BENDI mbili za muziki wa dansi, Akudo Impact, Mashujaa Music pamoja na kundi la mahiri la muziki wa taarab la Jahazi Modern Classic vitasindikiza uzinduzi wa albamu mpya wa msanii, Tarsis Masela (pichani katikati) unaotarajiwa kufanyika Novemba 21 kwenye ukumbi wa Ten Lounge jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es salam leo , Meneja wa mwanamuziki huyo, Ray Matata, alisema kuwa maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika na bendi zote tatu zimethibitisha kutoa burudani siku ya uzinduzi huo.
Matata alisema kuwa wameandaa onyesho ambalo litakuwa ni historia katika muziki wa dansi hapa nchini.
Masela alisema kwamba amejiandaa kuwapa mashabiki wa dansi wa Tanzania burudani yenye ubora na lengo lake ni kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya muziki.
“Huu ni mwaka wa saba niko Tanzania, nimejiandaa kuwapa burudani bora mashabiki wa muziki na kuwaachia zawadi ambayo hawataisahau kwenye tasnia ya muziki wa dansi,” alisema Masela.
Aliongeza kuwa albamu yake anayotarajia kuizindua ina jumla ya nyimbo nane na itajulikana kwa jina la Acha Hizo.
Alizitaja nyimbo zinazounda albamu hiyo kuwa ni pamoja na Tabia Mbaya, Mwiko, Chaguo Langu, Tusiachane, Penzi Langu Limezidi Asali, Vidole Vitatu na Nimevulimia.
Alieleza kwamba katika albamu hiyo ameshirikisha wasanii wa aina mbalimbali ili kuifanya iwe na ubora kwa kupendwa na wadau wa rika tofauti.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa bendi ya Mashujaa, Maximillian Luhanga, alisema kwamba wamekubali kusindikiza uzinduzi wa albamu hiyo kwa kuheshimu kipaji cha Masela na kutaka kuendelea wasanii wa muziki wa dansi.
Luhanga alisema kwamba hiyo itaondoka ile dhana ya wasanii wa dansi hawapendani na amewataka wanamuziki wengine kufuata nyayo za msanii huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...