Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara imeamuru kufurushwa kwenye jengo hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Center ya Msasani Jijini Dar es Salaam, baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi 26, inayofikia zaidi ya dola za kimarekani milioni 1.6 (zaidi ya Shilingi Bilioni tatu za Kitanzania).
Hatua hii imefikiwa baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria baina ya AMI na mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki wa jengo hilo, Bw. Navtej Singh Bains. Akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zimekutwa zikiwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.
Amri hiyo iliyotolewa wiki iliyopita (tarehe 7 Mei, 2015) na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, imeipa mamlaka kampuni ya mnada ya MEM (MEM Auctioneers and General Brokers Limited) kuifurusha Hospitali ya AMI kutoka kwenye jingo ambapo kampuni hiyo inafanya biashara yake.
Amri hiyo ya kutoka kwenye jengo itaanza mara baada ya kuisha kwa kipindi cha notisi cha siku kumi na nne ambacho kimeshatumiwa na AMI. “Ikiwa mdeni aliyetajwa katika hukumu hapo juu (African Medical Investment Limited –AMI) ameamuriwa kwa amri ya mahakama hii ya tarehe 9 mwezi Septemba, 2014 kuondoka na kukabidhi jengo, na ikiwa bado hajaondoka na kukabidhi jengo lenyewe.
“Unaelekezwa kumwondoa mdaiwa/wadaiwa au mtu yeyote anaefanyakazi chini yake atakayekataa kuondoka kwenye jengo na kumuweka anaemiliki amri hii ya mahakama (Navtej Singh Bains- Mwenyenyumba) kwenye nyumba yake,” inasomeka sehemu ya amri ya mahakama iliyoelekezwa kwa kampuni ya mnada ya MEM (MEM Auctioneers).
Amri hii sasa inapelekea kufungwa kwa Hospitali ya AMI, licha ya rufaa zake za kujaribu kuzuia kufukuzwa, imefikiwa baada ya hospitali hiyo kushindwa kutimiza amri ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania iliyoamuru kulipwa kwa dola za kimarekani milioni 1.514 mahakamani pamoja na kodi ya kila mwezi ya kiasi cha dola za kimarekani 64,000 kila mwezi kufuatia mgogoro wa kodi ya jengo.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Mbarouk, Salum Massati na Katherine Oriyo waliiamuru Hospitali ya AMI kufanya malipo hayo ndani ya mwezi mmoja baada ya hukumu iliyotolewa Februari 12, 2015, agizo ambalo halijatekelezwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...