Uzinduzi wa mradi huo wa maji umefanyika leo, Oktoba 25, 2019 kwenye ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo,Mboneko amelipongeza Shirika la Lifewater International, kwa kuanzisha mradi wa maji mkoani Shinyanga ambao utaanza kutekelezwa kwenye kata hizo tatu za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambazo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama. Amesema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli inasisitiza sana upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi ili wananchi waweze kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama, pamoja na kuugua magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji ambayo siyo salama kiafya, na kubainisha mradi huo upo sehemu sahihi.
“Tunalishukuru sana Shirika hili la Lifewater International kwa kutuletea mradi huu wa maji mkoani Shinyanga, na kuanza kutekelezwa kwenye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo tunaomba mradi huu pia ufike na kwenye maeneo mengine ambayo yana shida ya maji safi na salama ikiwemo wilaya ya Kishapu,”amesema Mboneko.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Lifewater International Tanzania Devocatus Kamara, amesema mradi huo kwa kuanza utatekelezwa kwenye kata hizo tatu za halmshauri ya wilaya ya Shinyanga, ambazo ni Mwantini, Mwamala na Mwalukwa , na baada ya hapo utapanuka kwenye maeneo yote ya mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine, ambayo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama na usafi wa mazingira.
Amesema mradi huo utadumu kwa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 na utagharimu kiasi cha Shilingi za kitanzania 4,286,070,528, ambao utajenga visima vipya virefu vya maji safi na salama na kuvikarabati vibovu, kujenga na kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora, kuboresha usafi wa mazingira, na utahamasisha na kuhimiza ushiriki wa jamii kikamilifu ili kuhakikisha uendelevu wa mradi.
Kwa upande wake,Meneja wa Shirika Lifewater International mkoa wa Shinyanga Benety Malima, amesema kuwa katika maeneo ambapo maji ya ziwa Victoria yamekwishafika, watafanya utaratibu wa kuendelea kuyasambaza katika maeneo yanayokusudiwa. Pia amesema maeneo ambayo yatapitiwa na mradi huo wa maji, ni sehemu za shule, zahanati, pamoja na kwenye makazi ya watu, ambapo mradi huo umelenga kufikia watu 100,000.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...