Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MAPENDEKEZO ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2019,2020 imeonesha namna ambavyo Serikali imedhamiria kuboresha sekta ya mifugo nchini.
Akizungumza Bungeni Mjini Dodoma wakati anawasilisha makadirio ya bejeti ya Serikali,Waziri wa Fedha Dk.Philip Mpango pamoja na mambo mengine amesma Serikali imependekeza kufuta tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo.
Amesema wamefuta tozo ya sh. 5000 ya vibali vya vyombo vya kusafirisha maziwa chini ya lita 51, pia kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa vituo vya kukusanyia maziwa lita 201 kwa siku.Pia imefuta tozo ya Sh.5000 ya usajili wa wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 kwa siku pamoja na kufuta tozo ya Sh.500,000 ya usajili wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa.
Waziri Mpango amefafanua pia wamefuta tozo ya sh. 15,000 ya usajili wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama na kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa wafgaji wadogo wa mifugo ya nyama.
"Tumefuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa wafugaji wa kati wa mifugo ya nyama, kufuta tozo ya Sh. 75,000 ya usajili wafugaji wakubwa wa mifugo ya nyama na kufuta tozo ya Sh. 20,000 ya usajili wasimamiziwa minada ya awali,"amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imependekeza kufuta tozo ya Sh. 30,000 ya usajili wasimamizi wa minada ya upili na mipakani pamoja na kufuta tozo ya sh. 50,000 ya usajili wa minada ya upili na mpakani.
Pia kufuta tozo ya Sh. 30,000 ya usajili wafanyabiashara wa minada ya awali na kufuta tozo ya Sh. 60,000 ya usajili wafanyabiashara wa minada ya upili na mipakani.Aidha, Waziri Mpango amesema Serikali imefuta tozo ya Sh. 100,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa nyama na bidhaa zake za nje ya nchi pamoja na kufuta tozo ya Sh. 1000 ya kibali cha kusafirisha kuku nchini ya vifaranga 100 kwa siku.
Wakati huo huo amesema amependekeza kufuta tozo ya Sh. 200 ya kibali cha kusafirisha kuku mkubwa nchini na kwamba hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa sh. bilioni 16.6.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...