Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen aksisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa Tanzania, mjini Kampala jana kuhusu mechi ya leo ya kufuzu kucheza michuano ya CHAN dhidi ya Uganda Cranes inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini humo. Wengine ni Kocha Msaidizi, Sylvester Marsh (kulia) na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura.
Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Sylvester Marsh akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa Tanzania (hawapo pichani) mjini Kampala jana kuhusu mechi ya leo ya kufuzu michuano ya CHAN dhidi ya Uganda Cranes inayotarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Namboole mjini humo. Wengine ni Kocha Mkuu, Kim Poulsen (katikati) na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura. 

Moja ya mikakati ya Taifa Stars kwenye mechi ya kesho (Julai 27 mwaka huu) dhidi ya Uganda kuwania kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini ni kushambulia kwa muda mwingi wa mchezo.

Kocha Kim Poulsen amesema maandalizi ya Taifa Stars jijini Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo ambayo Uganda inaongoza kwa bao 1-0 yalikuwa mazuri, lakini mabao ni muhimu hivyo watashambulia bila kusahau kulinda lango lao.

“Unapocheza mechi za aina hii za nyumbani na ugenini, huku mwenyeji akiwa anaongoza mabao yana maana kubwa katika mechi. Mabao yanabadili mchezo na pia wachezaji kifikra,” amesema Kim akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Mt. Zion ambayo Stars imefikia.

Amesema katika mechi ya kwanza walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia, hivyo wamekuwa wakifanya mazoezi ya kushambulia, jinsi ya kutengeneza nafasi, na jinsi ya kumalizia.

“Hivyo tuko hapa (Kampala) kwa ajili ya kufunga, ni lazima tufunge ili tuweze kuendelea na mashindano. Lakini ngome yetu nayo ni lazima iwe makini ili kutoruhusu bao,” amesema Kim na kuongeza kuwa kikosi chake cha kwanza ni lazima kitakuwa mabadiliko kutoka na Mwinyi Kazimoto kuingia mitini na Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio Uholanzi.

Amesema angalau kutakuwa na mabadiliko kwa kuingiza sura mbili mpya katika kikosi cha kwanza, na kuongeza kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mechi hiyo kwani timu ikienda kwenye Fainali za CHAN itakuwa manufaa kwao binafsi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefanya mazoezi ya mwisho leo jioni Uwanja wa Mandela ulioko Namboole ambao utatumika kwa ajili ya mechi hiyo kesho.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo namba 38 ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.

Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Kampala

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 26, 2013

    TAIFA STARS.
    wana sababu zote za kushinda mchezo wa kesho,kwanza Cranes-Uganda watajihami kutoka na ushindi wa mwanzo,tuzitumie nafasi za makosa ndani ya kujihami,pili wataingia uwanjani kama washindi
    "favourites" watakuwa na kazi kubwa
    kulitafuta goli japo moja watoke na ushindi wa mabao ya jumla, tuzitumie nafasi hizo za mapengo watakayoacha nyuma kwa kasi zao za ushambuliaji,muhimu kwa Taifa Stars wachezaji wa nyuma na washambuliaji wacheze mchezo sawa na mfumo wa Hollad National Team "TOTAL FOOTBALL" kuwepo na maelewano ya pasi za karibu na haraka na walinzi wetu kulinda ngome ya nyumba bila wingi wa makosa,washambuliaji kutopoteza nafasi wakiwepo ndani ya box la mauaji-penalt area tunataka ushindi
    KILA LA KHERI TAIFA STARS.
    Mickey "MIKIDADI" JONES
    Denmark

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...