Na Mohamed Saif
Imeelezwa kwamba huduma ya leseni za madini kwa njia ya mtandao
itampunguzia gharama na adha za usafiri mmiliki wa leseni za madini
kwa kumuwezesha kulipia ada za leseni yake pale alipo.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Afisa Madini Mkazi-Njombe, Samwel
Ayubu alipokuwa akifungua mafunzo ya matumizi kuhusu huduma za
leseni kwa njia ya mtandao yaani Online Mining Cadastre Portal
(OMCTP) kwa wachimbaji wa madini mkoani Njombe.
Ayubu alisema kupitia mfumo wa zamani, wakati mwingine mmiliki wa
leseni analazimika kusafiri umbali mrefu na kutumia ghrama kubwa na
vilevile kupata usumbufu usio wa lazima pindi anapohitaji kuhuisha
leseni yake ama pale anapokuwa na maombi ya leseni.
“Kwa kupitia huduma hii ya kielektroniki, mmiliki wa leseni ataweza
kuepuka changamoto mbalimbali alizokuwa akikutana nazo wakati wa
mfumo wa zamani wa uombaji leseni,” alisema Ayubu.
Alitaja manufaa mengine ambayo yanatokana na huduma hiyo kuwa ni
kuongeza uwazi na kasi ya utoaji wa leseni za madini kwakuwa
waombaji wa leseni wataingiza maombi ya leseni wao wenyewe na
hivyo kupunguza tatizo la mlundikano wa maombi kwenye ofisi za
madini.
Aidha, Afisa Madini Mkazi huyo aliwataka wachimbaji waliohudhuria
mafunzo hayo kuwa mabalozi kwa wale ambao hawakupata fursa ya
kuhudhuria mafunzo hayo.
“Kwa mafunzo mtakayoyapata hapa, nawaomba mkawe walimu kwa
wenzenu ambao hawakufanikiwa kuhudhuria semina hii,” alisema.
Alimalizia kwa kuwaasa wachimbaji hao kuhakikisha wanatembelea
Ofisi ya Madini-Njombe kwa lengo la kupatiwa elimu zaidi kuhusu
mfumo huo na vilevile kufika hapo kwa ajili ya kusajiliwa kwenye
huduma hiyo.
Afisa Madini Mkazi- Njombe, Samwel Ayubu (kulia) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo kwa wachimbaji Madini wa Mkoani Njombe kuhusu Huduma za Leseni kwa njia ya Mtandao (OMCTP) mjini Njombe. Wengine ni Maafisa kutoka Kitengo cha Leseni Mjiolojia Mwandamizi, Idd Mganga (kushoto) na Mhandisi Edward Mumba (katikati).
Watumishi wa Wizara ya Nishati wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Ofisi za Madini-Njombe baada ya Mafunzo kwa wachimbaji madini mkoani humo. Watatu kutoka kushoto ni Afisa Madini Mkazi-Njombe, Samwel Ayubu kushoto kwake ni Idd Mganga na kulia kwake ni Mhandisi Edward Mumba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...