WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekutana
na wakuu wa taasisi za kimataifa za WFP, IFAD na FAO na kufanya nao mazungumzo
kuhusu namna ya kuendeleza kilimo nchini Tanzania.
Waziri Mkuu amekutana na viongozi
hao Alhamisi (Machi 21, 2013) alipowatembelea kwenye ofisi zao jijini Roma,
Italia kila mmoja kwa nyakati tofauti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Mpango wa Chakula
Duniani (WFP), Bi. Ertharin Cousin, alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika lake
litaendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam kusafirishia vyakula kwenda nchi
zenye uhitaji wa chakula ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa bidhaa
kwa maendeleo (Purchase for Progress Programme).
“Tumekubaliana na wadau
tunaoshirikiana nao, tuendelee kutumia bandari ya Dar es Salaam kupeleka mizigo
Sudan ya Kusini na Uganda kwa sababu ya amani iliyopo nchini Tanzania. Kwa hiyo
muamini kwamba sisi ni wadau wenu wa karibu na wa kuaminika,” alisema Bi. Cousin.
Akitoa
mfano, Bi. Cousin alisema: “Kuna wakati kulikuwa na njaa kubwa kule Somalia na
Zambia wakawa na hifadhi kubwa ya mahindi, lakini tulishindwa kusafirisha mahindi
kutoka huko na kuyapeleka yanakohitajika kwa sababu ya hali mbaya ya usalama kwenye
ukanda wa magharibi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa miji
na kasi ya watu kuhamia mijini, Bi. Cousin alionya kwamba kuna haja ya
kuwianisha uendelezaji wa miundombinu kwenye maeneo ya mijini na yale ya
vijijini ili kuepuka tatizo la msongamano mkubwa wa watu mijini linalozikabili
nchi nyingi zinazoendelea.
Alisema shirika lake limefanya utafiti
nchini India na kubaini kuwa kadri kiwango cha ukuaji wa miji kinavyoendelea
ndivyo kasi ya wakazi kuongezeka inavyozidi. “Tumeziainisha nchi za Kenya,
Tanzania na Ethiopia na kuziweka kwenye mpango maalum ili zijipime jinsi
zitakavyokuwa katika miaka 20 ijayo ili zisije kuwa na hali kama ya India hivi
sasa,” aliongeza.
Naye, Rais wa Shirika la Kimataifa Kuendeleza Kilimo na Chakula
(IFAD), Dk. Kanayo Nwanze alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika lake limeandaa
mpando wa miaka mitatu ambao utazihusisha nchi 30 ikiwemo Tanzania ambazo
zitafanyiwa impact evaluation
kulingana na misaada ambayo zimekuwa zikipatiwa na shirika hilo.
“Tunataka tuangalie hali halisi
kule Vijijini, je maisha ya wananchi yamebadilika kulingana na misaada ambayo
tumekuwa tukiitoa? Je, wakulima wameongeza uzalishaji? Je wakulima
wameunganishwa na masoko? Je, taasisi za kifedha zinawajali wakulima wadogo?”
alifafanua Rais huyo wa IFAD.
Alisema hivi sasa wameanza
kukusanya takwimu za awali (baseline data) katika nchi husika kabla ya kuanza
kufanya tathmini itakayoanza mwaka huu hadi mwaka 2016.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja
wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Bw. Jose Graziano da Silva alimweleza
Waziri Mkuu kwamba shirika lake limetiliana saini makubaliano na benki ya Rabo
(Rabobank) ili iweze kuwasaidia wakulima waliojiunga kwenye vyama vya ushirika.
“RaboBank
imekubali kufanya kazi hiyo na imeichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi
zitakazokuwa waanzilishi wa mpango huo (pilot
project)… watawasiliana nanyi muda si mrefu kuhusiana na suala hili,”
alisema.Aliomba
wakati mpango huo utakapoanza, wakulima wa Tanzania wawe tayari kushiriki
kwenye mpango huo.
Waziri
Mkuu Pinda kwa upande wake, katika nyakati tofauti aliwaarifu wakuu wa taasisi
hizo za kimataifa juu ya hali ya uchumi wa Tanzania, Mpango wa Kuendeleza Sekta
ya Kilimo (ASDP), Ukanda wa Kilimo wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) na mchakato
wa kuandaa Katiba mpya.
Alisema ili kuendeleza kilimo, ipo
haja ya kushirikiana na wadau kutoka sekta binafsi kama njia ya kuleta maendeleo
ya haraka nchini Tanzania. Bado tunayo changamoto ya kukabiliana na umaskini,
lakini tunaamini kuwa kilimo ndiyo jawabu la tatizo hili,” alisema.
Waziri Mkuu alikwenda Roma, Italia
kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada maalum ya kumsimika Papa
Francis iliyofanyika Jumanne, (Machi 19, 2013) kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la
Mt. Petro mjini Vatican, kisha akaamua kukutana na viongozi wa taasisi hizo.
Waziri Mkuu alirejea nchini Ijumaa, Machi 22, 2013).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
JUMAMOSI, MACHI 23, 2013.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...