![]() |
| Iddi Cheche (kushoto) sasa ndiye atakaimu ukocha wa Azam wakati timu ikitafuta kocha mwingine. Kwa hisani ya Bin Zubeiry |
AZAM FC imetangaza rasmi kuachana na makocha wake kutoka Hispania chini ya Zeben Hernandez Rodriguez leo na kwamba kocha wa vijana, Iddi Nassor 'Cheche' ataiongoza timu kwa muda akisaidiwa na Iddi Abubakar.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amesema leo kwamba kwamba wamefikia makubaliano na makocha hao kutoka Hispania kuvunja mikataba.
Jopo hilo la makocha linaundwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake, Yeray Romero, Kocha wa Makipa Jose Garcia, Kocha wa Viungo, Pablo Borges na Mtaalamu wa tiba za Viungo, Sergio Perez.
Kawemba amesema kwamba uamuzi huo umefikiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo jana, na umetokana na mwenendo mbaya wa Azam FC kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo imefikia raundi ya pili hivi sasa.
"Azam FC inawatakia kila la kheri na mafanikio mema makocha hao huko waendako na inawashukuru kwa mchango wao wote walioutoa kwenye timu kwa kipindi chote walichokaa, ikiwemo kuwapa taji la kwanza la Ngao ya Jamii mwaka huu kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2,"amesema Kawemba.
Amesema wakati uongozi ukiwa katika mchakato wa kusaka kocha mpya, kikosi hicho kitakuwa chini ya makocha wa timu ya vijana ya timu hiyo, Idd Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, ambao walianza kazi jana jioni kukiandaa kikosi kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Tanzania Prisons.
"Azam FC inapenda kuwaambia mashabiki wake kuwa wawe watulivu katika kipindi hiki kwani uongozi umefanya uamuzi sahihi kwa ajili ya kuinyanyua timu juu ili hatimaye ushiriki wetu wa michuano mbalimbali uweze kuwa ni wa kiwango cha juu tofauti na hali ilivyokuwa sasa," amesema Kawemba.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...