MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa wiki mbili kwa viongozi tisa wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kujiandaa ili waweze kuanza kujitetea kwa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 4,5 na 8 mwaka huu.
Pia Mahakama imeagiza kielelezo cha video kilichotolewa na upande wa mashtaka, kinachoonesha maandamano ya viongozi hao kilichoombwa na upande wa utetezi, kisitumike nje ya mahakama bali kitumike kwa kutumia miundombinu ya mahakama chini ya usimamizi wa uongozi wa mahakama.
Akisoma uamuzi hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema ni kweli washitakiwa hao wanahitaji muda wa kufanya maandalizi na kwamba kipindi muafaka cha kujiandaa ni siku 14 na ameongeza kuwa, idadi ya mashahidi waliotajwa ni kubwa na wasipokuwa waangalifu kesi haitaisha hivyo, ni lazima kuwa na ratiba maalum ya kusikiliza kesi hiyo.
"Kielelezo mlichokiomba hakitaenda popote isipokuwa kitatumika kwa kutumia miundombinu ya mahakama ili iwe huru katika kuandika hukumu hivyo wakati upande wa utetezi wakitumia kielelezo hicho kuwaandaa washitakiwa, itakuwa chini ya usimamizi wa utawala ili kuhakikisha usalama wa kielelezo na miundombinu inazingatiwa, amesema Simba
Aidha, upande wa utetezi wametakiwa kutoa taarifa siku tatu kabla juu ya matumizi ya kielelezo hicho katika ukumbi wa mahakama na kusema kesi hiyo itaanza kusikilizwa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 4,5 na 8 na baadaye itapangiwa ratiba maalum.
Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.
Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...