Mkuu wa kitengo cha Ufundi, Strabag International, Bw. Peter Simoneit (kulia) akielezea jambo kwa ujumbe wa maafisa waliotembelea kituo kilichokamilika cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka eneo la Kimara Resort jana jijini Dar es Salaam. Wanaomsikiliza ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi John Shauri (wa pili kulia), Meneja Usimamizi na Uendeshaji Barabara, DART, Mhandisi Mohamed Kuganda na Mhandisi wa Mradi wa BRT, Strabag, Philip Patemann.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi John Shauri (wa pili kulia) akielezea jambo wakati wa ziara katika kituo kilichokamilika cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka eneo la Kimara Resort jana jijini Dar es Salaam. Wanaomsikiliza ni Mhandisi wa Mradi wa BRT, Strabag, Philip Patemann (kulia); Meneja Usimamizi na Uendeshaji Barabara, DART, Mhandisi Mohamed Kuganda (kushoto) na Mshauri Mazingira na Sayansi ya Jamii wa mradi huo, TANROADS, Bi. Josephine Mwankusye (wa pili kushoto).

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umeeleza kuridhishwa kwake na matayarisho ya kuanza kutolewa kwa huduma ya mabasi yaendayo haraka katika jiji la Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu DART, Mhandisi John Shauri amesema jana jijini hapa kuwa kituo cha kwanza cha mradi huo kimekamilika kwa mujibu wa makubaliano na mkandarasi anayejenga mradi huo, kampuni ya Strabag.

Jana timu ya wataalamu na maafisa kutoka DART na Wakala wa taifa wa barabara (TANROADS) walitembelea kituo hicho kilichokamilika kwa nia ya kuonyeshwa mambo mbalimbali na kukagua ubora wake kabla ya kukabidhiwa.

“Tulitaka kujiridhisha na kuona ubora wa kazi hii,” alisema Shauri akizungumzia ziara katika kituo hicho kilicho eneo la Kimara Resort.

Inatarajiwa kuwa baada ya wiki moja kuanzia sasa kituo hicho kitakabidhiwa TANROADS ambao pia watakikabidhi kwa DART.

Vituo vingine vinne vilivyosalia kati ya Kimara na Ubungo vitakuwa tayari na kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi wa Saba mwaka huu.

Mhandisi Shauri alisema inatarajiwa kuwa vituo vingi katika njia hiyo vitakuwa vimekamilika kabla ya huduma ya mabasi hayo katika kipindi cha mpito haijaanza mwezi Septemba mwaka huu.

Mshauri Mazingira na Sayansi ya Jamii wa mradi huo, TANROADS, Bi. Josephine Mwankusye alisema wanaridhishwa na matayarisho hayo isipokuwa vitu vidogovidogo ambavyo vinaweza kurekebishwa haraka.

Alisema kwa sasa ni muhimu wananchi wakaanza kushirikishwa kwa kupatiwa elimu ili waelewe mradi huo utakavyofanya kazi.

Vituo hivyo vya kisasa pia vimejali mahitaji ya watu wenye ulemavu kama wasioona na vilema.

Mkuu wa Ufundi, Strabag, Bw. Peter Simoneit alisema vituo vingine vitafanana na hicho kilichokaguliwa na jopo hilo.

“Tunashukuru kwa kujali wito huu, hii ni muhimu ili wadau wote tujue kinachofanyika na kurekebisha pale inapotakiwa,” alisema.

Utoaji wa huduma katika mfumo mzima wa DART umepangwa kuaza katika nusu ya pili ya mwaka 2016. 

Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2025 jiji la Dar es Salaam litakuwa na wakazi milioni 11.5  hivyo uboreshaji miundombinu ni jambo lisiloepukika.

Inatarajiwa kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta ahueni kubwa kwa huduma ya usafiri katika jiji hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 18, 2015

    Kuna baadhi ya watu wanahujumu miundo mbinu ya mradi huu kwa kubomoa vizuizi sehemu za wavuka kwa miguu nadhani ili wapite na magari. naomba mamlaka husika zifanya juu chini kuzuia uhalifu huu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...