Rais wa Chama cha Wafanyabiashara,Wenyeviwanda na Kilimo (TCCIA) Injinia Peter Chisawillo akizindua rasmi utafiti utakaohusisha ukusanyaji wa maoni kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS Mobile System) kuhusu madhara yatokanayo na urejeshwaji wa ada za biashara kila mwaka kwa lengo la kuishawishi serikali kuweka sera, sheria na taratibu rafiki kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini leo jijini Dar es salaam.
=======  ======  =========
TCCIA YAZINDUA UTAFITI KUKUSANYA MAONI YA WAFANYABIASHARA KUHUSU ATHARI ZA UREJESHWAJI WA ADA YA LESENI ZA BIASHARA.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
16/5/2014, Dar es salaam.

Chama cha Wafanyabiashara,Wenyeviwanda na Kilimo (TCCIA) kimezindua rasmi utafiti utakaohusisha ukusanyaji wa maoni kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS Mobile System) kuhusu madhara yatokanayo na urejeshwaji wa ada za biashara kila mwaka kwa lengo la kuishawishi serikali kuweka sera, sheria na taratibu rafiki kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Akizungumzia utafiti huo leo jijini Dar es salaam Rais wa cha hicho Injinia Peter Chisawillo amesema kuwa mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 serikali ilitangaza urejeshwaji wa ada ya leseni za biashara nchi nzima na kuongeza kuwa utaratibu huo unaomlazimu mfanyabiashara kukata leseni na kuilipia kila mwaka unakwenda kinyume na sheria ya leseni ya mwaka 1972.

Amesema kuwa sheria hiyo na hasa marekebisho yake ya mwaka 2004  yaliwezesha leseni za biashara kutolewa bure na mara moja tu kwa kipindi cha maisha yote ya biashara jambo ambalo linakiukwa.

“Tayari kuna malalamiko mengi kwa jumuiya ya wafanyabiashara yanayotufikia kutoka kuanzia ngazi za wilaya na mikoa juu ya urejeshwaji wa ada hiyo, sekta binafsi inailalamikia serikali kwa kutoishirikisha katika urejeshaji wa utaratibu huu ambao unaiathiri sekta hii moja kwa moja” amesema Injinia Chisawillo.

Ameeleza kuwa sekta binafsi inaamini kuwa serikali imeamua kuongeza mapato bila kuzingatia nia ya urasimishaji wa sekta isiyo rasmi kwa lengo la kuharakisha uchumi kwa ujumla na kuongeza kuwa hakuna mwongozo maalum uliotolewa na serikali kuelekeza namna maombi ya leseni yatakavyoshughulikiwa.

Amesema sekta binafsi inaamini kuwa ili kuondoa urasimu na usumbufu kwa wafanyabiashara pindi wanapoomba leseni kila mwaka , serikali itumie kumbukumbu zilezile kila mwaka bila kulazimu mfanyabiashara  kufuata mlolongo wa taratibu za kuomba leseni kila mwaka kwa lengo la kuokoa muda na kupunguza kupanda kwa gharama za uendeshaji wa biashara.

Aidha Injinia Chisawillo amesema kuwa utafiti huo unaofanywa na TCCIA) utafanyika kwa muda wa wiki 4 ukiwahusisha wanachama wote  takribani 22,000 (Elfu Ishirini na mbili) na wale wasio wanachama na unafadhiriwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la BEST –AC ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu zao kwenda namba 15539  na kutoa maoni kuhusu urejeshwaji wa ada hiyo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ni msimamo wa muhimu wa TCCIA kwa kuwa Benki ya Dunia inasisitiza kushusha gharama za kibiashara ili kukuza ushindani wa Kibiashara na kuongeza Faida ktk biashara.

    Hivyo kurudisha ADA YA LESENI ZA BIASHARA ZA KILA MWAKA itakuwa ni kikwazo kwa Ukuzaji wa biashara na Uchumi hasa:

    1.Kwa zile za hatua ya mwanzo 'Start ups', na.

    2.Zile ndogondogo SME's ambazo ndio mhimili wa Uchumi, (SME's are key drivers for economic growth).

    Serikali ingefikiria Kibiashara na Kiuchumi zaidi na kusitisha suala hilo kama ilivyofanya uamuzi wa maana mwaka 2006 kufuta Ada za Leseni za biashara za kila mwaka!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...