SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATC) lipo karibu kuanza
kung’ara hewani baada ya mwekezaji kutoka Oman
kuwa tayari kuwekeza kwenye shirika hilo na sasa
anasubiri serikali kukamilisha taratibu zake.
Miongoni mwa taratibu zinazosubiriwa ni kwa serikali
kulipa madeni makubwa ambayo ATC ilikuwa inadaiwa
ili kuweka mizania sawa ya vitabu vya hesabu za fedha.
Mwenyekiti na Rais wa Kampuni za Al Hayat
Development and Investment LLC ya Oman, Sheikh
Salim Bin Abdullah Al Harthy, alisema wana dhamira ya
dhati ya kuwekeza hapa nchini na hasa katika ATC.
“Tunatarajia kuwekeza kwenye maeneo tofauti katika
sekta za mafuta na uendelezaji wa maeneo ya fukwe,
lakini lengo letu kuu ni kuwekeza ATC,” alisema Sheikh
Salim na kuwa awamu ya kwanza watatumia sh, bilioni
160.
“Mpango wetu ni kujenga kituo cha mafunzo ya masuala
ya ndege, ofisi nzuri kwa ajili ya ATC, kununua ndege
na kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Tunatarajia
kufanya haya katika kipindi kifupi kijacho," alisema.
Alifafanua kuwa kuna wakati Kampuni ya Al Hayat
ilikaa kimya kuhusu uwekezaji huo na kuwa ilifanya
hivyo ili kutoa nafasi kwa serikali kukamilisha taratibu
zake ikiwemo kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya
kampuni hiyo na ATC.
Alisema watendaji wa kampuni ya Al Hayat wamekuwa
wakitembelea Tanzania mara kwa mara ili kufuatilia
suala zima katika uwekezaji kwenye ATC.
Sheikh Salim alisema ni kutokana na hali hiyo ndiyo
maana hata ule mpango wa kununua ndege aina ya
Bombadier, Air Bus na Embraer ulisimama kidogo kwa
kuwa mkataba rasmi wa uwekezaji bado haujafikiwa na
kutiwa saini.
Alisema safari hii wamekuja tena kuitikia wito wa ATC ili
kuendeleza makubaliano yaliyofikiwa na kuwa taratibu
zikikamilika watatia saini mkataba na kuanza uwekezaji.
Sheikh Salim alisema suala hili limechukua muda
mrefu kutokana na taratibu husika zinazohusu pande
zote, lakini anasisitiza azma ya kuwekeza iko pale pale
kwa kuwa linahusisha mambo mbalimbali ikiwemo ya
kisheria.
Hata hivyo, anasema kuna uwezekano mkubwa ndani
ya miezi sita tangu sasa kila kitu kitakuwa kimekamilika
na ATC itarudi kung’ara angani kwa kuwa serikali
inatoa ushirikiano mkubwa na wa kutosha.
Kuhusu utoaji wa huduma, Sheikh Salim anasema
lengo ni kuhakikisha inafika katika mikoa mingi kadri
iwezekanavyo na nchi jirani, na kufanya safari za mbali
katika nchi kama Uingereza na India.
Baada ya kukaribishwa na Sultani Qaboos kufanya
ziara Oman, Rais Jakaya Kikwete alikutana na
wafanyabiashara wan chi hiyo na kuwakaribisha kuja
kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.
Hivyo uwekezaji wa Al Hayat umetokana na jitihaza
zilizofanywa na Rais Kikwete katika ziara yake nchini
humo.
Kwa sasa ATC inafanya safari zake katika mikoa ya
Mtwara, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dar es Salaam,
Mbeya na katika nchi za Burundi na Comoro. Hivi
karibuni itaanzisha safari za Zanzibar na Kilimanjaro.
Hongera serikali kwa kuturejeshea ndege yetu ya taifa maana hizi kampuni nyingine zinakuja na mambo ya ajabu ajabu, tunataka twiga wetu arudi angani
ReplyDelete