BENDI ya muziki wa dansi hapa nchini,Mashujaa Band 'Wana Kibega' leo imemtangaza Aliyekuwa mwanamuziki na mtunzi wa bendi ya Ruvu Stars, Rogert Hegga 'Katapila' kujiunga rasmi katika bendi hiyo.

Mkurugenzi wa bendi ya Mashujaa, Maximilian Luhanga, alisema kuwa Hegga amejiunga rasmi na bendi hiyo na watamtambulisha katika onyesho maalumu litakalofanyika Aprili 5.

Luhanga alisema kwamba kujiunga kwa msanii huyo ni moja ya mikakati ya kuiimarisha Mashujaa ili iweze kuwa bendi bora hapa nchini kama ilivyoweza kung'aa kwenye tamasha la tuzo za muziki la Kilimanjaro.

Alisema kuwa ujio wa msanii huyo utaongeza changamoto kwenye bendi yao ambayo imelenga kufanya vizuri zaidi kwenye safu ya muziki wa dansi hapa nchini.

Hegga alisema kwamba ameamua kujiunga na Mashujaa kwa sababu anataka kufanya kazi katika bendi yenye wasanii wenye uwezo ambao watatumia vipaji vyao kuwafurahisha mashabiki wao.

Aliahidi kutowaangusha mashabiki wa bendi hiyo na mashabiki wake binafsi ambao wanakubali uwezo alionao kwenye sanaa hiyo.

"Nimekuja kuongeza chachu, nimejiunga Mashujaa kwa sababu nafahamu wasanii walioko kwenye bendi hii ni bora, naahidi kuwapa furaha na raha mashabiki wa bendi hii, hawatajutia ujio wangu ndani ya Mashujaa", alisema mwanamuziki huyo ambaye amewahi pia kufanya kazi katika bendi ya Mchinga Sound na African Stars 'Twanga Pepeta'.

Akizungumzia ujio wa mwanamuziki huyo Rais wa bendi hiyo Charles Gabriel 'Chalz Baba Kingunge' alisema kwamba amefurahia ujio wa Hegga ambaye anamuamini na kuufahamu uwezo wake wa kazi.

Alisema kwamba ushirikiano atakaouonyesha yeye na Hegga utasaidia kuinyanyua bendi na kuendelea kutamba hapa nchini.

"Moyo wangu umejaa furaha, nasema karibu sana Mashujaa, najua uwezo wangu na wako utatoa matunda mazuri na yenye kulifunuka jiji", aliongeza Chalz. Moja ya nyimbo ambazo zilipata umaarufu na kutamba zilizotungwa na Hegga ni Fadhila kwa Wazazi ambayo aliiandaa akiwa na Twanga Pepeta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...