Taifa letu likiwa katika mpito na wakati mgumu wa kuandika rasimu ya katiba mpya ya watanzania, hatuna budi kuweka kando itikadi zetu za kisiasa, tofauti za kiimani na hata maslahi binafsi ili tuungane katika kutafuta katiba itakayokidhi mahitaji yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Katika mchakato huu, inatubidi tuwe makini na wakweli katika kujadili hatma na haki ya kuzaliwa ya ndugu zetu ambao wanaishi ughaibuni. 
Lazima tuwajumuishe na kuwapa haki zao za msingi; haki ya kuzaliwa katika ardhi ya Tanzania ambayo ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu. 
Hii ni haki ambayo kamwe haiwezi kubatilishwa na mamlaka ya aina yeyote wala haiwezi kutenguliwa na binadamu yoyote. Ni kujidanganya kudai kwamba waliochukua uraia wa kigeni warudi Tanzania kama wageni.
Kwa makusudi kabisa, nimeamua kuchokonoa huu mjadala wa haki ya kuzaliwa nikiwa na sababu nyingi za manufaa kwa taifa letu; ya msingi ikiwa ni sababu ya kiuchumi na hatma ya taifa letu. Jamii ya watanzania wanaoishi ughaibuni ni hazina adimu ya rasilimali watu wanaohitajika katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya Tanzania.
Ni kundi lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao lazima tuwakumbatie. Mheshimiwa Rais Jakaya kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waheshimiwa Dr. Wilibrod Slaa, Freeman Mbowe, Bernard Membe, wote, kwa kipindi kirefu wameunga mkono haki ya kuzaliwa ya watanzania wanaoishi ughaibuni kupata haki zao za msingi za kurudi katika ardhi yao ya kuzaliwa bila masharti wala vikwazo vya aina yoyote
Bila shaka wapo wanasiasa wenye ajenda zao binafsi ambao wamekuwa kikwazo kikubwa katika kuwazuia wazawa wa Tanzania wanaoishi ughaibuni kupata haki sawa katika katiba mpya. Siwezi kuwalaumu, kwani pengine wengi hawana uelewa wa faida ambazo zitapatikana kwa kuwapa ndugu zetu waliozaliwa Tanzania haki ya kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Mjadala huu tuaouanzisha lazima uweke katika mizani faida na athari za kuwapa watanzania haki yao ya kuzaliwa na hatimaye kupata uwiano ambao utakidhi na kujibu maswali mazito ambayo ndio chanzo cha vikwazo vilivyopo kwa sasa.
Wiki chache zilizopita, Blogger-mwanasiasa mmoja nchini Tanzania alitoa shutuma dhidi ya watanzania wajulikanao kama wana Diasapora wanaodai haki zao za kuzaliwa katika ardhi ya Tanzania, huku akisahau kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwana Diaspora kwa miaka takribani thelathini. 
Hata kama alikuwa na uraia wa nchi thelathini, mwisho wa siku alirudi katika ardhi aliyozaliwa yaani, Tanzania. Nina imani kwamba anao wanafamilia ughaibuni ambao ndoto yao kubwa ni kutambulika kama watanzania wenye haki zote ambazo kila mzawa anazo.
Katika tafsiri isiyo rasmi ni kwamba amewatosa ndugu zake. Warudi Tanzania wasirudi siyo tatizo kwake. Tofauti na mategemeo ya wengi, huyu blogger alitegemewa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kutetea haki za kuzaliwa za watanzania wanaoishi ughaibuni.
Huyu blogger ndio picha kamili ya wanasiasa ambao mara nyingi hutafuta nafasi za kupiga picha na wanadiaspora pindi wanapotembea nchi nyingine ambako kuna watanzania. 
Wanasiasa hawahawa watakuwa mstari wa mbele kujipanga uwanja wa ndege kuonyesha huzuni na huruma na hata kumwaga machozi ya kinafiki pale majeneza ya wana Diaspora yanaporudishwa katika ardhi yao ya kuzaliwa huku wakiwanyima haki zao za kuzaliwa wanapokuwa hai.
Wengi wa watanzania waliomba uraia wa nchi nyingine siyo kwamba hawalipendi taifa lao,la hasha! Wengi ni wazalendo waliolazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine ili kupata ahueni kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili mamilioni ya watanzania. 
Wengine walitafuta vibali vya kuishi ili wapate elimu ambayo Tanzania isingeweza kuwalipia.
Badala ya kutafuta chimbuko la tatizo au wazo fulani, ni desturi yetu kama jamii kwa mjumbe kusulubiwa na hata kuuwawa ili kuliua wazo au jambo linalotishia maslahi ya wachache. Kumshambulia John Mashaka mathalani, hakutaweza kamwe kuliua swala ambalo wakati wake umewadia. 
Binafsi nimeamua kubaki na uraia wangu wa kitanzania licha ya kuwa na nafasi ya kuchukua uraia wa nchi nyingine. Kubwa ya yote, ninajikita kuanzisha huu mjadala ili kuitetea Tanzania na rasilimali zake hasa rasilimali watu.
Kama taifa, tunawahitaji ndugu zetu wenye taaluma mbali mbali waliotapakaa kote duniani na hata kufikia hatua ya kuchukua uraia wa nchi nyingine. Napigania watanzania milioni 45 nikizingatia faida za kiuchumi, kisiasa, kijamii ambazo zinapatikana na rasilimali watu wenye asili ya kitanzania. Wazawa wanaopigania haki zao za kuzaliwa pamoja na vizazi vyao.
Ni muhimu hawa wanasiasa wakakumbushwa kuhusiana na maamuzi yao ya kuwatenga watanzania walio nje ya nchi, hususan kuwanyima haki zao za kuzaliwa. Inabidi wakumbushwe kwamba, wazaliwa wa Tanzania wanaoishi ughaibuni wana ndugu zao Tanzania, ambao ndio wapiga kura wao. 
Na ikiwa wanaamua kwa makusudi kuwatenga, basi kundi hili maarufu kama Diaspora watumie uwezo wao, ushawishi wao na mbinu zote walizo nazo kuwaadhibu wanasiasa wanaozuia haki zao za kuzaliwa
Pengine niwakumbushie viongozi wa jumuiya za watanzania popote walipo duniani kwamba haki haiombwi. Haki inadaiwa, na asiyeweza kudai haki yake na hata kuiona haki yake kama zawadi au upendeleo fulani basi huyo amepoteza haki yake ya kuishi.
Viongozi wa jumuiya za watanzania ughaibuni hawana budi kuonyesha uwezo wao wa kuongoza kwa kuwa mstari wa mbele wakiwahamasisha watanzania waliotapakaa duniani kudai haki zao za kuzaliwa. Inabidi wapaze sauti zaidi ili viongozi wetu walioweka pamba masikioni wasikie madai yao. 
Mashabiki wa CCM, CUF, CHADEMA na wengineo wote wataathirika sawa. Kwa maana hiyo, vita hivi havina mipaka, ni vita vya watanzania wa matabaka yote. Wana diaspora lazima wawe na mshikamano kama watanzania.
Mungu Ibariki Tanzania

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 42 mpaka sasa

  1. Hii hapa ni changamoto yangu kwa kila mtanzania anayekubali au kukataa uraia pacha.

    Sababu hasa ya katiba mpya imesababishwa na mjadala wa muda mrefu juu ya muungano wa Tanzania. Na kwa taarifa iliyofikishwa kwenye bunge la katiba ni kuwa watanzania wengi wanataka serikali tatu.

    Hii ikubalika ina maana kutakuwepo nchi mbili zanzibar na tanganyika ambazo zitakuwa na serikali zao na kutakuwepo na serikali ya muungano wa Tanzania. Kila nchi itakuwa rais wake na bunge lake. Matokeo yake kutakuwa na raia wa nchi ya Zanzibar na raia wa nchi ya Tanganyika.

    Kwa maana hiyo kila mtanzania atakuwa na uraia pacha. Raia wa zanzibar au tanganyika na raia wa tanzania. Na kama ilivyo nchini uingereza, kwa mfano, wananchi wa wales na ireland wana haki ya kuwa na passport za nchi zao na vile vile za UK kwa sababu wao ni raia wa wales au ireland na UK.

    Sasa watanzania tuelewe hatuwezi kujadili suali la muungano bila suali la uraia pacha kwani muungano ni wa nchi na kila nchi ina wananchi na kila mwananchi ana haki ya kujinasibu uraia wake apendavyo yaani Mzanzibari, Mtanganyika au Mtanzania. Na kwa maana hiyo kila mwananchi wa nchi hizi mbili atakuwa na hiyari ya kutumia pasi ya nchi yake tu au pasi ya nchi yake na ya muungano.

    Uraia pacha ushapiga hodi Tanzania na kukataliwa kwake ni pale tu itakapoamuliwa kutokuwepo na serikali ya Tanganyika.

    ReplyDelete
  2. Wapende wasipende, huyu ndiye kiongozi wa tanganyika wa baadae. Kijana ni mahiri kweli. Mjadala kwisha

    ReplyDelete
  3. I salute you kijana weru ohn. You are always my hero.you are brave, brilliant and visionary, and these are the kind of people who are needed in Tanzania.

    I have lived in scotland for more than 30 years, teaching at a university though I was born in Tanzania. Mbeya, na niliporudi kuomba kazi UDSM usumbufu niliouoata haukuwa wa kawaida. Bila shaka umesikika. Tumekuelewa, muhimu ni wana diaspora kuungana kupigania haki zetu za kuzaliwa.

    Napendekeza watanzania ughaibuni wasusie balozi zetu na Viongozi wote ili waharakishe uraia pacha. Tudai tanganyika yetu

    ReplyDelete
  4. Bwana Mashaka asante sana kwa makala yako mazuri. Nikichukua uraia hapa uholanzi baada ya kujjfanya mkimbizi wa kinyarwanda ili nipate elimu baada ya kujabiru kwa kipindi kirefu kupata scholarship lakini mafisadi pale wizarani wakanifanyia ufisadi. Nataka kurudi nyumbani, sitaki kuchukua visa kama mgeni. Please. Nina uhakika tukiwa na wahamasishaji wazuri kumi kama mashaka john, tutapata nafasi kwenye jamii yetu

    ReplyDelete
  5. huyu mashaka kipindi alikuwa waziri wa mambo ya ndani mbona asingepigania uraia pacha ? Ila nimemkubali kwenye hii mada. Jamaa ni kichwa. Natumai huko bungeni atamwaga nondozzz zake za uhakika ili wakina Juma Nkamia waelemike

    ReplyDelete
  6. Lameck Ahiro, mbunge wa Rorya pamoja na Makongoro Mahanga wanapandwa na kiwewe wakisikia jina la John Mashaka. Mwezi wa February mwaka huu, Kwenye msimba kijini Ryagoro, mkazi mmoja alimuuliza Mh. Ahiro athibitishe uvumi jimboni kwamba atamuachia kijana uongozi 2015, lameck alimmiminia matusi ya mguoni na kuwaambia waombolizi kwamba mashaka atagombea ilala, kitu ambacho siyo kweli

    ReplyDelete
  7. serikali tatuMarch 25, 2014

    Ntatoa zawadi ya tsh . 1 million kwa yeyote atakaye leta ushahidi kwamba huyu john mashaka ni binadamu wa ukweli na anaishi wapi
    Michuzi na TISS wamefanya ujanaja wa hali ya juu kuchukua watu wenye akili ndani ya system na kuwapa jina feki la john mashaka ili kutingisha akili za watanzania.
    Nimewahi kuhoji na hata kumchalenji michuzi athibitishe uwepo wa john mashaka kwani amekuwa akimtumia kuvutia wasomaji na mada mzito nzito
    Huyu mashaka ni ujanja wa ccm na ikulu kuvuruga hoja za serikali tatu. Hakuna mtu mmoja ambaye anaweza kuwa na akili kama huyu jini wa michuzi mashaka
    Michuzi kuwenu wabunifu, mshaka is not real person it is fiction name nyinyi watu wa system mmetengeneza kutuadaa.
    Mtu wangu wa ndani amenitonya kwamba real mashaka is in USA, na huyu mwandishi siye, maybe ni dennis msaki wa mwananchi

    ReplyDelete
  8. Ndugu Mashaka,
    Asante sana kwa makala yako ya busara na yenye usito mwingi. Umezungumza mambo mengi ya maana. Hata wanangu waliokosa uraia wa bibi na babu zao wameifurahia sana makala yako. Nadhani: "ukuda" - hali ya kuwa na roho mbaya, kutopenda maendeleo ya wengine inachangia.

    ReplyDelete
  9. KAMA MLIAMAUA KUACHANA NA U TZ KIPI MMEKISAHAU?MCHAGUE KURUDI KWENETE U TZ AU MJE KAMA WAGENI NO DIASPORA TUTAIPINGA KWA NGUVU ZOTE,HATUWEZI KUFUNGUA MILANGO NA MADIRIRSHA ILI KILA KITU KIINGIE WADUDU,MAJAMBAZI,WEZI WATAKATIFU???????????NO TUNA WATU WAKUTOSHA KUWEZA KUIADILI NCHI SANA SANA MTATULETEA VIRUSI/MOLE AMBAZO AT THE END ZITAKUJA KUINGAMIZA NCHI..........................NO FOREVER FO DISPORA

    ReplyDelete
  10. Tanzania Diaspora needs unité like mashaka said.nineshangaa huyu jamaa anahachwa bne ya baraza la mawaziri ikhali mizigo kama kawambwa wanadunda tu

    ReplyDelete
  11. Hahahaaaaa,siri imefunguka. Michuzi si bora uziwanie hio milioni moja ujichane.Waonaje.

    ReplyDelete
  12. Mashaka ni nyerere wa kizazi chetu. Kijana amejaliwa akili. Busara zake zinahitajika sana kwa maendeleo ya Tanzania. Ila sikubariani naye kuwatetea hao wakimbizi wa Burundi

    ReplyDelete
  13. Mashaka, karibu wakati mwingi napinganaga na mawzo yako, lakini leo imebidi nikubaliane nawe. Kusema kweli, wakati huu si mzuri wa kuwa au kuwasapoti wanaDiaspora, kwani kuna watu wachache wanawachukia ndugu zao. Nakupongeza kwa kusimama kwa kikakamavu ukijua kabisa utatupiwa mawe, nao huo ndiyo uongozi. Wengi wetu tunajificha kwenye hizi Anonymous kwani ni waoga wa kupigwa mawe na Anonymous wengine. Kweli, haki ya mtu kuzaliwa haipotei ovyo na sababu nyingine nyingi tu.
    *Mmbongo Chiberia.*

    ReplyDelete
  14. Naungana kabisa na ndugu John Mashaka. Wachina wanazo passport zetu, matapeli ya kinaigeria yana passport zetu na zao pia alafu sisi wazawa tunaambiwa tulishaukana uraia wetu? Haikubaliki hii. Vijana kama mashaka wajasiri wajitokeze wapiganie haki zao.
    Tunataka uraia pacha. Pigeni kelele, wakeeni hawa mafisadi vikwazo watalegeza sasa hivi

    ReplyDelete
  15. TISS angalieni ili swala la uraia pacha linaweza kuweka nchi yetu pabaya tukizingatia wazi kwamba tuna maadui mbali mbali wakituzunguka kwa sasa.

    Mfano mzuri, Vyanzo vingine vya kijasusi vya nchi jirani wanaweza wakapeleka Sleeper Cells nje za nchi kama UK, USA wakasoma na kupata elimu nzuri tu then wakarudi Tanzania wakijifanya Watanzania waliojiita wakimbizi nje ili waje kutekeleza Mission zao ambazo zinaweza zikawa ata kugombea nafasi kubwa ndani ya nchi yetu ili waweze kutuzoofisha kisiasa, kiuchumi, kiulinzi, Kiutamaduni, na kuzoofisha Uzalendo na Muungano wetu tulionao!!

    Vile vile inawezekana wao ndio wanaochochea hii agenda ili watekeleza matakwa yao kwakuwa hakuna anayelifikiria kiundani ili swala.

    Pia ni vyema Wizara husika kutoa tamko rasmi la Serikali kuhusu maoni au mijadala ya hawa watu wanaotaka uraia Pacha. Usipoziba ufa ujue utajenga ukuta!! Sasa kazi kwenu na ni jukumu letu sote kuilinda nchi yetu na tuache pesa au maisha mazuri ya mataifa mengine kuleta matatizo nchini kwetu.

    Mh Michuzi najua unaipenda nchi yetu hii ya Tanzania na nakuomba sana sana kwa kuilinda nchi yetu usiibanie msg hii ili watu wetu wa TISS waweze kuiona na kuifanyia kazi na kuishauri Serikali kwa maelekezo zaidi.

    Asante.

    ReplyDelete
  16. The mdudu,anasema naungana na John Mashaka kwenye hii haki ya kuzaliwa ndani ya Tanzania yetu,maana mm hapa nilipo kama nimefungiwa kwenye CHUNGU ila sasa ndugu John Mashaka kakifungua gafra Chungu ndio nauona mwanga huo nje nje,nahitaji haki yangu mm ni mwana MOROGORO nakama sitoipata hiyo haki basi mm naongea na KINGALU au mizimu ya NYANYIKO nakitakachofuata ni mvua isiyo na kikomo.ni mm The mdudu au DIMOSO MKUDE.

    ReplyDelete
  17. Mashaka,
    I salute your brilliance and patriotism. Ila kwa hili swala naomba kutofautiana kidogo.
    Kwanza, niseme nasupport watanzania walio nje kupata uraia pacha. Sioni kwaninini. Binafsi nimekaa Marekani miaka zaidi ya 10 kabla ya kurejea nyumbani.

    Ukweli ni kwamba mjadala huu pamoja na umuhimu wake umekuwa poorly presented. Ninachohisi ni kwamba hata Diaspora wenyewe hawako on the same page. Juzi juzi nilimsikiliza mwakilishi wa Diaspora akiongea ila naona kama samaki mmoja akipigana ndani ya bahari kubwa. Kweli the whole diaspora imetuma mtu mmoja tuu. Naelewa kuna limit ya watu wa kuingia Bungeni ila kwanini hamkutuma watu wa kuja Dodoma kufanya kampeni?
    Besides, watanzania walio wengi wanaamini kama ulivyosema kwamba diaspora wameelimika. Ila issue yenu haijawa represented that way. Basically watu hawaoni sababu za kwanini kuwa na uraia pacha zaidi ya kwamba ni haki ya msingi au mna-invest.. really? that's not enough

    So, it is probably late but somebody need to rethink a new. Nyie ni wasomi, then make a case and not an argument.

    ReplyDelete
  18. Nimemkubali kuwatetea watanzania wenzake wanaojifanyaga wakimbizi na kutupa passport zetu. Hawa ni wa kuwaadhibu pindi watapopatiwa uraia walioukana . Inabidi wachapwe viboko pindi wanapewa passport za Tanzania, kama hawataki basi wabaki na hizo passport zao za welfare UK. Kitu kimoja ninachomsifia mashaka ni kimoja, ana akili. anajua kupanga na kupangua hoja, hilo halina ubishi. Ni moja kati ya ma genius hapa tanzania
    Mbaya ni kwamba ameegemea upande wa marekani zaidi huku akiwaponda wachina kila anapopata mwanya. Anasahau kwamba , hakuna taifa lenye watu wajanja kama wamarekani. Wamarekani wana tabia ya kutafuta vijana wenye vipaji na ma genius kama John Mashaka, kuwasomesha na kuwapa uwezo mkubwa kuchambua mambo na kuweza kuendesha akili za watu. Mimi sina shaka, John Mashaka ametayarishwa na ikulu ya marekani kuwa rais wa Tanzania siku moja. Haya makala yake yanaandikwa pale ubalozini au state department.

    ReplyDelete
  19. ujinga wetu, badala ya kuona uzito wa mada aliyoileta bwana mashaka, wengine wanageuka kumjadili na kumuita jini wa michuzi. grow up people. tunataka uraia pacha. tunataka haki yetu ya kuzaliwa

    ReplyDelete
  20. Thank you Mashaka

    ReplyDelete
  21. Duh...mdau wa hapo juu unanisikitisha sn...ina maana mpaka leo hujawahi kusikia jina la John Mashaka...?! Kijana mahiri aliyekuwa akifanya kazi ktk moja ya benki kubwa huko wachovia usa...mm namkubali sn najua wako wengi pia watakushangaa...

    ReplyDelete
  22. Mnataka haki zenu za kuzaliwa wakati wewe mwenyewe umeukana wazi wazi kwa manufaa na utajiri wa nchi nyingine?? Ambapo pia kumemfanya mtoto wako pia kuukana!!

    Kama hivi sasa unaweza kuukana uraia wa nchi yako kwa ajili ya Pesa na utajiri wa nchi nyingine, Je kesho wewe raia ulioukana U-Tanzania unaweza ukafanya nini kikubwa zaidi ya hapo???

    Nimeishi Uingereza zaidi ya miaka 12 lakini kamwe sijawahi kuukana uraia wangu na nilikuwa na nafasi ya kufanya hivyo ila kwakuwa naipenda Tanzania sikuwahi kufanya hivyo na Sasa nipo nchini ingawa maisha sio mazuri sana ila nipo vizuri sana zaidi ya nilivyokuwa Uingereza na bado ni Mtanzania 100%

    Hakuna uraia pacha SIO LEO WALA KESHO. NAUNGANA NA MSIMAMO WA SERIKALI.

    ReplyDelete
  23. Anayesema hamjui John Mashaka sijui anatoka dunia gani. Anamuonea ankal kumuita kwamba heti ni jinni la Ankal. John mashaka ndiye moja wa vijana mahiri wa kitanzania ughaibuni. Huyu yuko Wallstreet na Bank of America. Zamani alikuwa na Wellsfargo Bank.Huyu ndiye mchumi daraja la kwanza siyo mwigulu. Ni investment banks, na hizi kazi kuzipata siyo rahisi lazima uwe kichwa kweli kweli. Yaani lazima uwe kichwa hasa maana ni kazi maalum kwa ajili ya wazungu. Huyu ni mwanafunzi wa Prof. Nyan’goro. Amesoma pale duke MBA na JD. Watu wa aina hiyo ni wachache sana. Nakumbuka amewahi kuwaita Mwigulu na KIngwangallah ambao wote walitokomea. Katika vijana kumi wenye mafanikio makubwa marekani siyo wale wizi wa identity, John Mashaka na Hasheem Thabeet wako juu zaidi.

    ReplyDelete
  24. sIONI MAANA YA mUUNGANO WA NCHI MBILI KWA SERIKALI TATU ITAKUA NI JUMUIA HIYO TENA THEN BAADAE TUTAKUA NA PASI YA AFRIKA MASHARIKI BAADAE TENA UNGUJA NA PEMBA WATATAKA KUJITENGA NA KUA NCHI MBILI TOFAUTI HAPO TUNAZIDI KUONGEZA PASI TU.INANIKUMBUSHA NILIPOKUA SHULENI TULIKUA TUNAHIMIZWA KUUNGANISHA MADAFTARI AMBAYO NI MZIGO KUTEMBEA NAYO KILA SIKU. SERIKALI NI MBILI AU MOJA TU HIYO NI KUHUSU MUUNGANO. NA UPANDE WA ULAIA PACHA HAUNGII AKILINI KABISAAA KWANI IPO KISIASA ZAIDI INGENGUA KI MASLAHI YA NCHI TUSINGETAJA VYAMA KAMA MAMBO MENGINE YA SIVYO ENDESHWA KI UVYAMA VYAMA. MFANA RAHISI WA HAO WANAO PIGANIA URAIA PACHA. NGUNA NDUGU ZETU NI WATANZANIA WENYE ASILI YA UARABUNI LET SAY OMAN WAKATI HUO HUO ALIKUA RAIA WA TZ KWA MAANA YA KUZALIWA AKAENDA UINGEREZA AKAPATA URAIA HUYO ITAFIKA SIKU ATAHITAJI URAIA WA NCHI ZOTE TATU KWANI KOTE ANAHAKI NA PIA ANAWAJIBU WA KUCHANGIA KAMA MNAVYOTOA SABABU ZENU ZISIZO NA MASHIKO.
    MUHIMU.. NIKUTAFUTA NJIA RAHISI YA WATANZANIA WAASILI WENYE URAIA WA NJE KUFANYA SHUGHULI ZAO TANZANIA, WANAPO SEMA WANAHITAJI KUWEKEZA, KAMA WAZAWA WANAWEZA ONDOLEWA BAADHI YA VIKWAZO KAMA WANAVYO FANYA WENZETU WA INDIA.KAMA ANAHITAJI KUENDELEZA NCHI NA NI MZALENDO WAKWELI ARUDISHE URAIA WAKE WA TANZANIA KWA FAIDA YA NCHI NA YAKWAKE PIA.
    KWANI HAO WALIOKO NJE WAMEONDOKA NA KOO ZAO? HAMNA NDUGU WA KUWATUMIA KATIKA SHUGHULI ZA UWEKEZAJI?.
    NI HAYO TU.... SI PINGI WAKIJA KWA HOJA ZA MSINGI NA KUTUELIMISHA INAWEZA PATIKANA NJIA NZURI ZAIDI YA KUWASAIDIA WNA DIASPORA KUWEKEZA NYUMBAINI...KWANI KWENYE WENGI HAPAHARIBIKI JAMBO.

    ReplyDelete
  25. Rasimu ya KATIBA mpya imependekeza kuwa hakuna Dual Citizenship ila Diaspora wenye nasaba ya Kitanzania wapewe kitambulisho maalum ili mkija nyumbani msilipie viza ya kuingia Tanzania.

    Kitambulisho hicho maalum kwa wana Diaspora wa Kitanzania wenye uraia wa kigeni kina wapa uhuru wa kumiliki ardhi Tanzania,kuwekeza,ikitokea kifo ugenini kuzikwa ktk makaburi Tanzania n.k lakini hamtaruhusiwa kugombea au kupewa ajira nyeti Tanzania.

    Tembelea tovuti ya 1. MWONGOZO KUHUSU UTARATIBU WA WATANZANIA WANAOISHI UGHAIBUNI www.katiba.go.tz Tume ya Katiba Tanzania kuangalia masuala kama ya ndoa ya mtanzania na mgeni na mambo mengine kemkem.

    Hivyo Katiba mpya haina nafasi ya Dual Citizenship ila inapenedekeza mpewe vitambulisho maalum ambavyo vitawapatia nafasi ya kupata yale yote mnayoyapigania sasa.

    Hivyo wana-Diaspora mpende kujisomea machapisho mbali mbali ili kuelewa HAKI yenu ambayo bado ipo kwa kutumia kitambulisho maalum lakini suala la dual citizenship limetiwa kapuni kwa muda huu.

    Mdau
    Team Pasipoti Moja

    ReplyDelete
  26. MATATIZO YA KUUKUMBATIA UJAMAA KATIKA TAIFA LETU ATHARI ZAKE ZITACHUKUA MUDA MREFU KUTUFIKISHA KATIKA TAIFA JIPYA.
    MATAIFA YA KIAFRIKA AMBAYO HAWAKUPITIA MIFUMO KAMA YETU KISIASA WAMEGUNDUA FAIDA MAPEMA YA SEKTA NYINGI ZA KIUCHUMI NA KUSONGA MBELE.
    NI LAZIMA TUKAKUBALI KUWA KIZAZI CHETU KIPYA TUWAELEKEZE KWENYE USTAARABU HUU ILI WAWEZE KWENDA NA WAKATI.
    KUNA MENGI AMBAYO HAYAHITAJI USOME YANAHITAJI MTU MWENYE AKILI TIMAMU TU INATOSHA LAKINI MIFANO MSHAANZA KUIONA KWENYE KUTAFUTA KATIBA BADO VIONGOZI WETU WANA SHIKILIA ASILI ZAO HAWAONI UMUHIMU WA KUPATA KATIBA MPYA WANATAKA ILE ILE IENDELEE KUTIWA VIRAKA AU KWA LUGHA YAO MPYA KUBORESHWA HAO NDIO WANA UJAMAA.
    MIMI NAHAMIA KENYA HAPA NAONA ISHATOSHA MANENO MENGI VITENDO KIDOGO TAIFA HILI KWAHERINI.
    MDAU.
    NAMANGA/UPANDE WA KENYA.

    ReplyDelete
  27. Wanaotunyima uraia pacha wanapoteza muda wao kutokana na chuki na husda tu. Mbona wazanzibari wana uraia pacha wa Zanzibar na Tanzania na hamuhoji? Mbona wahindi wana uraia wa nchi zaidi ya tatu na hamuhoji? Mbona vigogo kama Lazaro Nyalandu, Andrew Mgimwa na wengine wana uraia pacha hamuhoji? Mbona akina Januari Makamba wanao hamuhoji? Kwani nikiamua kurudi Tanzania na uraia pacha mtanisachi na kujua? Wakati wa kurudi unaingia na pasi ya Tanzania na unaondoka na pasi ya kigeni simple. Tumeishafanya hivyo mara nyingi tu na hakuna nomi.

    ReplyDelete
  28. A hypothetical question; If the so called Tanzanians residing abroad want to have dual citizenship just to avoid paying for a visa when coming back home and further claim to bring development etc then why not surrender their current status quo as foreigners and return back permanently by seeking a Tanzanian citizenship? Development can only come around when a person is 'parked'permanently and not by 'dropping in' as when they feel to?

    ReplyDelete
  29. Nakubaliana na wachangiaji wengi kuhusiana na uwezo wa john. Huyu kijana ni genius kusema kweli, sema hao wenzske siyo serious. Tanzania ya sasa, ni wachache sana wenye vipaji kama John. Myika angekuwa na upeo mkubwa kama wa mashaka, niseme angekuwa karibu kidofo, ila mnyika is too local . Diasoora, nawapa siri moja, muweni seriius. Narudia, muwe seriius. Nimeongea na wenzangu kadhaa, lakini wote tunakubakiana kwamba hamko serious. Mnawezaje kumtuma mtu mmoja? Alafu Nyie Mtu kama Benjamin mwaipaja utasema ni mtu serious kupewa nafasi yoyote ya uongozi wakati anasifia rais handsome ?
    Diaspora jipangeni sana ili swala kenu lipate nafasi ya kupita. Nikiwa kwenye bunge la katika, sijamuona hata mmoja wenu anayeweza kuwashawishi wabunge hata kuwafikiria. Huyu mwakilishi wa sasa is not convincing At all. Kama kweli mko serious, fanyeni vitu in a serious way, muwatume wenzenu wenye uwezo kama 5 au 7 kuja hapa Dodoma, ila siyo the type of Benja Mwaipaja.

    ReplyDelete
  30. Mimi nataka kujua hiyo haki ya kuzaliwa watu wamenyang'aywa na nani?

    ReplyDelete
  31. Ndiyo, kuna mijitu mingine imeng;ang'ania Dar kujifanya ndo kwao na huko sweken tangu waondoke hawataki kusikia baki ya kuenda.Eti na huko diaspora ni wapi japo najua ni maeneo ya katavi. Hili swala laweza leta songombingo kama katiba mpya sababu ya kukosa moyo safi na nia njema.

    ReplyDelete
  32. Broo Mashaka,ujuwe pale wanasiasa wanapotokwa na machozi uwanja wa ndege kuipokea maiti ya mwanadiaspora hupatwa na hisia za kuwa Mzawa huyu au mzalendo huyu masikini kaikimbia nchi yake na hakuifanyia lolote na leo akiwa ni mzoga anarudi nyumbani bila taifa hili kufaidika na lolote.Hiyo ndio mana halisi ya viji machozi vile vinavyowapukutika na sio vyengine..

    ReplyDelete
  33. Mimi sihitaji uraia wa nchi mbili. Nimezaliwa Tanzania, na Tanzania ndio nyumbani. Nimechukua pasi ya Marekani, Canada na Uingereza. Elimu yangu, ndoa na kazi ndio zimenipa hizo pasi, kihalali.

    Nakuja Tanzania kila mwaka kusalimia wazazi na jamaa. Napewa visa yangu ubalozi wa Tanzania kwa kuwa kuna mstari mrefu uwanja wa ndege Dar. Bangkok wananipa visa kama ya Tanzania lakini inachukua dakika 20, sio masaa matatu.

    Sioni umuhimu wowote wa kuwa na pasi ya Tanzania. Sijaukana uraia wangu kwa kuwa sharia imeshasema kuwa nikichukua uraia mwingine, mimi sio raia wa Tanzania tena. Nilikwenda wizara ya ndani, wanataka nisubiri mwezi mpaka maombi yangu ya kuukana upitishwe. Nani ana muda huo. Tangu nichukue uraia mwingine, sitatumia tena pasi ya Tanzania. Na cha kushangaza na kutia huruma, mgeni uwanja wa ndege anaheshimiwa kuliko raia. Naona wazungu wanapita "green zone" lakini akipita raia anasimamishwa.

    Tanzania ni moya ya nchi masikini sana duniani na mpaka sasa raia wengi hawana elimu, maji safi, umeme wala tiba bora. Haki za binadamu kila siku haziheshimiki. Kansa ya Hongo imezagaa katika kila sekta ya uchumi. Asilimia 40% au zaidi ya bajeti ya nchi tunaomba wageni tangu uhuru!

    Serikali ya Tanzania kwa ujumla inanihitaji mimi kuliko mimi kuihitaji Tanzania. Kupitishga sharia ya uraia pacha hautaleta utajiri kesho. Kama ni hivyo, basi India na Philippines wangekuwa matajiri sana kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi wao wanafanya kazi nje na uraia pacha unaruhusiwa. Maendeleo yanakuja kwa kuchapa kazi, kuwa na elimu bora, kuwa na sheria zinazomlinda mtu haki yake, na serikali iliyomheshimu mfanyabiashara. Nipo nje sasa miaka 20, na kila mwaka ninapokuja naona maghorofa tu yanajengwa, sinema, makampuni ya simu na ulevi. Maendeleo ni kutengeneza magari wenyewe, kuuza bidhaa zinazotumiwa na wengi. Mpaka nitakapoona bidhaa za Tanzania zaidi ya kahawa na chai katika maduka ya ulaya, ndio nitaamini kweli Tanzania kuna maendeleo.

    ReplyDelete
  34. Ndugu Mashaka,

    Uraia pacha kama ulivyo Uchumi una FAIDA NA HASARA ZAKE.

    Serikali inalifahamu hili sana.

    Nchi kama Kenya, Uaganda na Rwanda majirani zetu mnazotolea mfano mara kwa mara zilizo amua kukubaliana na suala la Uraia pacha wameamua kuchukua upande wa FAIDA pekee na kupotezea upande wa HASARA ZAKE!

    Hivyo basi JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kama nchi makini na watu wake walio makini sana hata ktk mapendekezo ya Katiba yake mpya wameamua kukataa na kuzingatia zaidi upande wa HASARA ZA URAIA PACHA!

    Hakuna matatizo, tupo damu damu, mkija tutawatembeza kwenye Mabanda, Gongo letu kali sana na sio Wghisky, tutawafikisha Maskani zetu Mkavute kwa wale ambao wanavuta na huduma zingine nyingi tu za mahitaji ya ziada na ya kibinaadamu mtapata mkija kutembea Tanzania kama wageni!

    Hivyo undugu na ninyi Madiaspora kamwe hauwezi kufa, haujakufa mtaendelea kuja Tanzania kama wageni kwenye nchi yenu ya asili!

    ReplyDelete
  35. Madiaspora,

    Uwekezaji wa fedha Kiasi gani, US$ BILIONI NGAPI? mnaotaka kuutumia ili mpewe Uraia na Pasipoti ya Tanzania?

    Acheni upuuzi, acheni Usanii wenu wa Kughushi Bank Statement mlio utumia mkiomba visa za kwenda Majuu!

    Mlete hoja za maana lakini sio kudai Uraia mlio ukana hapo mwanzo kwa kigezo cha kutaka kuja kuwekeza nchini (ANGALIENI MNACHANGISHANA US$ 25,000.00 KUTEKELEZA MHCKATO WA HOJA YENU, JE HAWA MABILIONEA WA DUNIA NA US$ ZA KIMAREKANI WALIOLETA MITAJI YAO KUWEKEZA TANZANIA MBONA HAWAJADAI URAIA NA PASIPOTI?), kama mlikuwa na nia njema muda wote huo mlikuwa wapi msifanye kitu huku Tanzania eti hadi mpewe tena Uraia?

    ReplyDelete
  36. Wewe umezaliwa ukiwa unaitwa Jina lako CHAKUBANGA na leo unajiita JOHN SHIMTH ukiwa Majuu na ukaukana Uraia wa Tanzania na leo unataka urudishiwe tena Utanzania?

    ReplyDelete
  37. Nendeni KENYA, UGANDA AMA RWANDA MKAPATE HAKI YENU YA KUZALIWA, HII YOTE SI AFRIKA YA MASHARIKI?

    Hii TANZANIA ni nchi ya NYUNDO na JEMBE, hakuna URAIA PACHA!

    ReplyDelete
  38. John Mashaka na wenzako huko Majuu:

    Ni uamuzi wa kupiga moyo konde!

    Mchague moja kuacha kazi Bank of America na Wells Fargo, kuukana Uraia wa Marekani na kuja kufanya kazi NBC, CRDB ,NMB na Benki ya Posta (TPB).

    Suala si Benki tu, kama Marekani na Obama wana Mabenki na sisi Tanzania na Kikwete pia si Mabenki tunayo?

    ReplyDelete
  39. Madiaspora wengi mmesoma kama hamkusoma vile?

    Unakuta mtu anakaa miaka kibao nje bila kurudi TZ je unafikiri Uraia wako utakuwepo tu?

    Nchi nyingi ikiwemo huko Marekani mliko Raia yeyote atakaye kaa nje ya US kwa zaid ya mwaka Uraia wake unapotea automatically!

    ReplyDelete
  40. Haya maoni nimeandika kwa habari nyingine nayarudia, Mdau #5, Kwanza kabisa, Namwombea kwa Mungu ampuzike pema peponi Ndugu Lukindo. Pili mdau#5 maswali yako ni ya kijinga, unapouliza, "miaka yote hiyo, je hakuwahi kuwasiliana na familia yake bongo?" Hivi maiti inaweza kukujibu?(na wakati wa kilio si wakati wa kuongea ujinga) na mawazo kama yako unadhani ndugu yako anaweza kuwa na moyo wa kukutafuta? Halafu wewe unasema wakati wa kifo ndiyo wanakutafuta. Hivi wewe umesoma hii habari?!! Hapa kweli marehemu anatafuta ndugu zake au watu walio hai? Kwa mawazo kama haya ndiyo maana hatufikii mbali jamani. Tusemage ukweli, maiti haina haya. Na hii ndiyo hali halisi. Endeleni tu kuongea pumba, sijui waliukana uraia, sijui wanajidai, na dharau nyingi(wabeba maboksi), mwisho tutavuna tulichopanda. Na sasa haivi mnawakatalia ndugu zenu huo uraia pacha, ambao na nyie sio wenu, sasa mnadhani watapata moyo wa kuwasaliana na nyinyi? Ndugu Lukindo mie naona alikuwa amejipanga vizuri tu. Kwani kabla ya kupumzika alishasema anataka mwili wake uchomwe na hii ni kupunguza gharama za kurudisha mwili Bongo. Na unaposema labda alikuwa awasiliani na ndugu, ni kweli inawezakana kuwa hivyo, maana kwa kauli za fitina, wivu, na uongo wabongo wachache wanazotoa kwa ndugu zao wanaDiaspora sasa hivi inawezakana zilimkatisha tamaa. Marehemu ana shida, yeye kampuzika najua labda ndugu zake(watoto na mke), ambao ni haki yao wanataka kujua ndugu zao wa TZ, lakini sasa kwa kauli kama zinazotolewa humu labda ndiyo maana marehemu akutaka ata kujuna na ndugu zake. Ndiyo maana inabidi tupiganie uraia pacha. *Mmbongo Chiberia*

    ReplyDelete
  41. Mdau huyu mtazameni:

    ........................
    ujinga wetu, badala ya kuona uzito wa mada aliyoileta bwana mashaka, wengine wanageuka kumjadili na kumuita jini wa michuzi. grow up people. tunataka uraia pacha. tunataka haki yetu ya kuzaliwa
    ........................

    NINYI MADIASPORA MNALILIA HAKI YENU YA KUZALIWA (mpewe Uraia pacha) WAKATI HIYO HIYO PASIPOTI YA RAISI KIKWETE MNAYOOMBA NA KUPIGA KELELE SASA MLIKWISHA IHARISHIA MLIPOFIKA HUKO MAJUU NA RAISI KIKWETE MKAMNYEA MIKONONI...JE ITAKUWAJE HAPA MNALIA LIA TENA?

    ReplyDelete
  42. ndugu watanzania na wafrica wote suala la uraia wanchi mbili. huo hauwezi kupukika kwa sababu za uchumi wa nchi naulinzi wa nchi kwasababu.nyie mliondani mna linda ndani nasisi mnaosema tupo nje tunalinda masirahi ya nchi zetu tukiwa huku nje ya mipaka ya nchi zetu. wahiyo wote tuna hakisawa.kuhakikisa nchi zetu zina amani.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...