SIMBA SPORTS CLUB
P.O.BOX 15318 | TEL+255 222183330 |FAX +255 222183330 |MSIMBAZI/MCHIKICHI STREET | DAR ES SALAAM | TANZANIA | EMAIL  simbasportsclub@yahoo.com|WEBSITE www.simba.co.tz| AFFILIATED TO TFF, DRFA and IDFA
                                                                                                                  15/04/2013
                          TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KLABU ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwa vyombo vya habari siku ya leo, Jumatatu, Aprili 15, 2013.
KUHUSU TIMU
MARA baada ya mechi ya jana dhidi ya Azam FC, wachezaji wote wa Simba walipewa mapumziko ya siku mbili (leo na kesho) na timu itaanza tena mazoezi keshokutwa Jumatano asubuhi katika viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wamepewa mapumziko hayo kutokana na kutumika kwa kipindi kirefu mfululizo tangu timu ilipokwenda katika mikoa ya kanda ya ziwa na kambini Bamba Beach jijini Dar es Salaam.
Ni matarajio ya uongozi na benchi la ufundi kwamba wachezaji hao wataanza mazoezi wakiwa na nguvu mpya na tayari kwa changamoto ya mechi nne zilizobaki kumalizia Ligi Kuu ya Tanzania.
Uongozi wa Simba unawaomba wapenzi na wanachama wake kuendelea kuisapoti timu yao kwa namna ileile waliyoionyesha katika mikoa ya kanda ya ziwa na dhidi ya Azam jana. Ingawa uwezekano wa kutwaa ubingwa haupo wala kutwaa nafasi ya pili, lakini bado kuna kazi ya kutetea heshima na hadhi ya Simba ili iweze kumaliza katika nafasi nzuri.
Wachezaji na viongozi hawataweza kufanya lolote pasipo umoja na mshikamano wa wapenzi na wanachama wake. Kama kauli mbiu ya Simba isemavyo, “NGUVU MOJA.”
MECHI YA AZAM
PAMOJA na kukubaliana na matokeo ya mechi ya jana dhidi ya Azam, uongozi wa Simba unapenda kuweka rekodi wazi kwamba haukuridhishwa na uchezeshaji wa mwamuzi, Oden Mbaga, hasahasa katika kipindi cha pili.
Kwa bahati nzuri, msimamo huu wa Simba hauna hata chembe ya ushabiki kwa vile hata washabiki waliokuwa katika upande wa watani wetu wa jadi, nao pia walionekana kutofurahishwa na uchezeshaji wa Mbaga.
Mbaga ni mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na katika hali ya kawaida ilitazamiwa mechi ingechezeshwa kwa viwango vya kimataifa lakini hali ilikuwa kinyume chake.
Simba inaamini kwamba Mbaga hakuutendea haki mchezo ule wa jana. Simba inasema hivi kwa sababu inataka mwamuzi huyo ajirekebishe na kwamba matokeo ya mechi viwanjani yaamuliwe na ubora wa timu na si maamuzi yenye utata.
UJUMBE MFUPI WA MANENO KWENYE SIMU (SMS)
KUNA ujumbe mfupi wa maneno umeenezwa kwenye baadhi ya simu za mkononi za wapenzi wa Simba zikidai kwamba washabiki wa Yanga waliokuwa wakiishangilia klabu yetu jana walifanya hivyo kwa sababu klabu hizi mbili zimeingia katika mahusiano.
Ujumbe huo ukadai kwamba lengo la mahusiano hayo mapya baina ya Simba na Yanga ni kuhakikisha kwamba Simba inafungwa kwa idadi kubwa ya mabao kwenye mechi ya watani wa jadi Mei 18 mwaka huu.
Ujumbe huo, ukaenda mbali zaidi kwa kudai kwamba hata kambi ya Simba ya Bamba Beach imefadhiliwa na Yanga.
Ujumbe huo wa simu ni wa kuchekesha. Na unachekesha sana. Yeyote aliyetunga meseji hii ana nia ya kuleta machafuko ndani ya klabu ya Simba. Inaonekana haridhishwi na hali ya amani iliyopo klabuni kwa sasa.
Uongozi wa Simba unakana kuwepo kwa mahusiano yoyote ya kuhujumu timu baina ya viongozi wa klabu na Yanga. Kitendo cha kushangiliwa kwa timu pinzani si kigeni kwani kimewahi pia kutokea katika nchi kadhaa duniani.
Ikumbukwe kwamba kimsingi, si jinai au mwiko kwa shabiki wa Yanga kuishangilia Simba. Kama washabiki wa wapinzani wetu wa jadi walivutiwa na kiwango chetu na kuamua kutushangilia, hiyo haikuwa dhambi.
Uongozi unapenda kuwaomba wanachama wa Simba kuwa na imani na uongozi wao na kufahamu kwamba unafanya kila unaloweza kulinda na kuhifadhi hadhi na heshima ya klabu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Si useme tu ukweli kuwa Yanga washindanani wao wakuu ni Azam, kwani wana nafasi kama yao ya kunyakua Ubingwa? Hakuna kiwango wala nini, wanapopambana jogoo mdogo na mkubwa, jogoo mdogo huwa na washabiki wengi zaidi, na Simba ndiye alikuwa Jogoo mdogo Jana.

    ReplyDelete
  2. Taarifa nzuri, ila nimecheka sana na kubaki sina mbavu kwa kusoma mistari ifuatayo nanukuu: Ingawa uwezekano wa kutwaa ubingwa haupo wala kutwaa nafasi ya pili, lakini bado kuna kazi ya kutetea heshima ya simba ili kumaliza ktk nafasi nzuri, mwisho wa kunukuu.Nilichokielewa hapa ni kwamba heshima ya simba haipatikani kwa kutwaa kombe, kushika nafasi ya pili au hata pengine nafasi ya tatu bali ni...................hapa nawaachia nyie wadau mjibu.Yaani hii ndio kitu inaitwa ngangari, au komaa kichwa kwa kulinda heshima.NIMEIPENDA SANAAAAA.

    ReplyDelete
  3. Simba mimi nimewafagilia sana,wengi walitegemea mtawaachia Azam(match fixing)ili Yanga isipate ubingwa kitu ambacho kinaharibu ushindani kwenye ligi na kudhohofisha timu yetu ya Taifa(Taifa Stars).Ili ligi iwe bora lazima tuache hayo mambo ya kizamani ya 'kuachiana'mechi.Timu zingine zijifunze hili.Kwa sasa ligi yetu ni bora kwenye ukanda wetu Fulani na ndiyo maana timu ya Taifa inafanya vizuri kwenye Brazil WCQ

    David V

    ReplyDelete
  4. Mimi nilifikiri utaongelea Madai ya Nsa HJob kuwa alipewa kitu kidogo wakati akichezea Villa hii ndiyo ingekuwa taarifa ya Muhimu siyo hizi ngonjera

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...