Azim Dewji
Na Mwandishi Wetu
MWANAMICHEZO aliyewahi kuifadhili Simba na pia kumiliki timu ya Ligi Kuu ya soka nchini, Azim Dewji ameingilia katika suala la mgogoro wa Katiba ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), akisema ni bora Tanzania ikafungiwa na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kuliko kuyumbishwa na Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga.


Dewji aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, huku akimtaka Tenga kuwa na msimamo katika maamuzi yake. Alisema kuwa, Tenga akiwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa tayari kuona Tanzania inafungiwa na FIFA, kuliko kuacha soka la nchi hii liendeshwe kiholela.


“Sasa kama wakati ule alitaka tufungiwe, kwa sasa anaogopa nini na kuanza kubishana na Serikali?

“Kwa maoni yangu, ni bora tufungiwe lakini tusiendeshwe na FIFA…Tanzania ina Serikali na ndiyo inayosimamia michezo, kwa hili sioni sababu ya TFF kuitunishia msuli serikali. Hii ni nchi, haiwezi kutishwa na taasisi tu ya soka ya kimataifa ambaye Tenga mwenyewe
aliwahi kukaririwa miaka ya nyuma akisema ina genge la wahuni…,” alisema Dewji.


TFF imejikuta ikiingia katika mgogoro na Serikali baada ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuingilia kati suala la mgogoro wa uchaguzi ndani ya TFF kwa kuagiza kufutwa kwa matumizi ya Katiba ya shirikisho hilo ya mwaka 2012, kwa kuwa imekiuka Kanuni na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT).


Waziri huyo aliiagiza TFF kufuata utaratibu wa kurekebisha Katiba za vyama vya michezo, kwa mujibu wa Sheria ya BMT iliyotungwa na Bunge pamoja na Kanuni zake ambazo ziko wazi na rahisi kuzifuata.


Hata hivyo uamuzi huo wa Waziri, ulipingwa na Tenga pamoja na Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, ambapo Tenga ameomba kuonana na Waziri akidai amepotoshwa na wasaidizi wake na uamuzi wake unaweza kulitia soka la Tanzania katika matatizo.


Tenga alidai Serikali na BMT vimeachana na kuingilia masuala ya soka tangu mwaka 2004 na ndani ya Katiba hiyo kuna utaratibu mzima ambao unaonesha namna ambavyo TFF inapaswa kufanya uamuzii wake kama chombo huru. Hata hivyo, kisheria Katiba ya TFF lazima isajiliwe serikalini.


Awali TFF iliomba kukutana na Waziri na ikafanya hivyo, lakini shirikisho hilo limeomba tena kukutana na Waziri Mukangara kwa madai kuwa katika kikao cha awali Tenga hakuwepo badala yake walienda watendaji, hivyo ni vyema kikafanyika kikao hicho ili kumpa ufafanuzi
wa baadhi ya mambo kwa nia ya kulimaliza jambo hilo.


Katika kikao hicho cha awali, Serikali iliitaka TFF kuitisha mkutano wa katiba ndani ya siku 40 na baada ya hapo kuitisha uchaguzi ndani ya siku kama hizo na pia imeitaka kutoa taraifa kwa wanachama wake kuhusu mkutano huo ndani ya siku tano tangu siku walipokutana.


Uamuzi wa Dk  Mukangara ulikuja siku chache kabla ya timu ya maofisa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuja nchini kufuatilia mgogoro ulioikumba TFF na wadau wake kutokana na masuala mbalimbali ya uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu. Ujumbe wa FIFA haukuja badala yake shirikisho hilo limetuma barua ya kutishia kuifungia Tanzania kama itathibitika serikali inaingilia masuala ya soka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. "kwa maoni yangu, ni bora tufungiwe kuliko kuendesha na FIFA..." alisema dewji
    ahhh mashindano yote ya kimataifa yako chini ya FIFA. Vyama vyote vya michezo vya mabara yote yako chini ya FIFA na yanaendeshwa kwa mujibu wa katiba za FIFA, toka shirika la mpira la nchi, bara na dunia kwa ujumla.

    Sasa bwana dewji anaposema tusiendeshwe na FIFA ana maana tujitoe katika mashindano yote ya kimataifa (vilabu na timu za taifa)?

    Dewji na wengine wakumbuke kuwa hata CAF haina nguvu mbele ya FIFA. FIFA wakiifunguia Tanzania ina maana hatutoweza kushiriki mashindano yeyote nje ya Tanzania.

    Tatizo ni kuwa moja ya msingi mkuu wa FIFA ni kuwa wanachama wake wote ni lazima wawe wanaongoza michezo katika nchi zao bila ya kuingiliwa na serikali za nchi zao. kinyume chake ni kuvuliwa uanachama. Tanzania hatuwezi kubadili msingi huo, England, France na hata Nigeria walijaribu katika nyakati tafauti na walishindwa.

    Kama tuko tayari kuwa tushirikishi mashindano yeyote nje ya nchi daima basi ni sawa, lakini siku yeyote ile tukitaka kurudi tena kuwa wanachama, sheria ile ile tutaikabili, TFF haitakiwi kuendeshwa na serikali

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...