Wauzaji wa Nyama wakiwa nje ya mabucha yao baada ya kugoma kuuza nyama. |
Baadhi ya mabucha yaliyofungwa. |
Na Dixon Busagaga wa
Globu ya Jamii, Moshi
Globu ya Jamii, Moshi
WAKAZI wa mji Manispaa ya Moshi, wametaabika kwa siku mbili sasa
wakiwa hawapati kitoweo cha Nyama baada ya halmashauri ya manispaa
hiyo na mamlaka ya udhibiti wa Chakula na dawa TFDA kuyafunga maduka
ya nyama ambayo hayakidhi vigezo vya afya.
Katika hali inayoonesha kuwapo kwa mgomo wa wauza nyama,pamoja na
manispaa kuyafunga maduka sita tu ambayo yalibainika kutokidhi
vigezo, katika manispaa hiyo yenye maduka zaidi ya 50, lakini hakuna
hata moja linaloendelea na biashara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Damian Temba alisema
pamoja na kwamba manispaa ilitoa muda wa wafanyabiashara kuyafanyia
marekebisho maduka yao lakini bado masharti waliyoweka
hayatekelezeki.
"Tulipewa notisi yenye masharti 16, ikiwamo bucha kuwa na kiyoyozi,
msumeno maalum wa kukata nyama, kuwapo kwa vioo na leseni ya
TFDA.......hii misumeno haipatikani na iliyopo haina ubora na bei yake
ni Zaidi ya Mil 1 ambayo ni vigumu kuinunua"alisema.
Alisema maduka mengi yamefanyiwa ukarabati uliohitajika lakini baadhi
yao walilipa fedha ili kupata kibali cha TFDA lakini bado hawajaletewa
jambo ambalo limeendelea kukwamisha jitihada zao za kutimiza masharti
yaliyowekwa.
Hata hivyo wafanyabiashara hao walisema wakati manispaa ikifunga
maduka yao, hali ni tofauti katika machinjio yanayomilikiwa na manispaa
hiyo ambayo walidai ni machafu na hayakidhi vigezo vilivyowekwa na TFDA.
"Manispaa haitutendei haki hata kidogo, machinjio ni machafu mno,
yanahatarisha afya za walaji,lakini hawaangalii hilo,wanatubana na
maduka yetu ambayo tayari yamekamilika na kilichokosekana ni
misumeno ambayo hata hivyo nayo haina ubora"alisema.
Alisema waliagizwa kwenda kujifunza maduka ya mfano mkoani Dodoma
lakini pamoja na kuyaona hayatofautiani na waliyonayo jambo
linalowatia shaka kama haki inatendeka au la.
Kwa mujibu wa notisi ya manispaa hiyo ya Novemba 20, 2013 yenye
kumbukumbu namba MMC HO/7012/Vol III/132 na kusainiwa na afisa afya wa
manispaa hiyo V.M Makundi lilitaja wahudumu kuvaa sare,kupimwa afya
kila miezi 6 na yapigwe rangi nyeupe ndani.
Masharti mengine ni pamoja na chumba cha duka kiwe na ukubwa wa Mita
tatu kwa mita mbili, sinki la maji, kutokutumia magogo kucharanga
nyama na kutoruhusu wateja kugusa nyama wakati wa ununuzi.
Hata hivyo mwendesha mashtaka katika idara ya afya ya manispaa hiyo,
Godfrey Meela alisema tayari manispaa hiyo imewaburuza mahakamani
wafanyabiashara wanne ambao wameshindwa kutekeleza maagizo ya TFDA na
manispaa hiyo kwa kutokidhi vigezo vya afya.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara katika soko kuu mjini Moshi
wanaoza vyakula, Halina Abdala na Zuleha Kasimu walisema wamekosa wateja kutokana kukosa
kitoweo hicho.
Tatito Watanzania tumekuwa na tabia ya kuhalalisha uvunjaji wa sheria.sasa hawa wanacho gomea ni nini? Wengu wao wamekuwa wakifanya biashara hii kwa zaidi ya miaka 10 huku wakiweka afya za walaji rehani.Leo hii unaambiwa ununue msumeno wa tsh.1m unaona ghali.nyie mnaona ni bora tuendelee kula nyama na vipande vya mbao!. TFDA msiwalegezee hawa hata kidogo..
ReplyDeleteBora wamefunga hayo mabucha manake picha tu ni machafu mno yaani siamini wanauza nyama na watu wanananunua. Uchafu unatisha hadi kinyaa.
ReplyDelete