TIMU ya wataalam wa biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na wafanyabiashara wengine wa nchini Tanzania wanatarajiwa kutembelea China baadaye Julai mwaka huu, ikiwa ni katika jitihada za kutafuta fursa za ki biashara ambazo zinaweza kutumika kuleta maendeleo nchini.

Hatua hiyo inakuja miezi michache baada ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete nchini ambapo serikali ya China ilikubali kusaidia Tanzania katika maendeleo na uendeshaji wa Viwanda nchini.

Akizungumza wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 50 ya ziara Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai nchini Tanzania iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dk Abdallah Kigoda alisema kuwa kuna faida kubwa sana katika uchumi wa viwanda na jopo la watalaam hao wanaotarajiwa kutembelea nchi hiyo iliyopo Mashariki ya Mbali, litasaidia kutoa utaalam juu ya fursa za kibiashara ambazo zinaweza kutumiwa na Watanzania.

"Tutahakikisha kuwa mahusiano yetu haya kati ya China na Tanzania yanakuwa na manufaa pande zote mbili. Tumeendelea kukuza uhusiano mkubwa kati ya nchi hizi mbili na China, ambayo kwa sasa ipo kwenye safu ya nchi zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani, imekubali ombi letu kutusaidia katika ukuaji  wa sekta ya viwanda," alisema Dk. Kigoda.

Dk Kigoda alisema uendeshaji mzuri katika sekta ya viwanda utasaidia kuinua uchumi wa watu nchini, ikiwa ukuaji wa biashara mpya na viwanda utajenga maelfu ya ajira mpya na kutoa fursa kwa watu wenye kipato cha chini kujiinua kiuchumi.

On hotuba yake, katika hafla hiyo, Balozi wa China nchini Tanzania Dk Lu Youqing alisema China imekuwa muwekezaji wa kigeni wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania ikiwa imefikisha uwekezaji wa jumla ya dola za Kimarekani  bilioni 4 mwishoni mwa mwaka 2014.

"China pia ni mbia mkubwa wa biashara nchini Tanzania ikiwa na jumla ya biashara zenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 4.3,” Balozi Dk. Youqing alisema.

Alibainisha kuwa Tanzania ni moja ya nchi tatu zilizopo kwenye mpango wa  China-Afrika wa ukuzaji wa Uwezo wa Ushirikiano katika Sekta ya Viwanda, huku Tanzania ni chachu ya kuonyesha mfano wa ushirikiano huo wa kirafiki wa China na Afrika.

"Kama rafiki wa kweli na mbia wa kuaminika wa Tanzania, China itazingatia nguzo za ushirikiano wa China-Afrika za ukweli, matokeo halisi, mshikamano na nia njema ambazo zilianzishwa na Rais Xi Jinping," alibainisha.

Balozi Dk Youqing alisema kuwa kutakuwa na uwekezaji zaidi wa China nchini Tanzania katika siku za  usoni hasa katika nyanja za miundombinu, mwanga/umeme na viwanda vikubwa na pamoja na habari na mawasiliano ya kisasa.

"Uwekezaji wa China nchini utazidi kuwa na manufaa makubwa kwa serikali ya Tanzania na watu wake kwa kulipa kodi na kutengeneza idadi kubwa ya ajira za wazawa," alisema.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dk Abdallah Kigoda (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 50 ya ziara Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai nchini Tanzania zilizofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wa Kwanza kushoto ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Ali Juma Shamhuna, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Janet Mbene (wa pili kulia) na Balozi wa China nchini Tanzania Dk Lu Youqing (kulia).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...