiwe ya kwamba mna ndugu yeni, msikane mtu hutyu bila kufanya uchambuzi bayana, maana mnaweza kuja oana ndugu, kama si ninyi watoto wenu au watoto wa watoo wenu, hivyo fanyeni uchunguzi kwanza.

    ReplyDelete
  4. Mi ningeshauri wampime DNA. Mara nyingi DNA haidanganyi.

    ReplyDelete
  5. Never say never!

    ReplyDelete
  6. Hamna haja ya kupima DNA wala nini huyo ni ndugu yao na wanamjua vizuri leo hii kwasababu ana kesi ndo maana wanakmana

    ReplyDelete
  7. huyu bwana makongoro hivi sasa ana kesi mbaya ya kuuwa iko haja ya kumkana kwa nguvu zote nafikiri ingelikuwa ameshinda bahati nasibu ya hela nyingi ingelibidi wana familia wamkumbatie kwa hali yoyote ile na kumkaribisha kwenye familia kwa ngoma na vifijo na DNA wangelipiga marufuku isitumike huenda wangelitumia mganga wa kienyeji kuhalalisha undugu.
    mdau.
    mahakamani dar.

    ReplyDelete
  8. Ah kazi kweli kweli, ama kweli Dunia ikikuangukia mara nyingi unakuwa upo peke yako!

    ReplyDelete
  9. Hili ni tatizo kubwa sana na sio siri sio rahisi kupata jibu la haraka haraka.

    Ukiacha hii ya Makongoro Joseph Nyerere-TANZANIA, pana mkasa wa Etienne Kabila (KONGO-DRC) ambapo huyo Etienne anadai ni mtoto wa Hayati Raisi Laurent Kabila , yaani baba yake Joseph Kabila Raisi wa sasa Kongo-DRC!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...