Serikali imesema ujenzi wa daraja la mto Mara lenye urefu wa mita 94 lililopo katika barabara ya Tarime-Mugumu-Nata litakamilika mwanzoni mwa mwezi wa nne mwaka huu.

Amezungumza hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo ambalo linaunganisha wilaya ya Tarime na Serengeti na kuwatoa hofu wananchi wa wilaya hizo kuwa endapo daraja hilo likikamilika litaondosha adha waliyokuwa wanaipata ya kuvuka hasa vipindi vya masika.

“Niwahakikishieni daraja hili litamalizika mapema mwezi wa nne pia nimemuagiza mkandarasi huyu ambaye ni mzawa kuhakikisha anazingatia viwango na wakati” amesema Prof. Mbarawa.Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo itakuwa dira kwa wakandarasi wazawa kupewa miradi mikubwa kwani pamekuwa na changamoto kwenye utekelezaji wa miradi hususani kwa wakandarasi wazawa.

Kwa upande wake Mkandarasi wa kampuni ya M/S Gemen Engineering & Mayanga, Mhandisi Andrew Nyamtori, amesema kuwa mradi umekamilika kwa sehemu kubwa hivyo kazi zilizobakia ni kutandika vyuma juu ya daraja ili likamilike na kuanza kutumika na hivyo kuiomba Serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kwa kuwapa miradi mingine mikubwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Gemen Engineering & Mayanga, Mhandisi Andrew Nyamtori (kulia), alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mto Mara, linalounganisha Wilaya ya Tarime na Serengeti, Mkoani Mara.
Muonekano wa Daraja la Mto Mara lenye urefu wa Mita 94 na kuunganisha Wilaya za Tarime na Serengeti likiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake. Daraja hilo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Bi. Bertha Bankwa, wakati akikagua kiwanja hicho. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (wa pili kulia) mara baada ya kukagua ujenzi wa Daraja la Mto Mara, linalounganisha Wilaya ya Tarime na Serengeti, Mkoani Mara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...