Hali ya kustaajabisha imejitokeza jioni ya leo katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi,kwa washabiki na wadau wa soka zaidi ya elfu moja (1000) kushindwa kuingia uwanjani wakati wa mtanange uliozikutanisha timu za Azam Fc ya Tanzania na El Merreikh ya Sudan ikiwa ni mchezo wa awali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Hali hiyo imekuja baada ya watu hao waliokuwa na tiketi zao mkononi kuambiwa uwanja umejaa,hivyo hakuna sehemu ya kuwaweka.
Taarifa za chini ya kapeti zinaeleza kuwa,uwingi huo wa watu wenye tiketi zao mikononi,umetokana na ujanja ujanja uliofanywa na baadhi ya wakaguzi wa tiketi waliokuwepo milangoni kwa kucheza michezo michafu ya kutozichana tiketi wakati wa ukaguni na kuja kuziuza tena kwa bei ya juu kwa wale waliokuwa wamekosa tiketi,hali iliyopelekea kutokea hamaki kubwa baada ya kushindwa kuingia uwanjani kutokana na uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watazamaji 7,000, kuonekana kujaa kupita uwezo wake.
Katika mazingira hayo, baadhi ya mashabiki walianza kufoka kwa hasira wakihoji mantiki ya wao kuuziwa tiketi wakati uwanja huo ukiwa hauna uwezo wa kubeba mashabiki wengi, jambo ambalo kwa kiasi fulani liliondoa hali ya utulivu katika milango yote ya kuingilia uwanjani hapo.
Miongoni mwa walioonja joto ya jiwe kwa kushindwa kuingia katika mechi hiyo, ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni na Kocha wa timu ya soka ya Wanawake, Twiga Stars, Rogasian Kaijage.
Wengine ni Mwakilishi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Henry Tandau maofisa wengine wa Programu ya kuvumbua vipaji ya NSSF-Real Madrid Sports Academy, walioambatana na Kayuni,pamoja na baadhi ya waandishi wa habari.
Wakati wanafika tayari mageti yote ya uwanja huo yalikuwa yamefungwa kwani isingewezekana tena watu kuendelea kuingia kutokana na watu waliokuwa wameingia kutosha idadi inayotakiwa kwa mujibu wa uwezo wa uwanja huo,na wakati huo mchezo ulikuwa bado haujaanza.
Kwa mujibu wa waliokuwepo ndani ya uwanja,wametudokeza kuwa Timu ya Azam FC imeibuka kidedea kwa kuwachapa El Merreikh ya Sudani kwa mabao 2-0, yaliyowekwa kimiani na washambuliaji Didier Kavumbagu dakika ya 8 na John Bocco 'Adebayor' dakika ya 77.

Baadhi ya viongozi mbali mbali wa soka nchini akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni (wa pili kushoto) wakiwa nje ya Uwanja wa Azam Complex,Chamanzi baada ya kushindwa kuingia uwanjani hapo kutokana na kufungwa kwa mageti baada ya kuonekana kujaa kwa uwanja huo.
Safi sana Usalama kwanza.
ReplyDeleteNa masuala ya tiketi kuzidi uwezo wa uwanja kuchukua watazamaji inabidi uchunguze.
Maana hali hiyo ya tiketi kuzidi uwezo wa uwanja inaweza kusababisha tafrani maana leo walioshindwa kuingia ni 1,000 na bahati hakukutokea maafa.
TFF , AZAM COMPLEX na wanausalama isije ikaja siku mechi kubwa zaidi na idadi ya walioshindwa kuingia uwanjani ikawa 7,000 na wenye tiketi wakaamua kujaribu kuingia kwa nguvu na kusababisha maafa kama yale ya karibuni Misri.
Mdau