*Yaondoa msamaha wa kodi kwenye taulo za kike kisa...

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BAJETI ya Serikali ambayo imewasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk.Philip Mpango imeonesha namna ambavyo imefuta msururu wa kodi ambazo nyingine zilikuwa kero ka Watanzania.

Mbali ya kufuta utitiri huo wa kodi,Waziri Mpango amesema ni marufuku kwa watumishi wa TRA kufunga biashara kwa madai ya kudai kodi.

Akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni Mjini Dodoma,Waziri Mpango amesisitiza kwa watumishi wa TRA kuwa hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe kodi au malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha kamishina Mkuu wa TRA.

Amefafanua alipendekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya serikali.

Dk.Mpango amesema marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wakutabirika.

Amesema kwamba marekebisho hayo yanalenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo,viwanda,kukuza ajira, na kuongeza mapato ya serikali.

Wakati huo huo ameeleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na mamlaka za udhibiti kwa lengo la kupunguza na kuondoa muingiliano katika kutoza tozo hizo.

"Marekebisho yanayopendekezwa yanahusu Sheria ya Kodi ya Ongezeko la thamani, Sura 148, Sheria ya kodi ya mapato, Sura 332 na Sheria ya ushuru wa bidhaa, Sura 147.

"Pia yatahusu Sheria ya usimamizi wa kodi, Sura 438, Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168, Sheria ya forodha ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004, Sheria ya bajeti Sura 439, na marekebisho madogo katika baadhi ya sheria za kodi na sheria nyingine mbalimbali,"amesema.

Ameweka wazi kuanza utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara kwa kurekebisha ada na tozo mbalimbali, kuchukua hatua za kisera na kiutawala katika kuboresha ukusanyaji wa mapato.

Kuhusu sheria ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) Waziri huyo wa fedha amesema marekebisho yanayopendekezwa yanahusu sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya VAT, Sura ya 148, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147.Pia amependekeza kufanya marekebisho kwenye sheria hiyo ambayo inasamehe VAT kwenye makasha yenye majokofu yanayotumika kwenye kilimo cha Kisasa cha mboga mboga kwa wakulima wanaoingiza makasha hayo kutoka nje ya nchi.

"Lengo la hatua hiyo ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika uzalishaji na kuhamasisha kilimo cha kisasa cha mboga mboga nchini.Pia kufanyika marekebisho kwenye kifungu cha 68(3)(d) ili kisihusishe uuzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje ya nchi."Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wauzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje ya nchi kuendelea kufanya biashara hiyo kwa kadri ya kibali kitakavyotolewa na serikali,,"amesema Wazriri Mpaango.

Amesema msamaha huo unatarajiwa kutoa unafuu kwenye gharama za kukausha nafaka kwa ajili ya kuzihifadhi na kwamba hatua hiyo itachochea ukuaji wa kilimo cha mazao ya nafaka.

Amesema kupunguza kiwango cha VAT kutoka asilimia 18 hadi sifuri kwenye huduma ya umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ili kuwapunguzia gharama za maisha wananchi wa Tanzania Zanzibar.

Amesema kuwa "Serikali iliridhia na kuelekeza kuwa umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania visiwani utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri."

Kwa upande mwingine ,Waziri Mpango amesema Serikali imeamua kufuta msamaha wa VAT uliokuwa umetolewa kwenye taulo za kike kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha wafanyabiashara.
Amefafanua kuwa Serikali ilipoweka msamaha kwenye taulo za kike ilitarajia wazalishaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi.

Hata hivyo amesema hatua hiyo ya VAT zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh.Milioni 1,646.7.

Kuhusu sheria ya kodi ya mapato,Waziri Mpango amesema katika sheria hiyo ya mapato inapendekezwa kufanyika kwa marekebisho ya kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa makampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzlaisha taulo za kike.

Amesema kuwa Serikali itaingia mkataba wa makubaliano na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande na lengo la hatua hiyo ni kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu, kuongeza ajira na mapato.

"Pia hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wake ndani ya nchi,"amesema Waziri Mpango wakati anawasilisha bajeti hiyo yenye kurasa 74.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...