Kontena la Lori hilo likiwa limewekwa pembeni baada ya kuondolewa kwenye eneo la Ajali.
Picha na mdau Baraka wa Chibiriti

Watu zaidi ya 30 wanasadikiwa kupoteza na maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya sana katika ajali mbaya iliyotokea mapema leo asubuhi,maeneo ya Changarawe,Mafinga Mkoani Iringa,iliyohusisha Lori la Mizigo na Basi la abiria la Kampuni ya Majinja lililokuwa likitokea Mkoani Mbeya kuelekea jijini Dar es salaam.



Ajali hiyo imetokea baada ya Lori hilo la Mizigo lililokuwa likitokea Jijini Dar kuelekea Mbeya kuligonga na kuliangukia basi hilo wakati lililokuwa likikwepa shimo kubwa lililopo katikati ya barabara wakati wakiwa kwenye mwendo walipokuwa wakipishana. 

Hali ya Uokoaji wa maiti na majeruhi walionasa kwenye ajali hiyo bado ni tete na hasa kutokana na ukosefu wa Gesi ya kukata basi hilo kukosekana eneo lote la Mafinga,Juhudi zinafanyika ili kuweza kuokoa majeruhi pamoja na maiti.

Globu ya Jamii inaendelea kufuatilia kwa ukaribu tukio hili ambalo ni la kusikitisha sana na ni msiba mkubwa kwa taifa,na tutaendelea kujuzana kupitia hapa hapa.

Mungu azipokee na kuzilaza mahala pema peponi roho za marehemu wote katika ajali hii na awajaalie kupona kwa haraka majeruhi wote - Amin.
Kwa picha zaidi BOFYA HAPA

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea tarehe 11 Machi, 2015 Mafinga katika Mkoa wa Iringa katika eneo lijulikanalo kwa jina la Changarawe, ambayo imepoteza uhai wa watu zaidi ya 40 waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Ajali hiyo imetokea baada ya basi la Kampuni ya Majinja Express walilokuwa wakisafiria watu hao kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kugongana na lori lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya, hivyo kusababisha kontena lililokuwa limebebwa na lori hilo kuliangukia basi.

 “Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kufuatia taarifa za vifo vya watu zaidi ya 40 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali hii mbaya ambayo imesababisha simanzi na majonzi makubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huu.

“Huu ni msiba mkubwa, na Taifa kwa ujumla limepata pigo kubwa, hivyo naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali hii iliyotokea Mkoani kwako. Naomba, kupitia kwako, rambirambi zangu  na pole nyingi ziwafikie watu wote waliopotelewa ghafla na wapendwa wao.  Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote mahala pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Katika Salamu zake hizo, Rais Kikwete amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa ndugu na jamaa zao, lakini amesema, pamoja na machungu yote ya kupotelewa na ndugu na jamaa zao, anawaomba wafiwa wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao. 
Aidha, Rais Kikwete amehitimisha rambirambi zake kwa  kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema watu wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wapone haraka, ili waweze kuungana tena na ndugu na jamaa zao.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

11 Machi, 2015




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 15 mpaka sasa

  1. Poleni wote mliofiwa na wale walioumia katika ajali hii mbaya.

    ReplyDelete
  2. Hivi tanroads kwa nini hawazibi haya mashimo
    Juzi nami nusu nigongwe na roli njia ya dodoma baada tu ya kibaigwa kama unaenda dom wakati lilipokuwa linakwepa shimo
    Tanroafs mashimo yanatumaliza jamani

    ReplyDelete
  3. Ni UZEMBE mkubwa wa TANROADS wanaacha vijishimo barabara kuu mpaka yanakuwa makubwa na kusababisha ajali mbaya kama hizi, tungekuwa na utaratibu wa kuwajibishana mambo haya yasingetokea.

    ReplyDelete
  4. Audhubillah
    Michuzi, sisi huku wakati wote twapenda kujua habari zinazotokea nyumbani, na ni blog yako ndiyo inayotusaidia. But often we are on the move and use ipads or iphones. So mheshimiwa, why dont you ask wakina Manywele na jamaa hapo mitamboni kucreate apps for the blog
    ibrahim

    ReplyDelete
  5. Mungu azipokee roho zote za marehemu waliofariki katika ajali hii mbaya. Madereva kuweni waangalifu barabarani munasababisha ajali nyingi zinazoweza kuepukika. Na hilo shimo lililosababisha ajali ya watu wengi hivyo, jamani lilishindwa kufukiwa hata kwa halimashauri ya Iringa mpaka kusababisha kutoa roho za watu wengi hivyo? hii ndo Tanzania. Wapumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka.

    ReplyDelete
  6. Kwa kweli nimekerwa sana na huu uzembe wa hii sehemu ya barabara ya Mafinga..eneo la Changarawe na ajali ambayo ingeweza kuepukika. Mashimo makubwa yamekuwepo muda mrefu..sana kweli wakala ka wa barabara (TANROADS-ngazi ya mkoa) wameshindwa kufukuia haya mashimo..jamani kwani ni ghali sana kuweka kifusi..changarawe na kupasawazisha..mimi ni mdau natumia sana barabara hii inauma sana mara nyingi tunasema uzembe wa madereva lakini hili lingeweza kuzuiwa mapema

    ReplyDelete
  7. Mungu atunusuru na hizi ajari mungu wapokee waliopoteza maisha na uwaponye kwa haraka majeruhi wote

    ReplyDelete
  8. Barabara zote za TZ zina nashimo ya ghafla na wakati mwngine wanachimba wakati wana repair na kuacha hivyo kwa siku kadhaa. Mfano Mafinga mpaka Njombe yapo kibao. Mbezi mpaka Chalinze ndiyo usisikie. Roho mkoboni. Lakini cha kushangaza mabasi na malori yanapita huko kwenye mashimo kwa kasi ya ajabu. Polisi na viPaso vyao wanasubiri rushwa kwenye sehemu za 50mph. Aibu hii kwa taifa lenye neema za kila aina.

    ReplyDelete
  9. Tumechoka na maneno ya rambirambi kinachotakiwa ni vitendo. Barabara hiyo ni kuu, ilipaswa ijengwe njia nne kuepusha ajali jamani. Hivi lini Tanzania itasikia kilio cha watu. Au mpaka mtu aliyekufa aje kutoka kuzimuni aseme sasa ajali basi? no no Inatosha kama wadau wanaopinga mauaji ya albino. Inatosha ajali Tanzania tumechoka sana sana.

    ReplyDelete

  10. MAAMUZI SAHIHI YA MADEREVA NDO SULUHISHO LA KUPUNGUZA AJALI, NA KUNUSURU MAISHA YA WATANZANIA. VYANZO VYA AJALI NI VITATU
    1.DEREVA
    2.GARI YENYEWE NA
    3. BARABARA
    LAKINI DEREVA ANAPEWA ASILIMIA 72 ZA KUSABABISHA AJALI.

    ReplyDelete
  11. Hii Serikali yetu basi tu..Pesa za kununua magari ya luxuries, kwenda kutembelea nchi za nje kwa trip ambazo hazina tija zipo nyingi tu..lakini pesa za kufukia mashimo..TANROADS wanasema hakuna...jamani..

    ReplyDelete
  12. Uzembe wa madereva pia unachangia kama huyo Dereva wa basi anapita eneo hilo kila siku na anajua lina mashimo makubwa kwanini hakuchukua tahadhari ya kupunguza mwendo tumechoshwa na ajali hizi za kizembe ambazo zingeweza kuepukika mwenyezi mungu azilaze pema peponi roho za marehemu wote waliopoteza maisha katika ajali hii mbaya.
    Amen

    ReplyDelete
  13. Maneno hayavunji mfumpa. Vinatakiwa vitendo. Ndugu wafrica wenzangu tutumie akili na marifa. Tuachane na ujinga uliotujaa kutatua matatizo yetu. Jambo ili la ajali linakost maisha ya mamilioni ya watanzania. Muda wa kutumia maneno bila vitendo umeshapitwa na wakati. Vyanzo vya matatizo vinajulikana, lakini atujali, tunawaza peana pole tu basi yamekwisha. Ndani ya mwezi tena yale yale. Hivi Lini? Wafrica tutaamka na kuanza kutatua matatizo yetu.

    ReplyDelete
  14. Kipande kutoka Mafinga msitu wa Sao Hill mpk Mbeya barabara ni nyembamba sn mashimo kila mahali. Naulizankwa nini ile barabara mpya iliishia Mafinga mjini ni mipango ya pesa au ndio kila mtu alichukua chake na biashara kuishia hapi

    ReplyDelete
  15. HAYA MALORI YANAYO BEBA MAKONTENA SIO YENYE VIWANGO PIA MADEREVA HAWAZINGATII USALAMA WA RAIA MIMI NINGELIWAPA WAZO MALORI YA MIZIGO YAWEKEWE SIKU TATU KWA WIKI KUSAFIRISHA MIZIGO NA MABASI YA ABIRIA SIKU NNE ILI KUEPUSHA WASIKUTANE NAELEWA SIO WAZO RAHISI LAKINI IKIWA HAMJAPATA UVUMBUZI WA HIZI AJALI NI LAZIMA TURUDI NYUMA KATIKA KUFIKIRI. AJALI NYINGI NI BAINA YA MALORI YA MIZIGO NA MABASI HAWA SIO MARAFIKI HIVI VIFO NA SALAAMU ZA POLE TUTACHOKA TUMEZIDI UZEMBE BARABARA KAMA WEMBE BADO ZINAJENGWA MPYA SASA TUJIPANGE KWA KUTOA SALAAM ZA MSIBA SIKU ZIJAZO.

    MDAU.

    KILIONI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...