Fundi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) akifanyia marekebisho moja ya mabasi ya shirika hilo.
 

Wakazi wa Dar es Salaam wataanza kupokea huduma zilizoboreshwa zaidi kila watakapotumia mabasi yanayomilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), hii inatokana na mafunzo ya mwezi mmoja yanayotolewa na shirika kwa madereva, makondakta pamoja na wafanyakazi wengine wa shirika hilo.

Akizungumza wakati wa ziara fupi ya waandishi wa habari katika makao makuu ya UDA jijini Dar es Salaam Jana, Mkuu wa kitengo cha mahusiano ya umma wa UDA, Bw.  George Maziku alisema kuwa miongoni mwa mambo mengine, kampuni yake imejikita katika utoaji wa mafunzo madhubuti kwa wafanyakazi wake ili kuboresha huduma zote zinazotolewa kwa wateja wa UDA.

“Uongozi wa UDA unalichukulia kwa uzito mkubwa sana suala la usalama. Tumeupitia mtaala wa utoaji elimu kwa wafanyakazi wetu lengo likiwa ni kuboresha usalama na kufanya wateja wetu wafurahie huduma zinazotolewa na shirika. Tunatoa mafunzo haya kwa madereva wetu ili kuinua hali yao ya uzingatiaji wa usalama,” alisema Maziku.  

Mbali na masuala ya usalama, mkuu huyo wa kitengo cha uhusiano aliahidi uboreshaji wa huduma kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwajali wateja, suala ambalo limekua likizua mjadala mkubwa.

Bw. Maziku alisema kuwa kampuni yake ina mabasi yapatayo 400 jambo linayoifanya UDA kuwa kampuni ya kwanza Tanzania kuwa na magari mengi yanayofanya kazi kwa mkupuo, hivyo kuna uhitaji mkubwa sana wa kuweka viwango thabiti ambavyo vinaweza kuigwa na makampuni mengine.

“Tunalenga kuwa na mabasi 3000 ifikapo mwakani lakini kikubwa zaidi kabla hata ya kupata idadi hiyo ya mabasi ni kuwapa mafunzo madereva wetu ili wawe na elimu ya kutosha na uzoefu wa kutosha katika sekta ya usafirishaji wa umma.

“Kwa kulitambua hili, kampuni imeajiri wakufunzi kutoka ndani na nje ya nchi, ili kutoa mafunzo kwa madereva wetu na wafanyakazi wengine wanaojihusisha na usafirishaji, mafundi na wafanyakazi wote (hasa makondakta) katika kuwajali wateja,” alisema.

Bw. Maziku alisema kuwa mbali na mafunzo hayo, kampuni imekuwa ikifuatilia kwa karibu sana tabia na  mienendo ya madereva na makondakta wake mara kwa mara kwa kuwatumia wasimamizi ambao hupanda mabasi ya kampuni hiyo bila ya makondakta na madereva kupewa taarifa.

Kwa sasa, mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na kampuni hapo awali, yameonyesha kuzaa matunda yaliyotarajiwa kwa kuwabadilisha baadhi ya madereva na makondakta wa kampuni hiyo.

Hii ilibainika baada ya mkazi wa Dar es Salaam, ambaye amekuwa akitumia huduma za UDA kwa nyakati tofauti, Bw. Andrew Sanga , kukiri kuwa madereva wa UDA wapo tofauti ukilinganisha na madereva wengine wa mabasi ya abiria.


“Ilikuwa ni adha kubwa kutumia usafiri wa umma kutokana na huduma mbovu ambazo abiria tulikua tukikumbana nazo. Madereva wengi wa abiria hawazingatii suala la usalama barabarani. Wanaendesha hovyo  bila kujali kuwa kuna watumiaji wengine wa barabara. Lakini nina furaha kusema kuwa madereva wa UDA wapo tofauti sana na wenzao,” alifafanua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hongereni sana, kwa mtindo huo mtapunguza ajali za makusudi na vifo vya makusudi. Ningependa zaidi kama mungepata mabasi mazuri ya kusafilia toka mkoa kwa mkoa kama shirika lenu ili kupunguza msongamano wa mabasi ya watu binafsi yaliyochoka na kusababisha ajali mara kwa mara. Pateni hata mabasi makubwa mawili mawili kila mkoa yaani linalokwenda na linalorudi kama wafanyavyo wenzetu wa nchi za nje.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...