Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa amewataka watendaji wa Shirika la Posta Tanzania na Kampuni ya simu ya (TTCL) kufanya kazi kwa
weledi na mtazamo wa kibiashara ili kuyaongezea mapato mashirika hayo na
hivyo kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanaoyotokea
nchini.
Akizungumza
na wafanyakazi wa TTCL na POSTA mkoani Mwanza Prof. Mbarawa amesema kutokana na
kukua kwa teknolojia ya mawasiliano duniani biashara simu na posta hivi sasa ina
ushindani mkubwa unaohitaji mtazamo mpana wa kibiashara ili kukidhi mahitaji ya
soko.
“Serikali
inajitahidi kuisaidia TTCL na POSTA hivyo wekezeni vizuri kwenye data na
uharaka wa utoaji huduma ili muweze kushindana kwenye soko na kukuza uchumi wa
taasisi hizi muhimu kwa usitawi wa nchi”, amesema Prof Mbarawa.
Prof.
Mbarawa amezitaka menejimenti za POSTA na TTCL kufanya kazi kwa uwazi na
uadilifu ili malengo na mikakati ya taasisi hizo yafahamike kwa wafanyakazi
wote na kuwezesha kujipima kama wanafikia malengo yaliyokusudiwa.
“Hakikisheni
wafanyakazi wote wanaelewa malengo na mikakati ya tasisi zenu ili kazi ya
kuyatekeleza ifanywe kwa umoja na ushirikiano”, amesisitiza Waziri Prof.
Mbarawa.
Aidha,
Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi kuwa wadilifu na
kuepuka kuwa mawakala wa mashirika mengine na hivyo kuihujumu Serikali.
“kuna
watu ndani ya TTCL na POSTA ambao ni wazembe, wavivu na wanao hujumu Serikali
tutawaondoa mara moja, Ni vema kubaki na wafanyakazi wachache waadilifu kuliko
wengi wasiotimiza maelngo yaliyokusudiwa”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa
Naye
Meneja wa TTCL mkoa wa Mwanza Bw. Johnbosco Kalista amemweleza Waziri Mbarawa
kuwa wigo wa mtandao kutofikia walaji wengi, wateja kutolipa madeni kwa wakati
na ulinzi na usalama wa miundombinu ya mawasiliano ni miongoni mwa changamoto
zinazoikabili shirika hilo mkoani Mwanza.
Kwa
upande wake Meneja wa POSTA mkoa wa Mwanza, Bw. Julius Chifungo amebainisha
kuwa uchakavu wa barabara, maslahi yasiyokidhi ya wafanyakazi na uchakavu wa
majengo ni miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri utendaji kazi wa shirika hilo
mkoani Mwanza.
Takribani
masanduku elfu tisa yanasimamiwa na Shirika la Posta mkoani Mwanza katika ofisi
zake kumi na moja na asilimia 96.8 hukodishwa na kuingizia shirika hilo faida,
Wakati takriban wateja 45,041 wanahudumiwa na TTCL katika Mkoa wa Mwanza.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia) akipata
maelezo ya namna mitambo ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) inavyofanya kazi
kutoka kwa Mtaalamu wa Mitambo (Technician) Edward Lukungu (wa pili kushoto) wakati wa ziara ya
kutembelea Shirika hilo jijini Mwanza.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) akipata
taarifa ya utendaji wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kutoka kwa Meneja Mkoa
wa Mwanza Bw. Julius Chifungo (katikati) wakati alipotembelea ofisi za Shirika
hilo jijini Mwanza. Kulia ni Meneja wa TTCL Mkoa wa Mwanza, Johnbosco Kalista.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiangalia moja ya mitambo
ya mkongo wa taifa iliyopo Mkoani Mwanza.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa
menejimenti ya TTCL na POSTA alipowatembelea jijini Mwanza.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa
wafanyakazi wa TTCL na POSTA mara baada ya kutembelea na kuona utendaji kazi
wao, jijini Mwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...