Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KAMPUNI ya TOL Gases Limited imetangaza kutoa gawio la Sh.bilioni moja kwa wanahisa wake ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo kwa kipindi ha miaka 20 tangu walipoingia kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam(DSE).

Hayo yamesemwa leo Juni 28,2019 na Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases Limited Daniel Warungu wakati wa Mkutano wa mwaka 2018 wa uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa kutokana na mageuzi makubwa ya kiuendaji ambayo yamefanyika katika menejimenti hivi sasa wamekuwa wakijiendesha kwa faida na kwa mwaka wa fedha wa 2018 wamepata faida ambayo imewezesha kuanza kutoa gawio ikiwa ndio mara ya kwanza kufanya hivyo tangu mwaka 1998 walipoingia kwenye Soko la Hisa.

"Kwa kweli hivi sasa tunajivunia kwani tunajiendesha kwa faida, na ndio maana leo tumekutana na wanahisa kutangaza kugawa gawio ambapo hisa moja ni Sh.17.37.Jumla ya gawio ambalo limetengwa kwa wanahisa ni Sh.bilioni moja.

"Tunawashukuru wanahisa wote, menejimenti na bodi ya wakurugenzi kwa namna ambavyo wameshirikiana kwa pamoja kuhakikisha kampuni yetu tunafanya vizuri kwenye kuuza bidhaa zetu katika soko,"amesema Warungu.

Pia amesema katika kuhakikisha wanapata faida walimua kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na matokeo yake leo wanajipongeza kwa mafanikio yanayokwenda sambamba na utoaji wa hisa kwa wanahisa wote.

Kuhusu mikakati yao amesema ni pamoja na kununua mitambo miwili na kuongeza magari kwa ajili ya kusafirisha bidhaa katika nchi za SADC pamoja na Afrika Mashariki na kufafanua katika uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhamasisha ujenzi wa viwanda umeisaidia kampuni yao kuongeza idadi ya wateja.

"Tunalo soko la uhakika ndani ya nchi ya Tanzania, lakini pia tunafanya biashara zaidi ya kuuza bidhaa zetu kwenye nchi mbalimbali za Afrika.Hivyo katika kufurahia mafanikio yetu , tunakwenda pamoja na kuweka mikakati ya kujiimarisha zaidi,"amesema Warungu.

Akizungumzia mkutano wa wanahisa amesema , umefanyika kwa mafanikio makubwa na wanahisa wameridhishwa na juhudi ambazo kampuni hiyo inafanya huku wakitoa ushauri na maoni ya namna bora ya kuendelea kutengeza faida kwa miaka mingi ijayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni hiyo Michael Shirima amewahakikishia wanahisa wote kuwa wamejiridhisha na utendaji kazi wa menejimenti ya sasa ambayo inafanya kazi vizuri na wameanza kuona matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

"Tunawapongeza menejimenti yetu, huko nyuma kwa miaka mingi hatukuwa tunafanya vizuri na ndio maana hatujapata gawio lakini safari hii tunapata gawio.Hata hivyo menejimenti tuliiuliza zaidi ya mara moja hili la gawio litakuwa kila mwaka au itakuaje.Wametujibu kuanzia sasa itakuwa ni kila mwaka kwani wanakwenda vizuri"amesema Shirima.

Shirima ametumia nafasi hiyo kueleza kampuni yao inafurahishwa na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyipo nchini na hivyo wataendelea kufanya kazi kadri ya uwezo wao kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda.
 Mwenyekiti wa  Bodi ya Kampuni ya TOL Gases Limited Michael Shirima akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka 2018 wa wanahisa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 28,2019
 Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases Limited Daniel Warungu(wa nne kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano wa mwaka 2018 wa wanahisa uliofanyika leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases Limited Daniel Warungu akifafanua jambo baada ya kumalizika kwa mkutano wa mwaka 2018 wa wanahisa wa kampuni hiyo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam
 Wanahisa wa TOL Gases Limited  wakiendelea kuchambua taarifa ya mkutano mkuu wa mwaka 2018 wa kampuni hiyo uliofanyika leo Dar es Salaam
 Baadhi ya wanahisa wa kampuni ya TOL Gases  Limited wakipitia taarifa ya mkutano wa mwaka 2018 wa wanahisa uliofanyika leo Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...