STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.10.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed
Shein amesisitiza kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho utakuwa huru, haki
na wenye utulivu na kuwahakikishia washirika wa maendeleo likiwemo Shirika la
Misaada la Uingereza (DFID) kuwa Zanzibar itaendea kuwa na amani kwani ndio
msingi wa maendeleo.
Dk. Shein aliyasema hayo katika
mazungumzo kati yake na Kiongozi wa Shirika la Misaada la Uingereza anayefanya
kazi zake nchini Tanzania Mhe. Vel Gnanendran, huko Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza
kiongozi huyo wa Shirika la DFID ambaye alifuatana na Balozi wa Uingereza
nchini Tanzania Mhe. Dianna Melrose kuwa Zanzibar itaendelea kuwa visiwa vya
amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu na hata baada ya
uchaguzi.
Dk.Shein alisema kuwa hatua za maendeleo
zilizofikiwa na Zanzibar sambamba na amani na
utulivu uliopo ndivyo viliyoyapelekea mashirika mbali mbali ya Kimataifa
ulimwenguni kuendelea kuiunga mkono Zanzibar likiwemo Shirika la DFID kwa
kuthamini na kutambua juhudi zake hizo.
Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo
wa Shirika hilo kuwa Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika hilo kwa lengo
la kuleta maendeleo endelevu nchini.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema
kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na vyombo vya ulinzi kwa kuendelea kusimamia amani
na utulivu pamoja na vyama vya siasa wakati wote wa kampeni hivyo ni matarajio
yake kuwa hatua hiyo itaendelezwa hata kwa siku za usoni ikiwemo siku ya kupiga
kura hapo kesho.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza
wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali
mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo pamoja na utafiti wake.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza
haja ya kuweko mpango maalum wa nafasi za masomo nchini Uingereza kwa vijana wa
Zanzibar ikiwa ni pamoja na kupitia Shirika hilo la DFID.
Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa
Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Shirika hilo la DFID.
Nae
Kiongozi huyo wa Shirika la DFID Mhe.
Vel Gnanendran alimueleza Dk. Shein kuwa Shirika hilo limeazimia kuiunga
mkono Zanzibar kwa kutambua juhudi zake katika sekta za maendeleo.
Alisema kuwa juhudi zilizochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo
zinahitaji kupongezwa na kuungwa mkono ili zizidi kuimarika.
Aidha, kiongozi huyo alimpongeza Dk.
Shein kwa kuendelea kusimamia amani, utulivu na mshikamano hapa Zanzibar na
kueleza kuwa hiyo ndio nguzo pekee itakayoendelea kuikuza Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.
Balozi wa Uingereza Mhe. Dianna Melrose
kwa upande wake alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake inatambua na
inathamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Zanzibar na Tanzania
nzima pamoja na Uingereza uliopo ambao aliahidi kuuendeleza.
Balozi Melrose alimueleza Dk. Shein kuwa
wawekezaji wengi wa nchi hiyo wanavutiwa kuja kuekeza Zanzibar kutokana na
kuwepo kwa amani na utulivu sambamba na vivutio kadhaa vya utalii.
Kwa upande wa mashirikiano katika sekta
ya elimu alisema kuwa juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na
zitachukuliwa katika kuhakikisha nafasi za masomo kwa Zanzibar nchini humo zinaongezeka.
Sambamba na hayo, Balozi huyo alimpongeza
Dk. Shein kwa kuisimamia vyema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa
Umoja wa Kitaifa ambayo imepata mafanikio makubwa na kuwa kigezo ndani na nje
ya bara la Afrika.
Pia, Balozi huyo aliisifu na kuipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kutoa fursa
sawa ya kufanya Kampeni zilizokuwa huru na amani kwa vyama vyote hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...