Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

OFISA Upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe, Emmanuel Njegele  leo Oktoba 16,2019 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa na maofisa wenzake watatu  katika kesi ya kushawishi rushwa ya Sh milioni 200 iliyoko mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.  Mbali na Njegele, washtakiwa aliounganishwa nao ni, Maofisa Upelelezi, Shaban Shillah, Joyce Kitta na Ulimwengu Rashidi.  

Mapema, wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Nickson Shao alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa upelelezi bado haujakamilika ila pia ameomba  kumuunganisha mshitakiwa Njegele katika kesi hiyo. 

Akisoma hati ya mashitaka Shao amedai Desemba 17, 2018 maeneo ya Rainbow Social Club, Kinondoni, wakiwa maofisa wa uchunguzi, waliomba rushwa ya Sh milioni 200 kutoka kwa Diana Naivasha kama kishawishi cha kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali. 

Alidai washitakiwa hao wakiwa maeneo ya Kituo cha Polisi Kawe, wakiwa waajiriwa wa Jeshi la Polisi, walipokea rushwa ya Sh milioni sita kutoka kwa Naivasha.  Alidai Desemba 18, 2018 washitakiwa hao walipokea rushwa ya sh. milioni sita kutoka kwa Naivasha na Desemba 19, 2018 washitakiwa hao wakiwa Kituo cha Polisi Kawe, walipokea Sh milioni mbili kutoka kwa Naivasha.

Pia inadaiwa Desemba 23, 2018 washitakiwa walipokea rushwa ya Sh milioni mbili na Januari 3, mwaka huu maeneo ya Tamarind Restaurant wilayani Kinondoni, walipokea rushwa ya Sh milioni mbili.

Aprili 13, mwaka huu maeneo ya Tripple 7 Bar and Restaurant, wakiwa maofisa wa jeshi la polisi Idara ya Upelelezi walipokea rushwa ya Sh milioni moja Naivasha kama kishawishi cha kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.

Katika mashitaka ya nane, inadaiwa kati ya Desemba 17,2018 na Aprili 13, mwaka huu maeneo yasiyojulikana jijini Dar es Salaam, Kitta alighushi maelezo ya Naivasha ya Desemba 17, 2018 ili kuonesha kuwa maelezo hayo ni ya kweli na yalisainiwa na Naivasha wakati si kweli.

Pia inadaiwa mshitakiwa Shillah na Njegele, Aprili 13, mwaka huu wakiwa maeneo ya Triple 7 walikiuka amri halali ya kukamatwa na Mpelelezi wa Takukuru, Colman Lubis.

Washitakiwa wote walikana mashitaka na upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi bado unaendelea.

Hakimu Rwizile aliwataka washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya taifa ambapo kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni 10.

Pia aliwataka kuwasilisha mahakamani hapo hati za kusafiria na mmoja kati ya wadhamini hao ametakiwa kuwa na hati au uthibitisho wa mali isiyohamishika.

Washitakiwa wote wametimiza masharti ya dhamana na kesi imeahirishwa hadi Novemba 11, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...