Mkuu wa kitengo cha Ufundi, Strabag International, Bw. Peter
Simoneit (kulia) akielezea jambo kwa ujumbe wa maafisa waliotembelea kituo
kilichokamilika cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka eneo la Kimara Resort jana
jijini Dar es Salaam. Wanaomsikiliza ni
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala wa Mradi wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi John Shauri (wa pili kulia), Meneja
Usimamizi na Uendeshaji Barabara, DART, Mhandisi Mohamed Kuganda na Mhandisi wa
Mradi wa BRT, Strabag, Philip Patemann.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi John Shauri (wa pili kulia) akielezea jambo wakati wa ziara katika kituo kilichokamilika cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka eneo la Kimara Resort jana jijini Dar es Salaam. Wanaomsikiliza ni Mhandisi wa Mradi wa BRT, Strabag, Philip Patemann (kulia); Meneja Usimamizi na Uendeshaji Barabara, DART, Mhandisi Mohamed Kuganda (kushoto) na Mshauri Mazingira na Sayansi ya Jamii wa mradi huo, TANROADS, Bi. Josephine Mwankusye (wa pili kushoto).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umeeleza
kuridhishwa kwake na matayarisho ya kuanza kutolewa kwa huduma ya mabasi
yaendayo haraka katika jiji la Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu DART,
Mhandisi John Shauri amesema jana jijini hapa kuwa kituo cha kwanza cha mradi
huo kimekamilika kwa mujibu wa makubaliano na mkandarasi anayejenga mradi huo,
kampuni ya Strabag.
Jana timu ya wataalamu na maafisa kutoka DART na Wakala wa taifa
wa barabara (TANROADS) walitembelea kituo hicho kilichokamilika kwa nia ya
kuonyeshwa mambo mbalimbali na kukagua ubora wake kabla ya kukabidhiwa.
“Tulitaka kujiridhisha na kuona ubora wa kazi hii,” alisema Shauri
akizungumzia ziara katika kituo hicho kilicho eneo la Kimara Resort.
Inatarajiwa kuwa baada ya wiki moja kuanzia sasa kituo hicho
kitakabidhiwa TANROADS ambao pia watakikabidhi kwa DART.
Vituo vingine vinne vilivyosalia kati ya Kimara na Ubungo vitakuwa
tayari na kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi wa Saba mwaka huu.
Mhandisi Shauri alisema inatarajiwa kuwa vituo vingi katika njia
hiyo vitakuwa vimekamilika kabla ya huduma ya mabasi hayo katika kipindi cha
mpito haijaanza mwezi Septemba mwaka huu.
Mshauri Mazingira na Sayansi ya Jamii wa mradi huo, TANROADS, Bi.
Josephine Mwankusye alisema wanaridhishwa na matayarisho hayo isipokuwa vitu
vidogovidogo ambavyo vinaweza kurekebishwa haraka.
Alisema kwa sasa ni muhimu wananchi wakaanza kushirikishwa kwa
kupatiwa elimu ili waelewe mradi huo utakavyofanya kazi.
Vituo hivyo vya kisasa pia vimejali mahitaji ya watu wenye ulemavu
kama wasioona na vilema.
Mkuu wa Ufundi, Strabag, Bw. Peter Simoneit alisema vituo vingine
vitafanana na hicho kilichokaguliwa na jopo hilo.
“Tunashukuru kwa kujali wito huu, hii ni muhimu ili wadau wote
tujue kinachofanyika na kurekebisha pale inapotakiwa,” alisema.
Utoaji wa
huduma katika mfumo mzima wa DART umepangwa kuaza katika nusu ya pili ya mwaka
2016.
Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2025 jiji la Dar es Salaam
litakuwa na wakazi milioni 11.5 hivyo uboreshaji miundombinu ni
jambo lisiloepukika.
Inatarajiwa kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta ahueni kubwa
kwa huduma ya usafiri katika jiji hilo.
Kuna baadhi ya watu wanahujumu miundo mbinu ya mradi huu kwa kubomoa vizuizi sehemu za wavuka kwa miguu nadhani ili wapite na magari. naomba mamlaka husika zifanya juu chini kuzuia uhalifu huu.
ReplyDelete