Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na taasisi ya Kimataifa ya Global Peace Foundation katika kuhimiza amani na utulivu Duniani. Maalim Seif amesema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka jumuiya hiyo, ulioongozwa na Rais wake, James Flynn huko ofisini kwake Migomnani mjini Zanzibar. 
Amesema Dunia inakabiliwa na matukio mengi yanayo hatarisha amani na utulivu, hivyo mchango wa jumuiya hiyo ni muhimu katika kupatikana ufumbuzi wa migogoro hiyo na kuwezesha watu kuishi katika hali ya utulivu na kuvumiliana. 
Maalim Seif amesema kwa upande wa Zanzibar kuna kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa watu wake kuishi kwa kuvumiliana, licha ya kuwepo watu wenye imani tafauti za kidini, na itikadi za kisiasa. 
Hata hivyo, Maalim Seif alihimiza juhudi kubwa zichukuliwe kuimarishwa uchumi wa nchi na kuandaliwa mazingira yatakayowezesha kupatikana ajira za kutosha kwa vijana na kuwaletea matumaini mema katika maisha yao. Amesema hatua hizo zitawaepushia kuchukua maamuzi yasiyokuwa ya busara yanayosababishwa na vijana kupoteza mweleko wa kimaisha ambapo matokeo yake ni amani na utulivu wa nchi kuvurugika. 
Naye Rais wa Jumuiya hiyo, James Flynn amesema nguvu kubwa wanazielekeza kusaidia ujenzi wa familia zinazozingatia maadili mema, pamoja na kushirikiana na Serikali za nchi tafauti kusimamia utawala bora ambao una umuhimu wa kipekee katika kudumishwa amani na utulivu.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwajua watu waliohusika kuchoma moto ofisi za chama hicho jimbo la Dimani na baadaye wafikishwe mbele ya mkono wa sheria. 
Maalim Seif amesema hayo wakati alipotembelea ofisi hizo zilizoteketezwa kabisa kwa moto, tukio lililofanywa na watu wasiojuilikana juzi usiku, huko katika eneo la Kisauni Wilaya ya Magharibi Unguja. Katibu Mkuu wa CUF amesema tukio hilo ni la kusikitisha lililolengwa kuchafua hali ya amani na utulivu iliyopo Zanzibar, baada ya kufikiwa maridhiano ya kisiasa yaliyosababisha wananchi kuishi kwa amani. 
“Polisi hili ni tukio baya sana na hili sio la kwanza, kama mtawaachia watu hawa waendelee kufanya haya wataipeleka nchi hii pabaya”, amesema Maalim Seif alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea eneo hilo. 
Aliwataka Polisi katika kufanya kazi yao kwa weledi na wasiingize mitazamo ya kisiasa hata kama kitendo hicho kimefanyiwa CUF, bali walichukulie ni tukio la kihalifu lililopangwa linalohitaji kufanyiwa kazi kwa kina. 
Aidha, aliwataka wananchi hasa wanachama na wafuasi wa CUF wawe watulivu na wala wasilipike kisasi kwa sababu kitendo cha kulipa kisasi kitawafanya nao wanachangia vitendo vya kihalifu. 
“Tunawaomba wanachama wa CUF wawe watulivu katika kipindi hichi na kamwe wasichokozeke kulipiza kisasi, wakifanya hivyo nao watakuwa wanachangia matukio ya kihalifu”, alionya Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais. 
Amesema matukio ya kuchomeana moto ofisi na kushushwa bendera za vyama yameshapitwa na wakati Zanzibar yalijitokeza katika miaka ya 1990 hadi 2005 na yalikomeshwa baada ya maridhiano ya kisiasa, hivyo hayapaswi tena kukaribishwa Zanzibar. 
Katika hatua nyengine, Maalim Seif ameitaka Kamati Tendaji ya chama hicho ibuni njia za kulijenga haraka jengo hilo la ofisi ya jimbo la Dimani katika eneo hilo hilo, ili iweze kutumiwa na wanachama wa eneo hilo. 
Mapema akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa CUF, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani alisema mashuhuda wa tukio hilo walisema watu wasiojuilikana walifika katika ofisi hizo majira ya saa nane usiku wakiwa na gari na waliposhuka waliingiza matairi ya gari ndani ya ofisi na baadaye kuilipua. Bimani alimweza Maalim Seif kuwa kiasi cha shilingi milioni 135 zimepotea kufuatia hujuma hiyo.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Rais wa taasisi ya Kimataifa ya Global Peace Foundation , James Flynn, alipofika ofisini kwake Migombani kwa mazungumzo.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipokea jarida la Grobal Peace Foundation kutoka kwa Rais wa taasisi hiyo  James Flynn, ofisini kwake Migombani.
 Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuangalia ofisi ya (CUF) jimbo la Dimani iliyochomwa moto na watu wasiojulikana hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akitembelea Ofisi ya (CUF) jimbo la Dimani kuangalia uharibifu uliofanywa baada ya ofisi hiyo kuchomwa moto na watu wasiojulikana hivi karibuni.
Picha na Salmin Said, OMKR

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Jengo hilo limekuwa likitumiwa na chama hicho kwa muda sasa. Kwa nini lichomwe sasa? isijekuwa kuna wanaotaka kuchafua hali ya hewa kisiwani hapo. Viongozi wa kisiasa inabidi wawe waangalifu sana kwani uharibifu wowote wa hali ya hewa ya kisiasa itaathdiri zaidi wananchi, uchumi wa nchi na ustawi wa jamii

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...