Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
BAADA ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kuvurunda kwenye mchezo wao wa mwishoni mwa wiki dhidi ya Misri kwa kukubali kichapo cha goli 2-0, wadau wa mpira wa miguu wamemshushia zigo la lawama kocha mkuu wa timu hiyo kwa kuonyesha udhaifu katika kuteua kikosi cha timu hiyo na kuishilia kuwalaumu wachezaji kwa kiwango kibovu wanachokionesha uwanjani.
Moja ya wadau wa mpira, Musa Adinani amesema kuwa Mkwasa hakutaka kuangalia na mechi inayotukabili ambayo ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kwetu na hata ukiangali kikosi alichokipanga kilikuwa na mapungufu makubwa sana hasa safu ya kiungo kwa kuchezesha viungo wenye aina moja ya mpira na kushindwa kutengeneza nafasi kwa washambuliaji.
"Hatuelewi kwanini aliwaanzisha wachezaji Himid Mao na Mwinyi Kazimoto ambao wote wana aina moja ya mpira, hata ukiangalia washambuliaji wameshindwa kupata mipira mingi ya kulishwa kutoka safu ya kiungo na muda mwingi sana Mbwana Samatta alikuwa anazunguka na mpira akitafuta kwa kupiga,"amesema Adinani.
Misri waliweza kumiliki pale kati na hata ukiangali kuanza kwa washambuliaji wawili ambao wote ni wapiganaji lilikuwa ni kosa sana. Samatta na Elius Maguli ni wachezaji wa aina moja huwezi kuwaanzisha katika mechi yenye umuhimu kama hiyo tena ukiweka viungo wawili tu kati.
Wadau wengine wameonekana sana kuchukizwa na kitendo cha Mashabiki wa Timu za Simba na Yanga kuwazomea wachezaji wa timu pinzani pale anapofanya makosa na hilo limeonekana ni kama hali isiyo nzuri hasa ukizingatia ni timu ya Taifa ndiyo inacheza na ni muhimu kuungana ili kuwapa hari na hamasa wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...