Rais Kikwete akikata utepe katika sherehe za uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote eneo la Msijute mkoani Mtwara Jumamosi Oktoba 10, 2015
Rais Kikwete akifunua pazia katika sherehe za uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote eneo la Msijute mkoani Mtwara Jumamosi Oktoba 10, 2015
Rais Kikwete akiweka sahihi katika kitabu cha wageni katika sherehe za uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote eneo la Msijute mkoani Mtwara Jumamosi Oktoba 10, 2015
Wataalamu wakiwa kazini katika kiwanda cha Dangote Mtwara.
Kwa picha zaidi BOFYA HAPA
Tutakidhi
mahitaji yote ya saruji Tanzania – Alhaj Dangote:
·
Tanzania
itaanza kujitegemea kwa saruji karibuni, bila kulazimika kuagiza bidhaa nje,
kufuatia kuzinduliwa kwa kiwanda kikubwa zaidi cha kuzalisha saruji kuliko
kingine chochote katika Afrika Mashariki kilichojengwa katika eneo la Msijute,
Mtwara Vijijini, Mkoa wa Mtwara ikiwa ni uwekezaji wa mabilioni ya fedha wa Kampuni ya
Dangote Group ya Nigeria.
Aidha,
Kampuni hiyo imesema kuwa imechagua kuwekeza Tanzania katika ujenzi wa Kiwanda
hicho na huduma za upakiaji na upakuaji mizigo katika eneo lenye ukubwa wa
hekta 25 katika Kijiji cha Mgao, kilichoko karibu na kiwanda hicho, kwa gharama
ya dola za Marekani milioni 600 kwa sababu ya sera nzuri za Serikali na
mazingira mazuri na rafiki ya kufanyia biashara yaliyojengwa na Serikali ya
Tanzania.
Kampuni
hiyo pia imesema kuwa Kiwanda hicho ndicho kimejengwa kwa kasi zaidi na kwa
muda mfupi zaidi miongoni mwa viwanda vyote vya saruji ambavyo vimejengwa na
Kampuni hiyo katika Bara la Afrika. Ujenzi wa Kiwanda hicho umechukua miezi 30
tu, miaka miwili unusu, tokea ujenzi huo ulipoanza Mei 27, mwaka 2013, kufuatia
mkataba uliotiwa saini kati ya Kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania.
Vile
vile, Kampuni hiyo imetangaza kuwa imeamua kuwekeza zaidi katika Tanzania, na
zamu hii, katika sekta ya kilimo ambako Dangote Group imeanza majadiliano na
Serikali kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa sukari.
Kiwanda
hicho kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete umefanywa Jumamosi, Oktoba 10, 2015 ni Kiwanda cha nne
cha saruji kuzinduliwa na Kampuni ya Dangote Group katika Bara la Afrika katika
miezi minne tu iliyopita na wala siyo cha mwisho kuzinduliwa na Kampuni hiyo
mwaka huu.
Akizungumza
katika sherehe ya uzinduzi, Rais na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj Aliko
Dangote amesema kuwa kiwanda hicho ambacho kitazalisha saruji tani za ujazo
milioni tatu kwa mwaka ni kiwanda kikubwa zaidi cha saruji katika Afrika
Mashariki na kitakidhi mahitaji ya bidhaa hiyo nchini na kubakiza kiasi cha
kutosha kwa ajili ya kuuza nje.
“Tutakapofikia
kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji wetu, Kiwanda hiki kitaiwezesha Tanzania
kujitegemea kwa mahitaji ya saruji na kubakiza kiasi kikubwa tu kwa ajili ya
kuuza katika masoko ya nje,” Alhaj Dangote amemwambia
Rais Kikwete na mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uziduzi huo ambao
walikuwa ni pamoja na wafanyabiashara 172 kutoka Nigeria ambao Alhaji Dangote
aliwaalika katika sherehe hiyo.
Miongoni
mwa wageni hao pia walikuwepo kwenye sherehe hizo ni Mwakilishi wa Serikali ya
Nigeria, Alhaj Mallam Nasir Ahmad el Rufai, Gavana wa Jimbo la Kaduna, Wajumbe
wa Bodi ya Dangote Group na mabinti zake Dangote watatu ambao karibu wote
wamepanda ndege zao binafsi jioni ya leo baada ya shughuli hiyo kurejea kwao
Nigeria.
Kuhusu
uamuzi wa Makampuni ya Dangote kuwekeza katika Tanzania, Alhaji Dangote amesema:
“Tunamshukuru
sana Rais Kikwete. Serikali yake ilitengeneza mazingira rafiki ya kutuwezesha
kuwekeza. Jambo kubwa kwetu sisi wafanyabiashara ni kuwepo kwa mazingira rafiki
ya uwekezaji. Kwa hakika, Tanzania ni moja ya nchi rafiki zaidi kwa ajili ya
kuvutia uwekezaji katika Afrika. Mageuzi ambayo nchi hii imefanya katika sekta
mbali mbali na kukua kwa uhakika kwa uchumi, ni mambo yaliyotuongoza kuichagua
Tanzania kama nchi yetu ya kuwekeza.”
Ameongeza
kuwa Dangote Group imeamua kuwekeza katika Kiwanda hicho katika Tanzania kwa
sababu inataka kuchangia katika ujenzi wa miundombinu ya Tanzania, kupanua
fursa za ajira na kushiriki katika maendeleo ya jumla. Kiwanda hicho
kinatarajia kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na 9,000 zisizokuwa za moja kwa
moja.
“Visheni
yetu pia ni kuwekeza katika uchumi ambazo zina uwezo wa kurudisha gharama za
uwekezaji huo kwa uhakika na kuwa ujenzi wa Kiwanda hicho utazidi kuimarisha
uhusiano kati ya nchi rafiki za Tanzania na Nigeria.”
Kuhusu
mipango yake ya kuiwezesha Afrika kujitegemea kwa uzalishaji wa saruji na
kupunguza idadi ya fedha za kigeni zinazotumiwa na nchi za Afrika kuagiza
saruji kutoka nje, Alhaj Dangote amesema: “Kiwanda
hiki ni moja ya miradi yetu yenye mafanikio ambayo inaendelea kujengwa
katika nchi 18 za Afrika kwa mujibu wa
mkakati wetu wa uwekezaji katika Bara la Afrika.”
Ameongeza:
“Agosti
mwaka huu, tumezindua viwanda viwili vipya katika Zambia na Cameroon. Na mwezi
Juni, mwaka huu, tulifungua kiwanda chetu katika Ethiopia. Kabla ya mwisho wa
mwaka huu, tutazindua viwanda vyetu vingine katika baadhi ya nchi nyingine za
Afrika zikiwemo Senegal na Afrika Kusini. Tunaamini ipasavyo katika uwezo wa kiuchumi wa Afrika na
maendeleo ya baadaye ya Bara la Afrika.”
Ameongeza
Alhaj Dangote: “Vile vile mwezi Agosti mwaka huu mjini Lagos, tuliwekeana saini
makubaliano ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.34 na Kampuni ya Sinoma
International Engineering kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vingine 10 vya saruji
katika nchi nyingine za Afrika na katika nchi ya Nepal iliyoko Bara la Asia.
Uwezo wa jumla wa kuzalisha tani za ujazo milioni 25 kwa mwaka. Miradi hii ikikamilika
katika miaka michache ijayo, Dangote Group itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani
za ujazo milioni 81 kwa mwaka na hivyo kuifanya Kampuni yetu kuwa moja ya
kampuni kubwa zaidi za uzalisha saruji duniani.”
Kampuni
ya saruji ya Dangote Cement Plc ndiyo kampuni kubwa zaidi katika Nigeria na
Afrika Magharibu nzima katika Soko la Hisa la Nigeria (NSE) tokea
ilipoandikishwa kwenye Soko hilo Oktoba mwaka 2010. Kampuni hiyo inasudia
kujisajili kwenye masoko ya hisa ya Johannesburg (Afrika Kusini) na London
(Uingereza).
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
11
Oktoba, 2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...