Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Meja Erick Komba akiongea na waandishi wa habari  leo katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Jeshi hilo  jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Tanzania ni moja kati ya nchi tatu zilizopeleka kikosi chake nchini DRC ikiwa ni sehemu ya SADC standby brigade inayotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO) na kinafanya kazi chini ya Force Commander  huku majukumu yake yakiwa ni kuzuia waasi kujitanua, kuvunja nguvu ya waasi na kuwapokonya silaha makundi yote ya waasi. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Assah Mwambene. 
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Assah Mwambene akiongea na waandishi wa habari jinsi baadhi ya vyombo vya habari vinavyoandika taarifa zisizo  sahihi  kuhusu  ushiriki wa  majeshi ya Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa ni sehemu ya SADC standby brigade inayotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO)  . Kushoto ni Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Meja Erick Komba.
Ushiriki wa Tanzania katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani nchini DRC, unatokana na mgogoro kati ya Serikali DRC na waasi hususan kikundi cha waasi cha M23. Mgogoro huo ulianza mwezi Aprili 2012 ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika Jeshji la serikali ya DRC na kuanzisha mapigano hali iliyopelekea hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.

Kufuatia hali hiyo mbaya ya usalama, wakati wa kikao cha International Conference on the Great Lakes Region kilichofanyika tarehe 12 Julai 2012 mjini Addis Ababa, Ethiopia, Mhe. Rais Joseph Kabila aliwasilisha ombi kwa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu ambazo Rwanda, Uganda, Tanzania,  na DRC akaomba nchi wanachama wa Maziwa Makuu zisaidie kuwapokonya silaha waasi wa M23.

Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu walikubaliana na ombi hilo na kutoa maelekezo kwa Mawaziri wa Ulinzi ambao walikutana tarehe 01 hadi 2 Agosti 2012  na kujadili maelekezo ya Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu. Mawaziri wa Ulinzi walikubaliana kuwa ni muhimu kwa vikundi vyote vya Waasi (ADF, FDLR na M23) kushughulikiwa na wakawasilisha mapendekezo yao kwa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu.

Tarehe 7 Agosti 2012, Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu walikutana tena mjini Kampala, Uganda na kupanga mkakati wa kuanzishwa kwa ‘Neutral Intervention Force (NIF)’ na nchi wanachama wa Nchi za Maziwa Makuu zikaombwa kuchangia askari watakaounda ‘Neutral Intervention Force (NIF)’ambapo Tanzania iliombwa na ikahadi kuchangia kikosi kimoja. Kikao hiki kilitoa maelekezo ya hatua inayofuata kwa Mawaziri wa Ulinzi wa Maziwa Makuu.

Tarehe 7 hadi 8 Sep 2012, Mawaziri wa Ulinzi wa maziwa Makuu, walikutana na kujadili utekelezaji wa uanzishwaji wa ‘Neutral Intervention Force (NIF)’. Wakaunda ‘Military Assessment Team (MAT)’ kufanya tathmini ya tishio. Timu hiyo ililifanya tathmini na kuwasilisha taarifa yake kwenye kikao cha Mawaziri wa Ulinzi kilichofanyika tarehe 25 Oktoba 2012 mjini Goma, DRC na baadaye taarifa hiyo iliwasilishwa kwa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu ambao waliagiza kushirikishwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika(AU) na Umja wa Mataifa(UN) ili kufanikisha mkakati huo.

Nchi wanachamma wa SADC na Nchi za Maziwa Mkuu kwa pamoja walikubaliana na kupendekeza SADC Standby Brigade ipelekwe DRC kama ‘Neutral Intervention Force (NIF)’. Kufuatia ridhaa hiyo nchi wanachama wa SADC ziliombwa kuchangia ambapo nchi mbalimbali wanachama zilikubali kuchangia, lakini Umoja wa Mataifa(UN) ilizipitisha nchi za Tanzania, Afrika Kusini na Malawi kuchangia askari nguvu ya Brigedi moja kuunda NIF ya MONUSCO.

Aidha, Umoja wa Mataifa mwezi Januari 2013 uliridhia mapendekezo ya Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu na Nchi wanachama wa SADC ya kuundwa ‘Neutral Intervention Force (NIF)’ na kupelekwa DRC. Kufuatia idhini hiyo tarehe 28 Machi 2013, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha    Azimio (Resolution) namba 2098 (2013) na kutoa jukumu maalumu la ulinzi wa amani nchini DRC, likijumuisha ushiriki wa Neutral Intervention Force (NIF)kama sehemu ya MONUSCO, na ikaitwa ‘Force Intervention Brigade (FIB)’ ambayo kikosi cha Tanzania ni sehemu ya Brigade hiyo.

Kwa mantiki hiyo ieleweke kwamba, Kikosi cha Tanzania kilichopo DRC ni sehemu ya SADC standby brigade iliyotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO). Kinafanya kazi chini ya Force Commander, MONUSCO na majukumu yake ni:
    1. Kuzuia waasi kujitanua (Prevention of Expansion)
    2. Kuvunja nguvu za waasi (Neutralization)
    3. Kuwapokonya silaha makundi yote ya waasi.
Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko chini ya majeshi ya Umoja wa Mataifa ya MONUSCO, inamanisha kuwa Operesheni hiyo ni ya Umoja wa Mataifa, Tanzania haipigani na M-23 na haina tatizo na Rwanda kuhusiana na Operesheni hiyo na ridhaa ya kikosi chetu kwenda DRC ilikubaliwa pia na Rwanda, nchi ambayo ni mwanachama wa nchi za Maziwa Makuu. Aidha, Rwanda imesaidia sana kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha watu, vifaa na zana katika nchi yake kupeleka DRC.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi.
Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Pia kama nchi za Maziwa Makuu zimetoa taarifa kwa umma tarehe 6.sept. 2013 jijini Kampala kuwa serikali ya RDC isitishe mapigano na kuongea na M23, je hadidu rejea za jeshi la MONUSCO ( ikiwemo JWTZ) bado zile zile? soma taarifa hapa chini ya mkutano wa Kampala.

    Resume talks with rebels, Kabila told:
    the leaders yesterday ordered the resumption of talks between Congo’s M23 rebels and the Kinshasa government, which dialogue had stalled after renewed fighting broke out in eastern DR Congo.
    The talks, according to the joint communiqué released late in the evening, also directed fresh dialogue must be concluded within 14 days.


    “... The Kampala dialogue should resume within three days after this extraordinary summit and conclude within a maximum 14 days during which maximum restraint must be exercised on the ground to allow for talks to conclude. The chairman (President Museveni)
    Soma zaidi source: http://www.monitor.co.ug/News/National/Resume+talks+with+M23+rebels++Great+Lakes+leaders+tell+Kabila/-/688334/1981580/-/tsyj8g/-/index.html

    Mdau
    Globu ya Jamii

    ReplyDelete
  2. Hizi ndizo habari zinatakiwa kuzungumziwa siyo kusikiliza habari za watu amabao wanataka kutengenisha Rwanda na Tanzania. East Africa ni ndugu na kuna watu hawataki kuona east africa inafanikiwa.

    ReplyDelete
  3. Haya ndiyo mambo,

    Yanini tugombane tukiwa sote ni wanandugu ktk Afrika ya Mashariki?

    Hivi jamani tutajisikiaje kama ndugu zetu Rwanda wanaishi kwa tabu kila kukicha hawana amani na maisha yao?

    Hata wale waliotimuliwa kurejea nyumbani Watanzania tunge furahi kuona ndugu zetu Jirani wakirejea nchini Tanzania tukaungana nao LAKINI WAKIWA WAME FUATA SHERIA ZINAZO KUBALIKA NA KANUNI ZA UHAMIAJI ZINAZOTAKIWA KWA UKIMBIZI NA UKAZI WA MUDA NCHINI !!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...