Kaimu Rasi Mkoa wa Iringa Ndg Wamoja Ayubu akiwa na washiriki wa mafunzo kazi kwa watumishi wa afya chini ya mradi wa Mkapa Fellows
Kaimu Rasi Mkoa wa Iringa Ndg Wamoja Ayubu akifungua mafunzo kazi kwa watumishi wa afya chini ya mradi wa Mkapa Fellows

SERIKALI imewataka wakurugenzi wa halmshauri za wilaya nchini, kutowabagua wala kuwatenga waajiriwa wapya wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation, ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya vijijini.

Waajiriwa hao 32, kupitia mradi wa Mkapa Fellows wanatarajiwa kupelekwa kwenye vituo mbali mbali katika wilaya sita nchini, kwa lengo la kuongeza nguvu ya utoaji wa huduma za afya katika kitengo cha ukimwi na huduma za uzazi salama.

Akifungua mafunzo kazi kwa waajiriwa hao, wakurugenzi wa wilaya, waganga wakuu wa mikoa na wilaya yaliyofanyika katika chuo cha afya, Kaimu Katibu tawala wa mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alisema ni jukumu la serikali kuhakikisha watumishi hao wanaandaliwa mazingira mazuri kazini ili kuboresha huduma za afya.

“Hawa watumishi wapya watakuwa katika ajira ya miezi 18 baadae, halmshauri za wilaya lazima muandae mikakati mizuri ya kuwaajiri kwenye wilaya zenu, msiwabague wala kuwatenga zaidi muone namna gani mnaweza kuwapa ushirikiano ili kuimarisha huduma za afya,” alisema Ayubu.

Aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza pengo la uhaba wa watumishi wa sekta ya afya ambalo linaikabili serikali.

Awali, Meneja mradi huo Dk Zuweina Kondo akisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Afisa mtendaji mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Dk Ellen Mkondya alisema mradi huo unalenga kuimarisha huduma za ukimwi na afya ya mama na mtoto katika maeneo ya vijijini.

Alisema mradi huo wa awamu ya pili utatekelezwa kwa  miaka mitano na kusaidia kuboresha huduma za afya kwa kuajiri wataalamu wa afya 150, makatibu wa afya 30, kujenga vyumba 30 vya upasuaji sambamba na kuweka vifaa vyake.

Dr Senkoro aliongeza kuwa wamefanikiwa kuanza kutekeleza mradi huo kwa ufadhili wa mashirika mbalimbali, taasisi, kampuni na watu binafsi ambapo walifanya harambee na kupokea ahadi za jumla ya Sh.3.2 bilioni ili kufanikisha hatua ya kwanza ya mradi.

Alifafanua kuwa mradi wa Fellows utatekelezwa katika hatua mbili, ambapo hatua ya kwanza itakuwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2014, na hatua ya pili itakuwa kuanzia mwaka 2015 hadi 2017.

Katika hatua ya kwanza ambayo iliyoanza mwaka huu, wataalamu  32 wameajiriwa na kwenda kufanya kazi katika vituo vya afya tisa kwenye wilaya sitaza Sumbawanga Vijijini, Nkasi, Kalambo, Kahama, Kishapu na Biharamulo.

Kwa upande wao, waajiriwa hao walisema uwepo wa taasisi hiyo utasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi na kuboresha huduma za afya, lakini pia kuongeza fursa za ajira.

Kwa awamu ya kwanza Taasisi hiyo ilifanikiwa kuajiri watumishi wa afya 90, ambao baada ya ajira zao kumalizika wameajiriwa na serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...