*Yashauriwa fursa kutolewa kwa wanawake kutokana na utendaji wao wa kazi.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

NCHI za jumuiya ya maendeleo za Kusini mwa Afrika (SADC) wameshauriwa kuitumia wiki ya viwanda katika kutafuta masoko ya uhakika pamoja na kufanya tathimini ya walikotoka na wanapoelekea hasa katika kuiangalia mazingira wezeshi ya biashara, miundombinu na nishati hasa umeme kupitia vikao mbalimbali vitakavyofanyika katika wiki ya viwanda iliyoanza leo kwa kuzinduliwa rasmi na Rais Dkt.John Joseph Magufuli.

Akizungumza katika uzinduzi huo katibu mtendaji  wa jumuiya ya maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika Dkt. Stergomena Tax amesema kuwa jumuiya hiyo inajukumu la kuongeza kasi ya ukuaji wa viwanda kwa kuweka mazingira wezeshi hasa kwa kuhakikisha kuna uhakika wa nishati hasa umeme pamoja na miundombinu.
"Hatuwezi kushindana katika soko la biashara la kimataifa kama hatuna umeme wa uhakika na wanajumuiya ya SADC tunampongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za dhati za kuhakikisha suala la nishati linakuwa imara zaidi kwa kutafuta vyanzo mbalimbali vya umeme" ameeleza Dkt.Tax.

Aidha Dkt. Tax amemuoamba Rais Magufuli ziada ya umeme utakaobaki katika mradi wa umeme wa bonde la mto Rufiji ukasaidie nchi nyingine za SADC ambazo zina uhaba wa nishati ya umeme na kushauri nchi wanachama kufanya kazi kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuweza kukuza uchumi kwa nchi wanachama pamoja na kuimarisha uwekezaji na uhuru wa kusafiri kwa wafanyabiashara ndani ya nchi wanachama wa SADC.

Vilevile Dkt. Tax amewashauri watanzania kuitumia vyema wiki ya viwanda kwa kushirikiana na wizara ya viwanda na biashara ili waweze kutengeneza masoko ya uhakika pamoja na kubadilishana ujuzi kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nchi 16 washirika zenye zaidi ya watu milioni 300.

Kwa upande wake Waziri mwenye dhamana ya Viwanda na biashara Innocent Bashungwa amesema kuwa maonesho ya nne ya wiki ya viwanda yanaendelea vyema na wadau wengi wa sekta za umma na zile binafsi wamejitokeza kwa wingi hali iliyochangiwa na elimu kuhusiana na fursa za ugeni wa SADC.

" Zaidi ya washiriki 3000 wamejitokeza huku idadi kubwa ikiwa ni watanzania na Kati yao waoneshaji wa bidhaa wazawa ni 1401 na 172 ni waoneshaji kutoka nje hii ni ishara njema na mapinduzi ya maendeleo hasa katika umoja wetu na siku ya ijumaa wageni wetu watatembelea viwanda kadhaa ndani ya nchi na visiwani Zanzibar" ameeleza Bashungwa.

Aidha Waziri Bashungwa amewataka jumuiya ya taasisi ya sekta binafsi nchini na shirikisho la wenye viwanda (CTI)  kuchangamkia fursa hiyo kwa kuhakikisha mkutano huo unaacha alama nchini hasa kwa kuwepo kwa masoko pamoja na kubadilishana ujuzi kutoka kwa wafanyabiashara washirika kutoa nchi za SADC.

Awali akitoa salamu kutoka serikali ya Namibia mwenyekiti wa  baraza la biashara la SADC Charity Mwiya amesema kuwa jumuiya hiyo haiwezi kuongelea maendeleo Kama kundi jingine (wanawake) litatengwa na kuwashauri wanawake kutumia fursa kwa kuwa wanaaminika zaidi katika utekelezaji.

Pia Charity ameipongeza serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Joseph Magufuli  kwa kushiriki vyema katika shughuli za kimaendeleo na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 5 zinazokuwa kiuchumi barani Afrika. Na amewashauri wanachama wa umoja huo kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza kasi ya kuyafikia maendeleo.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi huku wafanyabiashara wengi wakijitokeza kuonesha bidhaa zao katika viwanja vya ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere, Karimjee, na Gymkhana jijini humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...