Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwafahamisha waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 kuwa imetoa orodha ya Awamu ya Pili yenye jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza 11,378 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 35.06 bilioni.
Taarifa iliyotolewa leo (Jumamosi, Oktoba 26, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru imesema idadi hii ya awamu ya pili inafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo kufika 42,053 na wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 148.56 bilioni.
Katika orodha ya awamu ya kwanza iliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi wa mwaka wa kwanza 30,675 walipata mikopo yenye thamani ya TZS 113.5 bilioni.
Badru amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga TZS 450 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 128,285. Kati yao, wanafunzi zaidi ya 45,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wanafunzi wenye mikopo wanaoendelea na masomo. Mwaka 2018/2019, TZS 427.5 bilioni zilitengwa na kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 123,285 wakiwemo wanafunzi 41,285 wa mwaka wa kwanza.
“Tumeboresha sana mifumo yetu, na sasa mwanafunzi anaweza kufungua akaunti yake aliyoombea mkopo maarufu kama SIPA - Student’s Individual Permanent Account - na kupata taarifa zake zikiwemo za kiwango cha mkopo alichopata,” amesema Badru.
Pamoja na SIPA, Badru amesema majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya pili yanapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo (https://olas.heslb.go.tz) na tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...