28/2/2013
Kina mama wajawazito wametakiwa kuhudhuria kliniki mapema pale
wanapojitambua kuwa na ujauzito hii itawasaidia kupata huduma mbalimbali
za afya ikiwa ni pamoja na kupima afya zao na kuona kama
wanambaambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) au la na hivyo kujifungua
salama mtoto asiye na maambukizi ya ugonjwa huo.
Kauli
hiyo imetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
alipokuwa akiongea na wananchi wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa wakati
akikabidhi pikipiki 10 za programu ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya
Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) zilizotolewa kwa
ufadhili wa Walter Reed HIV/AIDS Program.
Mama Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema
kuwa Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa afya wanahangaika
kuhakikisha kuwa watoto watakaozaliwa hawana maambukizi ya VVU kwani
dawa za kuzuia maambukizi zipo ni jukumu la kina mama kuhudhuria kliniki
mapema na kupima afya zao.
“Janga la Ukimwi ni tatizo kubwa kwa jamii yetu. Natoa Rai kwa wananchi wote tuwe waangalifu kujikinga na ugonjwa huu. Kutokana na takwimu zinaonyesha kuwa hali ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) kwa Mkoa huu ni 5.6% hivyo basi uwepo wa baba unatakiwa ili kuboresha afya ya mama na mtoto”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwaasa wote waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Na kuwakumbusha kuwa pikipiki hizo ni kwa
ajili ya ukusanyaji wa sampuli za damu kutoka vituo vilivyo mbali zaidi
na wilaya na kuvipeleka kwenye Maabara ya Kanda na pia kuimarisha
mawasiliano kati ya kituo na kituo na si vinginevyo.
Akisoma taarifa ya
mradi huo Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Rukwa Dk. Shadrack Mtulla
alisema kuwa wana vituo vya kutolea huduma za afya 267 kati ya hivyo
177 vinatoa huduma PMTCT ambavyo ni sawa na asilimia 66 ya vituo vyote na
kipindi cha mwaka 2012 jumla ya akina mama 3189 waliandikishwa katika
vituo vya kutolea huduma na malezi yaani CTC na kupewa dawa za ARV.
Alisema
kuwa , kwa kushirikiana na Walter Reed HIV/AIDS Program katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kipindi cha mwaka 2012/2013
wamenunua pikipiki 10 ambazo zitagawanywa katika vituo vya afya ambavyo viko mbali na makao makuu ya wilaya katika wilaya zote za mkoa huu.
Dk.
Shadrack Mtulla alisema, “Upatikanaji wa pikipiki hizi utarahisisha
ukusanyaji wa sampuli za damu kutoka vituo vilivyopo mbali zaidi na
wilaya, na kuzileta katika maabara tayari kwa kuzisafirisha kwenda
katika maabara za kanda pia zitaboresha mawasiliano kati
ya kituo na kituo na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa takwimu kutoka
vituo mbalimbali kwa muda uliopangwa”, Dk. Shadrack Mtulla.
Dk. huyo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu mkubwa wa vyombo vya usafiri hususani magari kwani mkoa huo una magari mawili na mahitaji halisi ni sita,
upungufu wa wataalamu wa afya vituoni ,watumishi walioko katika vituo
vya kutolea huduma ni asilimia 35 na upatikanaji wa vitendanishi
usiokidhi mahitaji ya mkoa na wilaya zake.
Pikipiki
hizo zilikabidhiwa kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ya
Sumbawanga tatu kwa ajili ya vituo vya Afya vya Milepa, Kasanga na
Mwitu, Nkasi mbili kwa ajili ya vituo vya afya Kirando na Kilangalanga,
Manispaa ya Sumbawanga mbili ambazo zitatumika katika vituo vya afya vya
Ntembo na Ulinji, Mji wa Mpanda moja kwa ajili ya kituo cha Afya
Mwangaza na wilaya ya Mpanda ambazo zitatumika katika vituo vya afya
Mamba na Mishano.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...