Harakati za kuanza rasmi kwa Benki ya Walimu Tanzania (Mwalimu Commercial Bank - MCB) zinapamba moto baada ya uongozi wa benki hiyo kufikia makubaliano ya huduma ya mfumo wa kiteknolojia wa kibenki kutoka kampuni ya Intrasoft International ya nchini Luxembourg.
Makubaliano hayo yaliyofikiwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki yataiwezesha kampuni hiyo kuanza kufunga mfumo unaojulikana kama ‘Profits’ utakaotumika kwa shughuli mbalimbali za benki hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi wa Tano mwakani.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Bw. Herman Kessy aliiielezea hatua hiyo kama muhimu sana katika azma ya benki hiyo kufungua milango yake kwa wateja wake.
“Huu ni mfumo mzuri na mkubwa utakaoifanya benki yetu kuwa ya kisasa kabisa katika utendaji wake,” aliwaambia waandishi wa habari.
Kampuni hiyo imepata kazi hiyo ya kuandaa na kutekeleza mfumo huo baada ya kuibuka mshindi katika zabuni iliyoshindaniwa na makampuni kadhaa ya ndani na nje ya nchi.
“Wananchi wawe na amani kuwa matayarisho ya benki yao yanakwenda vizuri kabisa,” alisema Mwenyekiti huyo wa benki.
Kampuni hiyo inatarajia kuanza kufunga mfumo huo mwezi wa Pili mwaka 2016 na kumaliza mwezi wa Tisa mwaka huo huo.
Hata hivyo, kufikia mwezi wa Tano tayari benki itakuwa na uwezo wa kuanza kutoa huduma kwa wateja.
Mkurugenzi wa maswala ya Benki na Fedha, Intrasoft International, Bw. Andreas Diamanteas alisema makubaliano hayo ni ya muhimu kwa MCB na kampuni yao.
Alisema ni muhimu kwa benki kwa kuwa inatakiwa kufungua milango yake kwa wateja hivi karibuni na kwa kampuni hiyo kwa sababu mradi huo unafungua milango kwao hapa Tanzania kama wa kwanza kutekeleza.
Alieleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa kuwa kampuni hiyo imetayarisha mpango mkakati wa miaka mitano wa kuingia katika soko la Afrika ya Mashariki na kuwa hivi karibuni walifungua ofisi ndogo mjini Nairobi, Kenya kama moja ya hatua yao hiyo.
“Tunaahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu kwa wakati, ubora unaotakiwa na kwa bajeti tuliyokubaliana,” alisema Mkurugenzi huyo.
Benki ya Walimu Tanzania (MCB) inatarajia kuanza kutoa huduma kwa wateja mwezi Mei mwaka ujao kwa mtaji wa jumla ya Tshs bilioni 31.
Mtaji wa benki ulipatikana kwa kuuza hisa kwa wananchi ambapo hisa moja iliuzwa Tshs 500.
Mwezi uliopita benki hiyo iliorodheswa katika soko la mitaji ya Dar es Salaam (DSE) katika tukio lililoshuhudiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Baada ya kuorodheshwa katika soko hilo, bei ya hisa moja ya benki hiyo ilipanda na kufikia Tshs 700.
Mwenyekiti wa bodi wa Benki ya Walimu Tanzania (MCB), Bw. Herman Kessy (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa maswala ya Benki na Fedha, Intrasoft International, Bw. Andreas Diamanteas (wa pili kushoto) wakitia saini makubaliano ambapo kampuni hiyo itafunga mfumo wa kiteknolojia wa kibenki kwa benki hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. kulia ni mjumbe wa bodi ya MCB, Bw. Ambrose Nshalla na Meneja Masoko Mwandamizi wa kampuni hiyo, Bw. Stavros Batoudakis (kushoto).
Mwenyekiti wa bodi wa Benki ya Walimu Tanzania (MCB), Bw. Herman Kessy (wa pili kulia) akibadilishana nyaraka na Mkurugenzi wa maswala ya Benki na Fedha, Intrasoft International, Bw. Andreas Diamanteas (wa pili kushoto) baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano ambapo kampuni hiyo itafunga mfumo wa kiteknolojia wa kibenki kwa benki hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. kulia ni mjumbe wa bodi ya MCB, Bw. Ambrose Nshalla na Meneja Masoko Mwandamizi wa kampuni hiyo, Bw. Stavros Batoudakis (kushoto).
Mwenyekiti wa bodi wa Benki ya Walimu Tanzania (MCB), Bw. Herman Kessy (kulia) akipongezena na Meneja Masoko Mwandamizi wa kampuni ya Intrasoft International, Bw. Stavros Batoudakis (kushoto) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo itafunga mfumo wa kiteknolojia wa kibenki kwa benki hiyo. Katikati ni Mkurugenzi wa maswala ya Benki na Fedha wa kampuni hiyo, Bw. Andreas Diamanteas.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...