Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WAZIRI wa Fedha Dk. Philip Mpango wakati anawasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 pamoja na mambo mengine amezungumzia kutoza ushuru kwenye nywele bandia(Mawigi).
Dk.Mpango akizungumza Bungeni Mjini Dodoma amesema Serikali itatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwenye nywele zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema lengo likiwa kuongeza mapato ya serikali."Nywele bandia ambazo zinatengenezwa nje ya nchini ushuru utakaotozwa ni asilimia 25,"amesema Waziri Mpango wakati anawasilisha bajeti hiyo.
Hata hivyo wakati anazungumzia kwenye nywele hizo bandia, baadhi ya wabunge walisikika wakisema kuwa Serikali pia iongeze ushuru wa kodi kwa kucha bandia ambazo nazo zimekuwa zikiingizwa nchini kwa wingi.
Mbali na ushuru kwenye nywele bandia,Waziri Mpango amesema Serikali imesamehe ushuru wa bidhaa kwenye vilainishi vya ndege vinavyoingizwa nchini na Shirika la Ndege la Tanzania au mashirika ya kimataifa ya huduma za anga.
Amesema lengo la hatua hiyo ni kuiwezesha nchi kusaini mikataba ya kimataifa ambayo ilishindikana kusainiwa awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo.
Amezungumzia pia kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye bidhaa za mabomba na vifaa vya plastiki vinavyotumika kwenye ujenzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo.
Waziri Mpango amesema hatua hiyo itahusisha bidhaa za mabomba ya plasitiki zinazotambuliwa na kwamba lengo la kuanzisha ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa hizo ni kulinda viwanda na kuongeza fursa za kazi, ajira na mapato ya Serikali.
Ameongeza kwa ushuru wa bidhaa kwenye bishaa zisizo za petroli kwa ujumla wake azinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh.bilioni 2. 9.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...