Wananchi wakisubiri kesi zao zianze.

Na Edwin Moshi wa Globu ya Jamii, Makete
Watuhumiwa na walalamikaji mbalimbali wenye kesi zao katika mahakama ya wilaya ya Makete mkoani Njombe wameendelea kuonja tena machungu ya kuahirishiwa kesi zao leo Ijumaa Mei 09, kwa kile kilichoelezwa kuwa hakimu kushindwa kufika

Wakisikika wakiongea mahakamani hapo wakiwa katika makundi makundi, wamesema hawakatai wao kuahirishiwa kesi zao ila zinapoahirishwa mara kwa mara kwa muda mrefu inawaumiza wananchi ukizingatia wengi wao wanatumia fedha nyingi ili kuweza kuhudhuria mahakamani
Wakisikiliza taarifa ya kuahirishiwa kesi zao.
"Hakimu wa wilaya sisi hatuna, hebu fikiria mara ya mwisho hakimu amefika hapa mwezi wa Februari akasikiliza kesi zetu vizuri tu, lakini tangu hapo tumekuwa tukiahirishiwa tu kesi kila tukija, na sababu tunaambiwa hakimu ametingwa na majukumu mengine, sasa jamani hii kero ni hadi lini" alisikika mmoja wa waliofika mahakamani hapo akizungumza

Licha ya kuongezeka kwa kesi na huduma mbalimbali za kimahakama katika mahakama ya wilaya ya Makete, bado wilaya hiyo imeendelea kusota kwa kukosa hakimu wa mahakama hiyo hivyo hakimu kutoka mahakama ya Njombe hulazimika kuja kuendesha kesi katika mahakama ya wilaya ya Makete na mahakama yake ya Njombe

Kutokana na jiografia ya Makete, mtu mwenye kesi katika mahakama ya wilaya kama yupo nje ya Makete mjini hulazimika kutumia gharama kubwa za kusafiri hadi kufika mahakamani kutokana na uhaba wa magari ya usafiri

"Kwa mfano sisi tuliahirishiwa kesi juzi tarehe 30 Aprili tukaambiwa tuje leo, bado na leo ni kama yale yale tu, mimi naiomba serikali itupe hakimu wetu kwa sababu huyu hakimu anatoka Njombe na huko ana kazi za kimahakama yake pia sasa akitingwa si rahisi kuja huku" amesema mwananchi mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake

Akitoa taarifa ya kuahirishwa kesi hizo hii leo Mkuu wa polisi wilaya ya Makete (OCD) Alfred Kasonde amewapa pole wananchi hao wenye kesi mahakamani hapo na kusema anawaomba wawe wavumilivu, na kesi zao zimeahirishwa hadi Mei 23 mwaka huu
Wakiondoka baada ya kesi zao kuahirishwa.
"Jamani naimani mmenisikia jinsi nivyokuwa nazungumza nao kwenye simu, nimewaeleza hali halisi lakini ndio hivyo tena, mimi nawaomba muwe wavumilivu yatakwisha tu, kila kitu kitakwenda sawa, naombeni mje kwa ajili ya kesi zenu tarehe 23 mwezi huu, poleni sana" amesema Kasonde

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 10, 2014

    Tena hapa ukiuliza utasikia waliowengi kesi zao ni zile ambazo uamuzi wake ni kusameheana tu.....maarufu kama kesi za wizi wa kuku.....au kumtusi jerani......

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...