Na Mwandishi Wetu
Machi 9 mwaka huu Tanzania itaungana na nchi nyingine za Afrika wanachama wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) kuadhimisha siku ya APRM barani humu.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa APRM Tanzania, Hassan Abbas alisema azimio la kusherehekea Siku ya APRM lilipitishwa Januari mwaka jana katika kikao cha Wakuu wa Nchi za APRM kilichofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.
“Kikao cha Wakuu wa Nchi za APRM ambacho pia Rais wetu Dkt Jakaya Kikwete alihudhuria kilikuwa cha kihistoria katika miaka 11 hii tangu kuanzishwa kwa taasisi hii ya Kiafrika ya APRM.
“Ni katika kikao hicho ambapo Rais Kikwete aliwasilisha kwa mafanikio ripoti ya tathmini ya Hali ya Utawala Bora ya Tanzania iliyoandaliwa na wataalamu wa APRM kwa kuwashirikisha wananchi wa Tanzania lakini pia kulipitishwa azimio la kuifanya Machi 9 ya kila mwaka kuwa Siku ya APRM,” alisema Bw. Abbas.
Aliongeza kuwa APRM ilianzishwa rasmi Machi 9 mwaka 2003 hivyo Wakuu wa Nchi za APRM waliazimia kuwa pamoja na shughuli za kila siku za kuchagiza utawala bora lakini kila mwaka ifikapo tarehe hiyo kufanyike shughuli mbalimbali kote Afrika.
Bw. Abbas aliongeza kuwa kwa kuwa lengo kuu la Siku ya APRM ni kuongeza uelewa wa umma katika nchi wanachama na Afrika kwa ujumla kuhusu chimbuko, muktadha na faida za APRM katika kukuza utawala bora, APRM tawi la Tanzania nalo limepanga matukio kadhaa.
“Kubwa ni kuendelea kuelimisha umma kuhusu mchakato ulipofikia hapa nchini. Machi 9 tutaeleza kwa waandishi wa habari kuhusu tathmini hii ilipofikia hapa nchini na kutoa msimamo wa APRM kuhusu masuala muhimu ya Kitaifa kama mchakato wa Katiba.
“APRM Tanzania imeamua kuwa matukio ya kuadhimisha Siku hii yatahusisha shughuli mbalimbali zaidi ya hiyo Machi 9. Katika mwezi huu tutafanya makongamano kwenye baadhi ya vyuo na tunatarajia baadaye tutazindua na kuisambaza Ripoti,” alisema.
APRM ni Mpango ulioasisiwa na Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) na unalenga katika kuwashirikisha wananchi ili kushirikiana na Serikali zao kubaini changamoto za utawala bora ili zifanyiwekazi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 kati ya 54 za AU zilizokwishajiunga na Mpango huu. Tanzania imekamilisha hatua zote za awali za tathmini ya APRM na hivi karibuni Ripoti itazinduliwa na kusambazwa kwa wadau wote.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...