Na Mwandishi Maalum
 Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, inaendelea kujizoelea umaarufu kwa kupanua wigo wake wa ushirikiano na vituo mbalimbali vya utangazaji katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Tanzania na Marekani. 
 Hii ni kwa mujibu wa Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, iliyowasilishwa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Habari ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma, Bw Peter-Launsky Tieffenthel Kamati ya Habari imeanza mkutano wake wa wiki mbili siku ya jumatatu, ambapo pamoja na mambo mengine imepokea na itazijadili taarifa tatu za Katibu Mkuu. 
Taarifa hizo zinaainisha utendaji kazi wa Idara ya Mawasiliano ya Umma katika maeneo mbalimbali kwa kipindi cha mwaka uliopita. Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu inabainisha kwamba Radio ya Umoja wa Mataifa imeendelea na juhudi zake za kuwafikia wasikilizaji wengi zaidi katika maeneo mbalimbali duniani kwa kutumia njia anuai ikiwa ni pamoja na kutafuta washirika wapya. Katika eneo hilo la Radio, taarifa imeeleza zaidi kuwa, kitendo cha kuajiri wafanyakazi zaidi katika Radio ya Kiswahili na Radio ya Kireno kumechangia kwa kiasi kikubwa kasi ya ongezeko la washirika wapi wanaotangaza habari za Umoja wa Mataifa zinazotayarishwa na Radio hizo. Radio hiyo ya Kiswahili imeongeza washirika wapya 15. 
 Akichangia majadiliano ya jumla ya taarifa hizo za Katibu Mkuu, Balozi Ramadhani Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesifu na kupongeza juhudi hizo za watumishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kwa kujituma kwao na kuongeza idadi wa washirika. 
Balozi Mwinyi amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia mafanikio hayo kwa kile alichosema Umoja wa Mataifa kupitia Idara yake ya Mawasiliano ya Umma imeendelea kuthamini na kutambua mchango wa lugha ya Kiswahili katika usambazaji wa taarifa za kazi zake kwa wananchi wengi zaidi. 
Lugha rasmi zinazotambulika katika shughuli za Umoja wa Mataifa ni sita ambazo ni kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kirusi, Kichina na Kihispania. Kiingereza na Kifaransa zinatambulika pia kama lugha za kufanyia kazi.
Hata hivyo katika juhudi za Umoja wa Mataifa za kutaka kuwafikia watu wengi zaidi duniani kote nje ya lugha hizo sita iliamua kwa makusudi kuanzisha idhaa hizo za Kiswahili na Kireno. 
Idhaa hiyo ya Kiswahili ambayo Mkuu wake ni Mtanzania Bi Flora Nducha, kuna pia watanzania wengine wawili, na hivyo kufanya idadi ya watanzania kuwa watatu na watumishi wengine wawili wanatoka Uganda na Kenya. 
Katika hatua nyingine, Balozi Mwinyi ameitaka Idara ya Mawasilano ya Umma, kuhakisha kwamba vyombo asilia vya habari kwa maana ya radio na magazeti vinaendelea kupewa umuhimu katika shughuli za Umoja wa Mataifa kwa kile alichosema ni vyombo ambavyo bado vinaendelea kuwa tegemeo kubwa hususani katika nchi zinazoendelea. 
Aidha Balozi Mwinyi ameishauri Idara hiyo ya Mawasiliano ya Umma, kuimarisha uhusiano, ushirikiano na kufanya kazi kwa karibu, na Vituo vya Habari vya Umoja ambavyo vipo katika nchi mbalimbali. 
Akasema vituo hivyo vya habari vimeendelea kutoa mchango mkubwa katika utoaji na usambazaji siyo tu wa shughuli za Umoja wa Mataifa, bali pia vimekuwa vikichangia katika kampeni za mbalimbali za uhamasishaji wa umma katika maeneo mbalimbali.
Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akichangia majadiliano ya jumla ya mkutano wa  36 wa Kamati ya  Habari ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  katika mchango wake  Balozi  pamoja na mambo mengine alipongeza juhudi zinazoonyeshwa na wafanyakazi wa Idhaa  ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kwa kupanua wigo wa washirika wake. Na kupongeza pia Idara ya Mawasiliano ya Umma kwa kuendelea kukienzi Kiswahili

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. ndugu Balozi wa Umoja wa Mataifa kwa mafanikio makubwa kwa kupanua wigo katika idhaa ya kiswahi nnawapeni pengezi sana katika kufanikisha kwa kupanua Kiswahili kupitia katika Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Ombi langu kwa baadae ipatikane TV ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ili kuelimisha zaidi kupitia Luninga kwa wafirika na watu wengine duniani wanaokipenda kiswahili.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...