Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seeif Sharif Hamad (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi mtendaji wa Community Forest Pemba, Mbarouk Mussa Omar,wakati akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi wao, wakati alipokutana nao, Ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seeif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira kutoka Canada, pamoja na watendaji wa ofisi yake, baada ya mazungumzo na wadau hao Ofisini kwake Migombani. (Picha na Salmin Said, OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesifu juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya inayojihusisha na urejeshaji wa rasilimali asilia ya “Community Forest Pemba”, katika kuwapatia wananchi elimu juu ya utumiaji wa nishati mbadala na kuhifadhi mazinigira kisiwani humo.
Maalim Seif ametoa pongezi hizo leo wakati alipokutana na uongozi wa Jumuiya hiyo, pamoja na watendaji wa Community Forest International ambao wamekuwa wakifanya shughuli hizo kwa mashirikiano.
Amesema elimu ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo nishati mbadala, upandaji miti na utaalamu wa uvunaji wa maji ya mvua inahimizwa sana na Serikali, na kwamba hatua ya jumuiya hizo kueneza taaluma hiyo inasaidia sana juhudi za serikali.
Maalim Seif amezihimiza jumuiya hizo kuendelea kuwa karibu na wananchi katika Shehia mbali mbali kisiwani humo, ili wananchi waendelee kunufaika na utaalamu wao, ambao ni rahisi na unaoepusha madhara ya uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Community Forest Pemba, Mbarouk Mussa Omar, wananchi wa vijijini wanaweza kupunguza gharama za matumizi kwa kutumia nishati mbadala na kuepuka uhariribifu wa mazingira, sambamba na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema mradi huo ambao pia unajihusisha na utengenezaji wa majiko sanifu, upandaji wa miti na kilimo, pia umefanikiwa kujenga skuli pamoja na hodhi linalohifadhi lita laki mbili katika kisiwa kidogo cha Kokota Pemba, vitu ambavyo tayari vimeanza kutoa huduma kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Amefahamisha kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi 14 ya Tanzania inayofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU), na kwamba wamebakiwa na mwezi mmoja kukamilisha mradi huo.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa “Community Forest International” Jeff Schnurr, amesema Zanzibar inavyo vianzio vingi vya upatikanaji wa nishati mbadala vikiwemo takataka zinazozalishwa pamoja na upepo.
Amesema Jumuiya yake itawahamasisha wadau wengine wa mazingira duniani kuja kufanya utafiti Zanzibar, ili kuona maeneo zaidi ambayo yanaweza kusaidia kupatikana kwa nishati mbadala na uhifadhi wa mazingira ya visiwa kwa ujumla.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...