Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein  akilakiwa na Balozi wa Tanzania Jumuiya ya Ulaya Dr. Diodorus Buberwa Kamala baada kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Schiphol,  Uholanzi,  kuanza ziara ya kikazi ya siku tano nchini humo leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewasili nchini Uholanzi kuanza ziara rasmi ya siku tano nchini humo kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bwana Mark Rutte.
Hapo kesho Dk. Shein atatembelea bandari ya Rottedam ambapo baadae atafanya mazungumzo na makampuni na makampuni yaliyo katika sekta ya miundombinu ya usafiri wa bahari.
Kesho jioni atakutana na Mfalme wa Uholanzi Willem Alexander na baadae kuhudhuria chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshma yake.
Jumatano ijayo tarehe 28 Agosti, 2013 atakutana na Waziri wa Biashara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bibi Lilianne Ploumen na pia atafanya mazungumzo na wadau katika sekta ya Nishati. Atatembelea pia Makao Makuu ya Kampuni ya Mafuta ya Shell.
Mapema Alhamisi asubuhi Dk. Shein atakutana na Waziri Mkuu wa Uholanzi Bwana Mark Rutte. Baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uholanzi Rais wa Zanzibar atatembelea Kampuni ya vifaa vya uchunguzi wa maradhi ya Sakura ambako atabadilishana mawazo juu ya masuala ya afya kati ya Zanzibar na Uholanzi.
Siku hiyo baadae mchana atatembelea bandari ya Scheveningen ambako atakutana na wananchama wa Muungano wa Wadau katika Sekta ya Uvuvi na kukutana pia na uongozi wa kampuni ya usindikaji na uuzaji wa mazao ya bahari nchini humo. Baadae jioni atakutana na watanzania wanaoishi nchini Uholanzi mjini The Hague.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Schiphol mjini Amsterdam Dk. Shein alipokelewa na Mwakilishi wa Mfalme wa Uholanzi Kamanda Juan Irausquin, Naibu Mkurugenzi wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi bwana Micheal Rauner, Balozi wa Uholanzi nchini Bwana Jaap Fredericks, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Balozi Diodorus Kamala na Bwana Frans Hakkenberg, Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini Uholanzi.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana Waziri Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Silima Kombo Haji.
Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Tarehe 1 Sept, 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...