Na Woinde Shizza,Michuzi Tv Arusha

WANANCHI wa kata za Moshono jijini Arusha na Mlangarini wilayani Arumeru wamemuomba Rais, Dkt John Magufuli kuingilia kati na kuumaliza mgogoro wa ardhi baina yao na Jeshi la Wananchi, (JWTZ) kikosi cha 977 kwenye eneo la mita 100 kuzunguka mlima Lesurwai.

Wamemuomba Rais Magufuli awasaidie kama alivyowasaidia wananchi wa mkoani Katavi ambao aliamuru wasiondolewe kwenye ardhi yao ambayo tayari mahakama ilikuwa imeshaamuru wananchi hao zaidi ya 1,200 waondolewe.Aidha wamemuomba awanusuru kwa kuamuru wanaostahili fidia walipwe kwa thamani halisi ya mali na wale walio maeneo nje ya mita 100 wasibugudhiwe.

Wananchi hao waliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati walipokusanyika pembezoni mwa mlima Lesurwai yalipo makazi yao kujadili hatma yao.

Akisoma maazimio ya kikao hicho, Jeremea Jacob alisema kuwa kwa pamoja hawakubaliani na namna zoezi la kulipa fidia linaloendelea kwa sasa kwa kile walichodai kuwa limetawaliwa na utata mkubwa kwani tathmini hiyo ilifanyika mwaka 2012 na kutokana na jeshi kuchelewa kurudi kulipa fidia kwa miaka mingi waliamua yaendeleza maeneo hayo na mengine kuwapa watoto wao wakayaendeleza jambo ambalo halijazingatiwa kwenye fidia inayolipwa.

Aidha wamedai kuwa kuna mkanganyiko umejitokeza kwenye orodha ya fidia ambapo kuna baadhi ya wananchi wa kata ya Mlangarini majina yao yanaonekana kwenye orodha ya wakazi wa Moshono hivyo kutakiwa kwenda kulipwa kwenye halmashauri ya jiji la Arusha wakati kiuhalisia hawako jiji.
Alisema hali hiyo ilimlazimu aliyekuwa mkurugenzi wa halamshauri ya wilaya ya Arusha, Dk  Wilson Mahera ambaye kwa sasa ameteuliwa kuaa mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusitisha zoezi la ulipaji fidia.

Jacob alisema kuwa kwa upande wa jiji la Arusha zoezi la ulipaji fidia limetawaliwa na urasimu wa hali ya juu kwa kile alichodai kuwa  mwananchi akifika kwenye chumba namba 52 ambacho kinashughulika na kulipa fidia akiuliza kiwango anachopaswa kulipwa haambiwi zaidi anaambiwa atoe namba za akaunti ya benki atakuta hela zake.

Alidai  kuwa kuna wananchi ambao wamejenga nyumba kwenye maeneo hayo lakini wamejikuta wakilipwa fidia ya shilingi laki tatu ambayo haimtoshelezi hata kulipia kodi ya pango ya nyumba ya kuishi na familia yake kwa mwaka mzima kulingana na kodi za pango zinazotozwa kwenye jiji la Arusha kwa sasa.

HOFU YATANDA WANANCHI WALIOPAKANA NA ENEO HILO

Aidha wakazi wengine waliopakana ya eneo hilo la mita 100 wameelezea hofu yao kuwa huwenda maeneo yao yakachukuliwa na jeshi kwani baadhi ya wananchi waliopakana nao wapo kwenye orodha ya fidia wakati eneo lao halihusiki.

Wananchi hao ambao wengine ni watumishi wa serikali walihofia majina yao kuandikwa gazetini alisema kuwa waliponunua hayo maeneo walifuata taratibu zote kwa kushirikisha ofisi ya kijiji mpaka kupata vibali vya ujenzi
hawakuwahi kuelezwa ni maeneo ya jeshi. Walisema kuwa maeneo yao yako karibu na nguzo za umeme na reli ambapo ni mbali kabisa na eneo la mita 100 na maeneo ambayo yanamilikiwa na jeshi.

AELEA JK ALIVYOWAPA ARDHI HIYO

Akiongea kwa niaba ya wenzake, Jacob alieleza historia ya mgogoro huo alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete alirejesha kwa wananchi zaidi ya ekari 6,000 ambapo eneo la mita 100 kuzunguka mlima Lesurwai liliombwa kwa ajili ya matumizi ya jeshi." Mwaka 2012 ilifanyika tathmini  kwa mtu mmoja ambaye ni baba, kwa kuwa
hatujapewa fidia na muda ni mrefu umepita baba amegawa eneo kwa watoto wamejenga nyumba za kuishi " alisema Jeremiah na kuongeza.

"Sasa leo jeshi wamerudi wanalipa fidia na wanawatambua watu walewale waliofanyiwa tathmini mwaka 2012 hawataki kuwatambua waliouziwa na waliogaiwa na wazazi kisha wakaendeleza,".Mwananchi mwingine ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa hakuna mwananchi aliyekataa kupisha kwenye eneo la mita 100 ili Jeshi walitumie tatizo ni fidia ndogo na ya isiyotolewa kwa uwazi.


"Na JPM (Rais John Magufuli) hajui hii kitu, Rais wetu ni msikivu na hapendi wanyonge tunyanyaswe tunamuomba aingilie kati ili haki yetu
isipotee. Hakuna mwananchi aliyevamia eneo la Jeshi bali wananchi tuko kwenye maeneo yetu tunasubiri fidia ili jeshi waweze kuyatumia," alisema Jacob

Wananchi walioathiri na tatizo hilo ni kutoka vitongoji vya Lesurwai na Chekereni vilivyopo kata ya Mlangarini na mtaa wa Lesurwai na Tanganyika Packers kwa upande wa kata ya Moshono iliyopo jiji la Arusha. Walidai kuwa kutokea mwaka 2012 kulipofanyika tathmini mpaka sasa ni miaka saba imepita na ni kipindi kirefu mno hali iliyowalazimu baadhi ya watu waliokuwa wakiumwa kuuza maeneo yao wakatibiwe na wengine waliuza ili kupata fedha za kulipia ada watoto wao walio vyuo vikuu.

Alisema changamoto iliyopo ni wahakiki hawataki kuwatambua hao waliouziwa maeneo na kuyaendeleza hivyo aliiomba serikali itambue hao wananchiwatambuliwe na walipwe fidia.

MKURUGENZI WA JIJI ANENA

Mkurugenzi wa jiji alikanusha madai ya zoezi hilo kufanywa kwa usiri hata kwa usika wenyewe kwa kike alichofafanua kuwa wananchi hao wanataka utishwe mkutano halafu itangazwe kila mtu analipwa kiasi gani jambo alilosema haiwezekani."Tunachofanya sisi tunawataka wafike na barua zao na utambulisho vyao kwenye ike orodha tunafunika majina ya watu wengine tunauonyesha la kwake na taarifa za kiasi anachopaswa kulipwa," alisema

Kuhusu suala la wananchi walio halmashauri ya wilaya ya Arusha kulipwa na upande wa jiji la Arusha halina athari yoyote kwa mthamini ni mmoja na anayelipa fedha ni wizara ya Ulinzi hivyo haiwezi kuwa na shida.
Hata hivyo alisema kuwa suala la mpaka kusogezwa halina ukweli mpaka uko palepale mita 100 kuzunguka mlima Lesurwai.

JESHI LATOA MSIMAMO

Akijibu malalamiko hayo, mkuu wa kambi 977, Luteni Kanali, Hamis Kinguye alikanusha jeshi kujiongezea maeneo kwa kile alichofafanua kuwa wao wanamiliki maeneo hayo kihalali na kuwa kwenye maeneo hayo ya mita 100 yalipimwa na kuwekewa mipaka lakini wananchi waliamua kung'oa bikoni. "Kimsingi hatujavamia maeneo ya wananchi ila tuko kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya jeshi kikosi 977 ambalo kutoka kwenye mlima na zile mita100. Ziko bikoni ambazo wao (wananchi) wenyewe wameziondoa kwa sababu zao binafsi," alisema Luteni Kanali Kinguye.

Alisema kuwa walitathminiwa na mwezi April walikuja wataalam kuwahakiki wananchi waliokuwa kwenye mita 100 kutoka kwenye mlima  ambapo waliohakikiwa malipo yao yamekuja sasa hivi ni masuala ya kwenda kuchukua hayo malipo ili maelekezo mengine yaweze kutolewa.

"Ramani ya mwanzo ilionyesha nguzo za umeme ni eneo la jeshi. Kwenye  reli ni eneo la serikali ambalo hatupaswi kufanya shughuli yoyote na kuna eneo la nguzo za umeme ni eneo la serikali," alifafanua Luteni Kanali Kinguye akijibu malalamiko kuwa wamevamia eneo hilo toka kwa wananchi


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...