Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea taarifa za kuwepo Mahujaji
wawili kutoka Tanzania ambao wamelazwa katika mojawapo ya hospitali nchini
Saudi Arabia baada ya kujeruhiwa kutokana na tukio la mkanyagano wa Mahujaji
lililotokea eneo la Mina, Makkah, tarehe 24 Septemba, 2015.
Mahujaji
hao ambao wanaendelea kupata matibabu na hali zao zikiendelea vizuri ni Bi. Hidaya Mchomvu na Bi. Mahjabin Taslim Khan.
Pia
kwa mujibu wa taarifa za Ubalozi Hujaji mwingine anayejulikana kwa jina la Mustafa Ali Mchira amelazwa katika
Hospitali ya Ansari Madina katika chumba cha wagonjwa mahututi. Taarifa
zinaeleza kuwa Bw. Mchira alipata ugonjwa tangu alipowasili Saudi Arabia na
hivyo ugonjwa wake hauhusiani na ajali iliyotokea tarehe 24 Septemba, 2015.
Vilevile, Serikali ya Saudi Arabia
imeanza kutoa taarifa za alama za vidole za Mahujaji waliopata ajali. Hivyo,
Ubalozi unazipitia na kuzihakiki taarifa hizo ambazo zitasaidia kuwabaini
Mahujaji wetu waliokufa katika ajali hiyo.
Kutambulika kwa Mahujaji hao
waliolazwa, kunatokana na jitihada zilizofanywa na Ubalozi kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na Vikundi vya
Mahujaji za kutembelea Hospitali zote zilizopo Makkah, Mina, Arafat, Muzdalifa,
Jeddah na Taif kwa ajili ya kuwatafuta Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia
au kulazwa katika hospitali hizo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
01 Oktoba, 2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...