Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw.
Ephraimu Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
kuhusu mfumuko wa bei nchini.
Baadi
ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya
Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo leo jijini
Dar es salaam alipokuwa akizungumzia suala la mfumuko wa bei nchini.(Picha
na Eleuteri Mangi-MAELEZO).
Wananchi
wameombwa kutoa ushirikiano wa dhati kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia
ofisi za takwimu za mikoa wakati wa ukusanyaji wa takwimu mbalimbali kwa lengo
la kutoa taarifa zilizo sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Kauli
hiyo imetolewa Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Kwesigabo
amesema kuwa pamoja na mambo mengine Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye
mamlaka ya kutoa taarifa za mfumuko wa bei nchini ambapo kwa mwaka huu
unaonesha umepungua kwa baadhi ya bidhaa za vyakula kuanzia kipindi cha mwezi
Oktoba 2013 hadi Oktoba 2014.
Kwesigabo
amesema kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua bei kwa
mwezi Oktoba 2014 zikilinganishwa na mwezi Oktoba 2013 ni pamoja na bei za
mahindi asilimia 7.2, unga wa mahindi asilimia 5.5 na unga wa ngano asilimia
4.4.
Bidhaa
nyingine za vyakula zilizoonesha kupungua bei ni ulezi asilimia 3.5, tambi
asilimia 2.2, samaki asilimia 4.6, mihogo asilimia 2.1 na sukari imepungua kwa
asilimia 4.6.
Aidha,
Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba 2014 umepungua
hadi asilimia 5.9 kutoka asilimia 6.6 tofauti na hali ilivyokuwa mwezi Septemba
2014. “Hii inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei
za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba 2014 imepungua ikilinganishwa na
kasi iliyokuwepo mwaka ulioishia mwezi Septemba 2014” alisema Kwesigabo.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi Bw. Kwesigabo amesema
kuwa umepungua kwa asilimia 0.2 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.4
kama ilivyokuwa kwa mwezi Septemba mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zimepungua
hadi kufikia 149.70 kwa mwezi Oktoba 2014 kutoka 149.93 za mwezi Septemba 2014.
Kwesigabo
amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni
pamoja na vitafunwa vinavyotokana na unga wa nagano kwa asilimia 2.4, unga wa
mahindi kwa asilimia 0.1, samaki kwa asilimia 1.7,ndizi za kupika kwa asilimia
7.5, mbogamboga kwa asilimia 2.2, viazi mviringo kwa asilimia 1.5 na sukari kwa
asilimia 1.6.
Aidha,
amesema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za
jamii umefikia shilingi 66 na senti 80 kwa mwezo Oktoba 2014 kutoka mwezi
Septemba 2010.
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki
amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini
Kenya umepungua hadi kufikia asilimia 6.43 kwa mwezi Oktoba 2014 ikilinganishwa
na asilimia 6.60 za mwezi Septemba mwaka huu, huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei
umeongezeka hadi asilimia 1.8 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikilinganishwa na 1.4
za mwezi Septemba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...