Na: Hassan Hamad (OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea haja ya kuwashajiisha wakulima kulima kwa wingi mazao yanayopendwa zaidi na wananchi, ili kupunguza mfumko wa bei hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Akitembelea masoko ya Chake Chake na Wete Kisiwani Pemba kuangalia bei za bidhaa mbali mbali zikiwemo za matunda, Maalim Seif amesema licha na kuwepo bidhaa nyingi lakini bei zake bado ziko juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi.

Amesema ili kupunguza tatizo hilo, hakuna budi kwa wakulima kutoa kipaumbele kwa mazao yanayotumiwa zaidi na wananchi katika kipindi cha Ramadhani yakiwemo ndizi, majimbi na viazi vitamu, ili kuepuka kuagiza mazao hayo nje ya Zanzibar. Hata hivyo Maalim Seif amesema bei ya baadhi za bidhaa inaridhisha kisiwani Pemba ikilinganishwa na Unguja, licha ya kuwepo bidhaa ambazo pia ziko juu kuliko Unguja, hali inayotokana na upatikanaji wa bidhaa hizo katika maeneo husika.

Baadhi ya wafanyabiashara katika masoko ya Wete na Chake Chake, wamesema wanalazimika kuuza bidhaa hizo kwa bei ya juu kutokana na wao kuuziwa kwa bei ya juu kwenye minada ya bidhaa hizo, ambapo baadhi yake zikiwemo viazi vitamu na majimbi hutoka maeneo ya Tanga. Wakati huo huo Maalim Seif ametembelea Bwawa la kufugia samaki Kiuyu Minungwini, na kuelezea kuridhishwa na maendeleo yaliyopatikana katika ufugaji wa samaki.

Amesema iwapo ufugaji wa samaki utaendelezwa, utasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wengi wanaomaliza masomo na kuongeza kipato chao. Amefahamisha kuwa wajibu wa serikali ni kuwajengea wananchi mazingira ya kuweza kujiajiri kwa vile haina uwezo wa kuajiri watu wote, na kwamba wananchi wana wajibu wa kutumia fursa hizo zinazowekwa na serikali kuweza kujiajiri.

Katika kuunga mkono juhudi za wafugaji hao Maalim Seif ameahidi kuwanunulia mashine ya kuvutia maji, ili kurahisisha uingizaji wa maji katika mabwawa hayo ya kufugia samaki. Mapema akisoma risala ya wana kikundi hao wa “Kichakaa si shangi”, Bi. Khadija Khamis amesema wameamua kuendeleza kazi ya ufugaji wa samaki ikiwa ni kuitikia wito wa serikali kwa vitendo.

Amesema tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho cha ufugaji mwaka 1994, wamepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza mabwawa ya kufugia samaki kufikia manane ambapo sasa wanajenga bwawa jipya la kitaalamu. Akielezea maendeleo ya ufugaji wa samaki, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdillahi Jihadi Hassan, amesema jumla ya vikundi 144 vya ufugaji wa samaki vimeanzishwa Unguja na Pemba.

Amesema kwa ujumla vijana wamehamasika na wamekuwa wakiwashajiisha wafugaji zaidi kuendeleza ufugaji huo, huku wakitoa taaluma kwa wafugaji ili kuleta ufanisi zaidi. Ameongeza kuwa Wizara yake ina mpango wa kununua boti mbili na kutoa mafunzo kwa wavuvi, ili waweze kutekeleza mrango mkubwa wa uvuvi katika bahari kuu.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihoji bei ya ndizi mbivu katika soko la Wete.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akitembelea soko la Qatar, Chake Chake Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihoji bei ya samaki katika soko la Mtemani Wete. Bei ya samaki hawa ni shilingi 1500 hadi 3000 kwa samaki mmoja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na mfanyabiashara za maboga katika soko Wete.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 17, 2014

    Samaki 3000 pemba tena mmezungukwa na bahari si hatari

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 18, 2014

    Maalimu nunua hao samaki. Si umemuona bosi wako JK juzi kanunua Ng'oda kwa laki mbili?

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 18, 2014

    Hili soko naona linahitaji kuboreshwa zaidi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...