Mkoa wa Kilimanjaro unatarajia kujenga mji wa viwanda na biashara katika eneo la Lokolova ili kuchochea uongezaji thamani mazao na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nchi jirani.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Bw. Leonidas Gama aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni mjini Moshi kuwa eneo hilo ambalo tayari limebainishwa litatoa fursa kubwa ya biashara.“Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na sekta binafsi tumepanga mipango hii ili kuboresha biashara,” alisema, na kuongeza kuwa eneo hilo litajengwa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Alisema mji huo utakuwa nguzo kubwa kwa soko la kisasa la kimataifa linalotarajiwa kujengwa katika eneo hilo la Lokolova kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.“Mkoa wetu huu upo mpakani na ni mashuhuri sana katika biashara lakini bado tunauza mazao ambayo ni ghafi ambayo hayana tija kubwa ya kibiashara,” alisema.
Alisema kama ilivyo katika maeneo mbalimbali nchini, bado wananchi wa mkoa huo wanauza mazao ghafi na kuwa ujio wa viwanda hivyo utasaidia kusindikwa kwa mazao hayo na hivyo kuleta tija zaidi.Alibainisha kwamba wakati wa kuuza mazao ghafi umepitwa na wakati, hivyo mipango hiyo imekuja katika kipindi sahihi ambapo mazao yataongezwa thamani na kupangwa katika madaraja ili kupata soko zaidi.
Mkoa huo ni maarufu kwa mazao mbalimbali kama nyanya, ndizi, maparachichi na mbogamboga.Akizungumzia mradi mwingine alisema katika wilaya ya Siha wanatarajia kuanzisha kituo kikubwa cha kisasa cha utalii ili kuongeza utalii katika mkoa wao.
“Kituo hiki kitajengwa katika maeneo yaliyokuwa ya Serikali ambayo kwa sasa hayatumiki, na kujengwa vivutio vizuri vya utalii mbalimbali,” alisema.Kwa mujibu wa Bw. Gama, mpango huo ukikamilika utaongeza idadi ya watalii na kusaidia kukuza mapato ya sekta binafsi na umma na kukuza uchumi wa nchi.
Alifafanua kuwa vivutio vitakavyojengwa ni pamoja na eneo la maonyesho, bustani mbalimbali ikiwemo ya wanyama, maua, mahoteli ya kisasa na maeneo ya michezo.Pia utajegwa mfano wa mlima Kilimanjaro kwa ajili ya watalii ambao hawawezi kwenda kuona na kuupanda mlima huo maarufu barani Afrika.
Alisema miradi yote hiyo itafanywa kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na biafsi kwa faida ya pande zote mbili.Alisistiza kuwa mkoa wake na halmashauri zote zimebainisha maeneo ya biashara na kuyatenga ambapo sekta binafsi itayatumia kufanya biashara bila vikwazo vyovyote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. I like the enthusiasm ila tumieni wataalamu katika yote haya msiwaachie wanasiasa to do the plans. Kwa viwandani itabidi mtafute umeme mbadala ili kushusha bei ya umeme na kuvutia viwanda vingi. Kwenye utalii msisahau utalii wa ndani ya nchi na nchi za jjirani, msiwekeze sana kwa kuwategemea wa ulaya na marekani.

    ReplyDelete
  2. Jitahidi mkoa wa Kilimanjaro mipango hii inatia moyo.

    ReplyDelete
  3. Hongera mkuu wa mkoa mipango mizuri na inatia moyo natamani rais ajaye asikuondoe hapo kilimanjaro ili utimize yale yote uliyoyaanzisha: na sidhan kama mkoa huu utapata kiongoz imara kama ww Mungu akubariki sana mweshimiwa mkuu wa mkoa

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...